Mijadala ya maendeleo ni muhimu katika ukuaji wa taifa letu

Jamii Africa

KWA mujibu wa nadharia kuhusu maendeleo, nchi yoyote haiwezi ikaendelea bila ya kuwa na mijadala juu ya mielekeo mbalimbali ya maendeleo. Jukumu mojawapo la wasomi wa kitanzania ni kuchochea na kuongoza mijadala” – Edward Moringe Sokoine.

Kwa kurejea maneno hayo hapo juu kutoka kwa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania chini ya Serikali ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni dhahiri ya kuwa tuna mengi ya kujifunza na kutafakari.

Tanzania yetu imepitia vipindi mbalimbali vya ukuwaji na kila kipindi kina changamoto zake ambapo kila kipindi kinapaswa kuwa msingi bora katika kujenga nchi kuelekea taifa bora zaidi. Tukitizama kwa ukaribu zaidi tutagundua ya kuwa katika karne hii ya ishirini na moja kuna ukuwaji wa technologia yenye kufanya mawasiliano kuwa marahisi zaidi katika kuboresha mijadala mbalimbali.

Hili ni Daraja la Kashahanzi katika barabara ya Tunduma –Sumbawanga. Kujengwa kwa barabara ya Tunduma – Sumbawanga kumechochea maendeleo katika mikoa ya Mbeya, Rukwa na Katavi.

Vivyo hivyo, karne hii ya ishirini na moja inakumbwa na changamoto lukuki ambazo zilipaswa kuwa zimetatuliwa hapo zamani na kusahaulika na sasa tuendelee kutatua changamoto zilizopo. Ila ukweli unabaki ya kuwa, maadui wale watatu ambao serikali ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilianza kupigana nao ambao ni ujinga, maradhi na umasikini mapaka leo wapo tunaendelea kupambana nao ila sio kwa mafanikio makubwa sana.

Jaribu kutafakari hapo ulipo je, huduma za afya, elimu, kilimo, viwanda na nyinginezo nyingi zina hali gani? Je, leo ni afadhali kuliko jana? Ama je, kuna kesho njema unayoweza kuiona?

Haya ni baadhi ya maswali ambayo unaweza kujiuliza ila majibu yake yanaweza kuwa tofauti kutokana na tabaka ulilopo kama unatoka kwenye tabaka la walalakheri unaweza kuwa na majibu bora zaidi ila kama unatoka kwenye tabaka la walalahoi majibu yako yanaweza yasiwe ya kufurahisha.

Nimeona ni vyema tuanze na tafakuri hii ndogo kabla ya kwenda kwenye msingi wa makala hii unaolenga kuangalia umuhimu wa mijadala katika kuleta maendeleo ya taifa letu. Katika wakati huu wa soko huria ambapo huduma za jamii zimegeuka kuwa bidhaa ya ghali sokoni ambapo wenye nacho ndo hunufaika kuliko sie walalahoi. Hii inamaanisha changamoto zinaongezeka kila kukicha kuliko kupungua kwani pengo la walionacho na wasionacho nalo huongezeka kila kukicha.

Hapa ndipo umuhimu wa mijadala hujitokeza ili kuweza kuwapa wananchi fursa ya kubangua bongo zao na kuweza kufikiri kwa pamoja nanma ya kutatua matatizo yao. Ni ukweli kwamba hakuna ayajuaye matatizo zaidi ya yule anayeyaishi kila siku na yule ayaishie matatizo hayo ndiye ajuaye suluhisho ya matatizo hayo kwani hutumia njia mbalimbali kukabiliana nayo.

Tatizo nilionalo mimi katika muktadha huu ni kwamba, mijadala inakosa nguvu kwani wataalamu wachache hufikri wao ndio wenye kuweza kuleta suluhisho bora kuliko kuwashirikisha wananchi. Na sio kweli kwamba wataalamu hawa hawajui umuhimu wa kuwashirikisha wananchi ila wanachagua kutofanya hivyo na mijadala inabaki kama nadharia tu ila katika uhalisia mambo hufanywa tofauti kabisa.

Hebu turejee mifano michache tu ambayo kwa hivi karibuni tumeishughudia ambapo tunaona viongozi mbalimbali wa serikali wanapopata fursa ya kutembelea wananchi hutumia muda huo kufanya nao mijadala mifupi ambapo wananchi hao huweza kutoa taarifa mbalimbali ya muenendo ya maisha yao na viongozi wao. Hapa ndipo tunapoona viongozi hao wakichukua hatua aidha kwa kuwasimamisha kazi wahusika ama kuhakikisha huduma stahiki inapatikana.

Kwa mfano huu, je, taifa letu halitafika mbali kama wananchi watapata fursa ya kujadili kwa uwazi yale yanaowasibu na suluhisho ya kile ambacho kitaweza kuwafaa? Isitoshe, kupata maendeleo bora ni kwa kuwashirikisha wananchi ili wawe sehemu muhimu ya maendeleo endelevu na sio kutenda kwa niaba yao.

Mijadala hii ina nguvu kubwa kwani huleta watu pamoja na kutizama jambo katika upana wake, japo mara nyingine katika mijadala hii tunaweza kusikia ukweli mchungu ila hii ndio nguvu ya mijadala na haipaswi kuogopwa kana kwamba inatishia amani ya nchi ama sehemu husika. Kuweza kupata maendeleo sio kwa kusikia hoja za kufurahisha tu pia tunaweza kusikia hoja za kuudhi ambazo zitatufanya tujitafakari na kufikia suluhisho endelevu.

Changamoto nyingi tulizonazo hazifanikiwi kwa kuwa suluhizo za changamoto hizo hazitokani na sisi wenyewe kwani hutoka katika nchi za Magharibi na Marekani kwa mfumo wa MKURABITA, MKUKUTA, MDGs, SAPs na SDGs ambazo hizi ni nadharia kutoka kwa wataalamu wa nchi nyingine ambao hupenda kuja kuzijaribu katika nchi zetu za Afrika.

Mipango hii kutoka nchi za nje inashindwa kueleweka na wananchi na viongozi wengi pia ndo maana utekelezaji wake huwa mgumu sana. Ila ingalikuwa mipango hii inatokana na sisi wenyewe basi ingekuwa rahisi sana kufanikiwa katika utekelezaji wake.

Mtu anaweza kuwa anatafakari tufanyeje ili tuweze kuja na mipango yetu wenyewe ya maendeleo na tuachane na hiyo ya kutoka nje?

Katika kitu nachoweza kujivunia kwa nchi yetu ya Tanzania ni namna uongozi ulivyotapakaa katika kila kona ya nchi hiii kuanzia balozi wa nyumba kumi mpaka kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kupita viongozi wetu hawa katika ngazi ya chini kabisa tunaweza kufanya mijadala katika kila ngazi ya uongozi na wananchi wake kujadili maswala mbalimbali kuanzia afya, elimu, kilimo, viwanda, miundombinu na mengine mengi na hatimaye mapendekezo hayo yakakusanywa na kutengeneza mpango wa pamoja.

Kuwa na viongozi wabunifu wasiosubiri kuambiwa nini cha kufanya kutasaidia kuleta mipango bora ya maendeleo inayotokana na mijadala na wananchi husika.

Nimalize kwa kusema, matatizo ya sehemu husika yanatatuliwa na watu wa sehemu husika na sio kuazima mipango mingine isiyoweza kuakisi ukweli husika.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *