Miwa ya Mkulazi kuiondoa Tanzania kwenye kundi la nchi zinazoagiza sukari nje

Jamii Africa

UAGIZAJI wa sukari nje ya nchi unaweza kuwa historia mara baada ya kuanza kwa mradi mkubwa wa kilimo cha miwa katika eneo la ukubwa hekta 40,000 kwenye Kijiji cha Mkulazi, Tarafa ya Ngerengere wilayani Morogoro.

FikraPevu imeelezwa kwamba, kilimo hicho cha miwa kinaambatana na ujenzi wa kiwanda kikubwa cha sukari ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 200,000 za sukari kwa mwaka na kutoa ajira 100,000, hivyo kupunguza pengo la tani 120,000 ambalo limekuwa likiikumba Tanzania kila mwaka kiasi cha kulazimika kuagiza sukari nje ya nchi, uagizaji ambao mara kadhaa umekuwa ukidaiwa kugubikwa na ufisadi na hujuma.

Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Kilimo Kwanza kupitia Mpango wa kuendeleza Kilimo wa Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).

FikraPevu inafahamu kwamba, licha ya kuendelea kwa ukarabati wa barabara ya Ngerengere – Mkulazi yenye urefu wa kilometa 61 kuelekea eneo la mradi, tayari uainishaji wa aina ya udongo umekwishaanza kufanywa na Taasisi ya Kilimo ya Mlingano katika eneo lenye ukubwa wa hekta 63,200.

Kampuni ya Shirika la Uchumi na Maendeleo ya Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) ndiyo inayokarabati barabara hiyo, ambayo iliharibika muda mfupi tu baada ya kujengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro mwaka 2011.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango vimedokeza kwamba, taratibu za fidia kwa wananchi walio ndani ya eneo la mradi zinaendelea ili kupisha ujenzi wa miundombinu mara baada ya wazabuni kupatikana.

Taarifa ambazo FikraPevu inazo zinasema katika Mwaka wa Fedha 2016/2017 Serikali ilitenga Shs. 17 bilioni kwa ajili ya kumalizia fidia na mipaka kwa wakazi wanaoishi kwenye shamba hilo ambalo zamani lilikuwa la umma.

Kukamilika kwa mradi huo kutawezesha kukidhi mahitaji ya ndani na kuuza nje ya nchi pamoja na bidhaa ambatano ikiwemo ethanol.

Utekelezaji wa mradi huo mkubwa ambao unasimamiwa na kampuni ya ubia ya Mkulazi Holding Co. Limited iliyoundwa na kwa pamoja na mashirika ya mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF na PPF, unahusisha pia eneo la hekta 20,000 la mashamba ya mpunga na hekta 3,200 za wakulima wadogo.

FikraPevu inatambua kwamba, Taasisi ya Kilimo Mlingano ilishinda zabuni hiyo namba PA/004/2016-17/HQ/CS/14 yenye thamani ya Shs. 122,142,400.00 iliyotolewa na NSSF kwa njia ya Uteuzi wa Pekee (Individual Selection) mnamo Januari 12, 2016.

Mnamo Desemba 19, 2016 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenister Mhagama, wakiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Stephen Kebwe, Mbunge Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Omari Mgumba, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyalala na Mkurugenzi Mkuu wa PPF Wilson Elio, walitembelea eneo la mradi na kujionea ukarabati wa barabara pamoja na eneo patakapojengwa kiwanda.

Upatikanaji wa sukari

Kwa miaka mingi sasa Tanzania imekuwa ikikumbwa na tatizo la uhaba wa sukari licha ya kuwepo kwa viwanda vinne vikubwa ambavyo ni Mtibwa, Kilombero, Kagera na TPC cha Arusha-Chini mkoani Kilimanjaro.

FikraPevu inatambua kwamba, uwezo wa viwanda hivyo vyote kwa pamoja ni kuzalisha wastani wa tani 300,000 kwa mwaka wakati mahitaji halisi ni tani 420,000 kwa mwaka, hivyo kuwepo kwa pengo la tani 120,000.

Taarifa kutoka Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo zinasema kwamba, mahitaji ya matumizi ya sukari kwa nyumbani na viwandani ni wastani wa tani 590,000 kwa mwaka, hatua ambayo inaonyesha kwamba, kwa uzalishaji wa sasa wa viwanda vinne kumekuwepo na upungufu wa jumla ya tani 290,000, ikihusisha tani 120,000 za matumizi ya nyumbani na tani 170,000 za matumizi ya viwandani.

FikraPevu inafahamu kwamba, matumizi ya sukari kwa Tanzania yenye wakazi takriban milioni 50 ni madogo ikilinganishwa na nchi jirani ya Kenya yenye wakazi milioni 44, ambako matumizi ya sukari ni tani 800,000 kwa mwaka.

Aidha, usambazaji wa sukari iliyopo nao umekuwa na utaratibu mbovu, hatua ambayo mara kadhaa inadaiwa kuwafanya wazalishaji na wenye viwanda kuficha kiwango kikubwa cha sukari kwenye maghala kwa hila ili serikali iwape kibali cha kuagiza sukari nje ya nchi isiyolipiwa ushuru, hivyo kuwanyima huduma wananchi pamoja na kuikosesha serikali mapato.

Mwaka 2014 katika Mkutano wa Wadau wa Sukari nchini uliofanyika mjini Morogoro, aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Injinia Christopher Kajolo Chiza, alisema kwamba serikali ingechukua hatua kadhaa ikiwemo kuimarisha usimamizi wa Sheria ya Sekta ya Sukari ya mwaka 2001 ili kuhakikisha kuwa utaratibu mzima wa uingizaji sukari nchini unazingatiwa.

“Serikali itaimarisha udhibiti wa sukari inayoingizwa nchini kwa njia ya magendo pamoja na kuhakikisha kuwa sukari inayoagizwa na nchi jirani kupitia bandari zetu (transit sugar) haipenyezwi kuuzwa katika soko la hapa nchini,” alisema Chiza.

Aidha, alisema pia serikali ingesimamia mfumo mzima wa usambazaji wa sukari nchini ikiwa ni pamoja na kuwadhibiti wafanyabishara wenye tabia ya kuhodhi soko la sukari kwa lengo la kusababisha upungufu usio halisi wa sukari (artificial shortage).

Licha ya baadhi ya jitihada hizo kufanyika, lakini FikraPevu inatambua kwamba, tatizo la uhaba wa sukari nchini limekuwa sugu na mara kadhaa limetikisa uchumi wa nchi.

 Ukubwa wa Mradi

Eneo hilo la Mkulazi lililoko umbali wa kilometa 60 kutoka barabara kuu ya Dar es Salaam – Morogoro pembezoni mwa Reli ya Tazara linaelezwa kuwa linafaa kwa kilimo cha miwa na mpunga kwa kutumia Mradi wa Bwawa la Kidunda na kwamba miradi hiyo itakapoanza itasaidia kuleta uhakika wa akiba ya chakula pamoja na kupunguza uhaba wa sukari nchini.

Uhawilishaji wa Shamba la Mkulazi lililogawanywa katika mashamba sita utakuwa wa miaka 66, kwa mujibu wa taarifa za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu, Jenister Mhagama (wa pili kulia) na Waziri wa Fedha na Mpango, Dr. Phillip Mpango (wa tatu kulia) walipotembelea bwawa la Kidunda lililopo kijiji cha Kidunda, kata ya Mkulazi, wilaya ya Morogoro Vijijini. Mawaziri hao walipokea ombi la kuwezesha ujenzi wa daraja litakalounganisha kijiji hicho na Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani ili kurahisisha mawasiliano baina ya mikoa hiyo miwili.

Mgawanyo wa mashamba hayo unaonyesha kwamba, mashamba ya miwa yatakuwa mawili yenye ukubwa wa jumla ya hekta 40,000 kila moja likiwa na hekta 20,000 (Shamba Na. 217/1 na Shamba Na. 217/2).

FikraPevu inafahamu kwamba, kilimo cha mpunga kitakuwa kwenye mashamba manne huku kila moja likiwa na ukubwa wa hekta 5,000 ambayo ni Shamba Na. 217/3, Shamba Na. 217/4, Shamba Na. 217/5, na Shamba Na. 217/6.

Tunachokijua FikraPevu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu,  Jenister Mhagama (kushoto) na Waziri wa Fedha na Mpango, Dkt. Phillip Mpango (katikati) wakimsikiliza Mbunge Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki Omari Mgumba (kulia) ambae jimboni kwake ndipo unatekelezwa  mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda hicho.

Washirika muhimu! Wakurugenzi wakuu wa mifuko hifadhi ya jamii ya NSSF na PPF,  Profesa Godius Kahyarara (kulia) na Bw. William Erio (kushoto) wakisikiliza hotuba ya  Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu,  Jenister Mhagama alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kidunda, kata ya Mkulazi, wilaya ya Morogoro Vijijini mwishoni mwa wiki.

FikraPevu inafahamu kwamba, NSSF kwa niaba ya Mkulazi Holdings Co. Limited iko katika mchakato wa kutafuta mzabuni Mshauri Mwelekezi kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu kwenye Mradi wa Shamba la Mkulazi Namba 217.

Kwa mujibu wa zabuni Namba PA/004/2016-2017/HQ/CS/13 iliyotangazwa Oktoba 10, 2016, Mshauri huyo mwelekezi, pamoja na mambo mengine, anatakiwa kushauri namna bora ya umwagiliaji na kiasi cha maji ambacho kinatakiwa kuhifadhiwa.

“Mshauri huyo atashauri mfumo wa umwagiliaji utakaotumika iwe ni kuhifadhi maji shambani kwa umwagiliaji, kujenga miundombinu kama mifereji ya maji na barabara, umeme na kujikinga na mafuriko,” yanasema maelezo kwenye tangazo la zabuni hiyo ambayo FikraPevu inayo nakala yake.

Awali, bilionea namba moja Afrika, Alhaj Aliko Dangote, alikuwa akitajwa kwamba huenda angejitosa kwenye uwekezaji katika shamba hilo baada ya zabuni kutangazwa mwaka 2015 na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kutokana na kauli yake kwamba baada ya kuwekeza kwenye uzalishaji wa saruji, alikuwa anataka kugeukia kilimo, hasa cha miwa.

Wakati wa uzinduzi wa kiwanda chake cha saruji mkoani Mtwara Oktoba 12, 2015, Dangote mwenyewe alikaririwa akisema kwamba kampuni yake imedhamiria kuwekeza kwenye kilimo na kwamba majadiliano baina yake na serikali ya Tanzania kuhusu kuanza uzalishaji wa miwa na mpunga yanaendelea.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *