Miundombinu duni, kikwazo cha kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga Tanzania

Gordon Kalulunga

Sera ya afya ya mwaka 2007 inaeleza mipango madhubuti ya kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana katika kila kata ambapo kila kijiji inatakiwa kuwe na Zahanati na kila kata kuwe na kituo cha afya na wataalamu wenye taaluma.

Sera hiyo inaeleza pia kuwa serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine yakiwemo mashirika mbalimbali itahakikisha kuwa katika sehemu hizo za kutolea huduma za afya kutakuwa na mazingira mazuri na vifaa tiba.

Neno mazingira ni neno pana sana, linajumuisha hewa, ardhi, maji, mimea, maisha ya wanadamu na wanyama ikiwa ni pamoja na mienendo na tabia za jamii na jinsi wanavyohusiana.

Lakini katika baadhi ya zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, mikoa na hata hospitali za rufaa hali haipo hivyo nchini.

Kuna uhaba mkubwa wa maji, tatizo la umeme ambapo kutokana na mfumo wa serikali kuamua kutumia Luku hospitali nyingi wanapata shida hasa wakati wa upasuaji(Oparation) huku wakihofia unit kuisha maana ukinunua umeme mwingi na hata makato wakati wa kununua tena yanakuwa makubwa zaidi na bajeti hazitoshi.

Katika kituo cha afya cha Manyamanyama Wilayani Bunda mkoani Mara wataalam akiwemo muuguzi mkuu wa hospitali hiyo Adelaida Masige anasema kuwa ni vema serikali ikabadili mfumo huo wa Luku katika hospitali zinazotoa huduma za upasuaji.

‘’Mfumo huu wa Luku haufai hasa katika hospitali tunazotoa huduma za upasuaji maana unit zikiisha ukiwa katika chumba cha upasuaji ni hatari kubwa kwa mgonjwa’’ anasema Adelaida.

Mjamzito Nyangeta Makori mkazi wa kijiji cha Nyambono wilaya ya Musoma vijijini, kutokana na usafiri unaofaa kwa mjamzito kutokuwepo, alilazimika kukodi pikipiki na kupita katika barabara mbovu kwa saa nne, huku akisikilizia uchungu kutoka Msoma vijijini mpaka Kituo cha afya cha Manyamanyama wilaya ya Bunda.

Alitoka saa 8;30 nyumbani kwake na kufika saa 11:30 jioni kisha kupokelewa katika kituo cha afya cha Manyamanyama, baada ya muda wa saa moja alijifungua mapacha, Doto akiwa na kilo 3.1 na Kulwa naye ana kilo 3.5.

Nyangeta anasema huu ni uzao wake wa tano ana watoto sita wote wakiume, watoto wa nne amejifungulia nyumbani akisaidiwa na wifi yake kwa kumshika sehemu ya mgongo wakati wa kujifungua na yeye kusukuma na kutoa mtoto.

Kitu kinachosababisha Nyangeta kuzalia nyumbani watoto wanne ni kijiji anachokaa hakuna zahanati na hospitali iko mbali.

Wifi yake Nyangeta ambaye tunaweza kumwita shujaa, amemuokoa Nyangeta asipoteze maisha kwa kumshawishi kwenda katika kituo cha afya kujifungua pamoja na kumsindikiza kutoka musoma vijijini mpaka Bunda, lakini pia ndiye mwanamke aliyemsaidia kujifungua nyumbani watoto wanne.

Huyo ni mmoja wa wajawazito Tanzania wanaokumbana na shida wakati wa kutafuta huduma za kujifungua ikiwa pamoja na umbali, usafiri usio wa uhakika, umasikini na barabara mbovu.

Kwa mujibu wa utafiti wa masuala ya afya ya uzazi ya Kitaifa wa serikali mwaka 2010(TDHS) unaeleza kuwa kila siku wajawazito 23 wanapoteza maisha kwa matatizo mbalimbali ya uzazi wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.

Zahanati ya Bunda, ni moja ya zahanati zinazokumbwa na changamoto ya miundombinu ikiwemo ya chumba cha kuchomea sindano wagonjwa kukosa madirisha!.

Msaidizi wa mganga wa zahanati ya Bunda Victoria Awino anasema kuwa hiyo ni changamoto kubwa katika zahanati yao.

‘’Tatizo kubwa la miundombinu ni pamoja na chumba cha kuchomea sindano wagonjwa kutokuwa na dirisha na sehemu ya mapokezi pia hatuna dirisha na nyumba za watumishi ni tatizo’’ anasema Victoria Awino.

Zahanati hiyo inahudumia wagonjwa kati ya 30 mpaka 40 kwa siku.

Katika kijiji cha Kambubu kata ya Nyamang’uta wilayani humo baadhi ya wananchi wamemuomba waziri wa nchi uratibu wa sera na Bunge Stephen Wasira kuokoa wajawazito katika kijiji cha Kambubu kutokana na kukosa imani na kituo cha afya cha Ikizu maarufu kama Nyamuswa.

Wanasema katika kituo cha afya cha Ikizu kumekuwa na manyanyaso makubwa kwa wajawazito huku wakitozwa gharama kubwa za kujifungua huku mazingira na miundombinu ya chumba cha kujifungulia ikiwa haina utu.

Kijana Samson James anasema kuwa wanalazimika kwenda katika kituo hicho cha afya kwa ajili ya kupata vipimo tu.

‘’Tunaenda Nyamuswa kwa ajili ya kupata vipimo na dawa huwa tunanunua maduma ya dawa na endapo katika maduka ya dawa kungekuwa na vipimo tusingethubutu kwenda huko’’ anasema Samsoni.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kambubu Warioba Kiharata anasema ili kupata huduma bora za afya katika kituo cha afya cha Ikizu hasa kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kama huna fedha basi ni lazima utambike.

‘’Huduma za afya ni shida na pale Nyamuswa ni za kutambikia na hapa hatuna zahanati, ukiwaambia kuwa wakusaidie mkeo anaumwa wanakuuliza kuwa sasa wao wafanyeje!’’ anasema Kiharata.

Anasema kutokana na hali hiyo, wananchi wamehamasishana kujenga zahanati ya kijiji chao na tayari wamekusanya mchanga na mawe na kwamba hata Mbunge wao Stephen Wasira anayo taarifa hiyo lakini bado hawajaruhusiwa kujenga kwa miaka zaidi ya mitatu sasa.

‘’Kwa sasa katika kijiji chetu tunasubiri kibali cha kujenga zahanati ambapo wanaotukwamisha ni serikali hawataki kutupa ramani’’ anasema Mwenyekiti huyo.

Mjamzito Agnes Baraka anasema wajawazito wanaopata huduma bora hospitalini ni wale wenye uwezo wa kifedha na ambao hawana uwezo huo wanajifungulia nyumbani au kwa wakunga wa jadi.

‘’Kama mimba haina matatizo unaweza kutozwa Sh.7,500 baada ya kujifungua ili utoke hospitali, na baada ya kujifungua mtoto akiumwa mapokezi ni Sh3,000, daftari 300 hapo bado gharama za vipimo na wenye bima ya afya ya jamii(CHF) wanapimwa bure lakini dawa wananunua’’ anasema Agness.

Anna Japhet(35) anasema kuwa wakunga wa jadi wanatoa huduma bure na wale wanaotoza fedha ni Sh. 3,000 tofauti na hospitalini ambako mjamzito analazimika kununua karatasi, gaharama za kitanda, na mafuta ya taa 1,000.

Diwani wa kata hiyo Kelemba Jonathan Ilubi anasema ujenzi wa zahanati katika Kijiji cha Kambubu anajua nguvu kubwa waliyoitumia wananchi lakini hawapati ushirikiano kutoka serikalini licha ya yeye pia kupigania ujenzi wa zahanati hiyo.

‘’Wananchi wamejitolea kwa kiasi kikubwa lakini hakuna utekelezaji kutoka serikalini na Mbunge Wasira anakwamishwa maana alishatoa Shilingi Mil.2 lakini mahitaji kamili ya ujenzi wa zahanati ni Mil.60’’ anasema Diwani Ilubi.

Kituo cha afya cha Ikizu hakina gari wala pikipiki kwa ajili ya wagonjwa hivyo hali hiyo inawalazimu wagonjwa wakiwemo wajawazito wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji kukodi pikipiki ili kupelekwa hospitali teule ya wilaya niliyopo umbali wa kilomita 25.

‘’Tunalazimika kukodi ‘’Toyo’’ au ‘’michomoko’’ tax kwa Sh.30,000 ili kuwapeleka wagonjwa ‘’DDH’’ hospitali ya wilaya’’ walisema baadhi ya wananchi ambao waliomba hifadhi ya majina yao.

Mganga mkuu kiongozi wa kituo hicho cha afya cha Ikizu kilichopo eneo la kata ya Nyamuswa tarafa ya Ikizu Dr.Abahehe Kanora, anasema kuwa kituo hicho hakina gari la wagonjwa na walitegemea kuwa Rais Jakaya Kikwete angewapelekea kutokana na ahadi yake alipokuwa akiomba kura kwa wananchi wa eneo hilo mwaka 2010.

‘’Hapa kulikuwa na gari Pick up lakini iliuzwa na kuharibika mwaka 1996 na wilaya ina ambulance moja tu, tegemeo letu kubwa pamoja na wananchi ilikuwa ni kutimia ahadi ya Rais Kikwete ambapo aliahidi pale njia panda kwenye mti wa kumbukumbu ya Chifu Makongoro aliposimamishwa na wananchi mwaka 2010’’ anasema Dr. Kanora.

Alipoulizwa kama wajawazito na watoto hupatiwa matibabu bure kama inavyoelekezwa na sera ya afya ya mwaka 2007 ili kupunguza vifo vya makundi hayo, alisema kuwa kwanza hakuna dawa zinazopelekwa maalumu kwa ajili ya makundi hayo.

Kuhusu maji anasema mpaka sasa kuna tatizo kubwa la maji na kila mgonjwa wakiwemo wajawazito lazima aende na ndugu yake ambapo baadhi ni lazima waende na maji eneo la kituo hicho cha afya.

Kituo hicho licha ya kukabiliana na hali hiyo ya miundombinu na mazingira,familia mbili za watumishi wa kituo hicho hawana vyoo na kulazimika kujisaidia katika choo cha wagonjwa kilichopo umbali wa mita 25 baada ya choo walichokuwa wakichangia kubomoka.

Katika hospitali ya Butiama, chumba chenye dirisha moja kina vitanda kumi na hewa ni ndogo na wanawake wajawazito wanalazimika kutumia choo cha nje kilichopo umbali wa mita thelathini hali ambayo ni hatari na wanaweza kujifungulia chooni.

Pia kuna ukosefu wa miundombinu ya kutosha zikiwemo wodi za watoto, wanawake na wanaume katika hospitali ya Butiama.

Hicho ni moja ya kielelezo tosha kuwa lengo la milenia la kupunguza vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kufikia vifo asilimia 75 kati ya vizazi hai 100,000 Tanzania haitatekelezeka.

Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dr. Joseph Musagafa anasema kuwa kwa sasa hospitali yake ina upungufu wa nyumba za watumishi, mawodi ya watoto, wanawake na wanaume.

‘’Nyumba za watumishi tunazo 14 wakati mahitaji ni 20, mawodi hayatoshi ambapo wodi moja ya wanawake, watoto na wanaume ni sawa na chumba kimoja cha mgonjwa staff na vyoo vipo vine wakati mahitaji ni vyoo sita’’ anasema Dr. Musagafa.

Kuhusu miundombinu, anasema hospitali hiyo ina wodi moja ya wanaume yenye vitanda kumi tu, wodi mbili ya wanawake na wodi mbili za watoto zenye vitanda kumi kila moja ambapo chumba cha wauguzi kinatumika kama chumba cha wagonjwa mahututi.

Anasema mawodi hayo yakipanuliwa mahitaji sahihi kwa upande wa vitanda vinahitajika 20 kwa kila wodi na visibanane kama ilivyo hivi sasa na kuwe na ukubwa mzuri wa vyumba ili kutenganisha wagonjwa badala ya kuchanganywa kama ilivyo hivi sasa.

‘’Hatuna miundombinu mizuri ya maji na tunategemea maji ya mvua na maji ya kupampu yaliyoelekezwa kwenda nyumbani kwa Mwalimu Nyerere’’ anasema Dr. Musagafa.

Dr. Musagafa anataja sababu zinazosababisha vifo kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano katika wilaya hiyo kuwa ni pamoja na upungufu wa damu, kuchelewa kufika hospitalini, kununua dawa madukani kabla ya kupima, kwenda kwa waganga wa jadi, usafiri duni na miundombinu mibovu, uchumi mdogo na ukosefu wa elimu ya afya.

Anakiri kuwa wajawazito wengi wanajifungulia nyumbani kutokana na sababu mbalimbali huku akitolea mfano kuwa umbali ni kikwazo pia ambapo wananchi wanaoishi katika maeneo ya Bugoji, Majila na Bulangi wapo mbali na hospitali.

‘’Wananchi hao wanaishi zaidi ya kilomita 100 hivyo kusafiri kuja hospitali kwa ajili ya kujifungua labda iwe rufaa ya kufanyiwa upasuaji maana jiografia ni mbaya na hakuna usafiri wa uhakika hivyo wengi wanaamua kujifungulia nyumbani’’ anasema Dr. Musagafa.

Naye muuguzi kiongozi wa hospitali hiyo Neema Muchunguza anasema kuwa kila mwezi zaidi ya wanawake 100 hujifungulia katika hospitali hiyo hivyo serikali inapaswa kufanyia kazi mapungufu na upanuzi wa miundombinu ya hospitali hiyo ya wilaya.

Mwandishi wa makala hii anapatikan kwa simu 0754 440749

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *