Waziri awataka wakulima kutumia mbaazi kwa chakula kukabiliana na anguko la bei

Jamii Africa

Kutokana na kudorora kwa soko la nje la mbaazi, Serikali imewataka wakulima kutafuta na kuimarisha soko la ndani kwa kutumia kama chakula ili kujenga na kuimarisha afya za wananchi.

Msimamo huo wa Serikali umetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Eng. Stella Manyanya wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye ambaye alitaka kufahamu mkakati wa Serikali katika kuwatafutia wakulima soko la nje la mbaazi.

Nape amesema kuwa Serikali iliwaahidi wakulima wa mbaazi kuwatafutia soko baada ya wanunuzi wakubwa toka nchi za nje kama India kusitisha mkataba na Tanzania wa kununua zao hilo katika msimu uliopita.

“Msimu uliopita soko la mbaazi lilisababisha kuanguka kwa bei ya mbaazi kutoka Tsh. 2000 (kwa kilo) kwenda mpaka sh.150. Serikali iliahidi hapa Bungeni kwamba itahakikisha kwamba inahangaika kupata soko la kuaminika la zao hili. Sasa mmefikia wapi kupata soko la zao hili?,” ameuliza Mbunge Nape.

Naibu Waziri, Eng. Stella Manyanya amekiri kushuka kwa bei ya mbaazi katika msimu uliopita wa 2016/2017 kwasababu ya kutofikiwa kwa makubaliano ya kibiashara na wadau ambao walikuwa wananunua zao hilo kwa wingi.

“Ni kweli kabisa katika msimu huu ulioisha kulikuwa na hali isiyopendeza katika soko la mbaazi lakini hiyo inatokana na wadau kusitisha manunuzi ya mbaazi toka Tanzania”, amesema Naibu Waziri.

Kutokana na hali hiyo Serikali imewataka wakulima kuachana na soko la nje na kuwekeza nguvu zao katika soko la ndani kwasababu bado bei ya zao hilo ni nzuri katika baadhi ya masoko kinyume na hoja za baadhi ya watu kuwa soko la zao hilo limeporomoka.

“ Tunaendelea kusisitiza hata sisi wenyewe, mbaazi inauzwa mpaka kilo 2400 kwahiyo tusitegemee soko toka nje hata ndani ya nchi bado kuna soko la uhakika”, amesema Naibu Waziri.

             Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Eng. Stella Manyanya

 

Wakati huo huo amewataka watanzania kuchangamkia zao hilo kwasababu lina protini nyingi ambayo inahitajika mwilini. Ameongeza kuwa ikiwa ulaji wa mbaazi utaongezeka nchini, kuna uwezekano wakulima wakafaidika na soko la zao hilo.

“Mbaazi ni chakula ambacho kina protini na hata sisi wenyewe tunaweza tukawa soko kuliko kutegemea soko la watu wa nje”, amesema Naibu Waziri na kuongeza kuwa mbaazi inahitajika sana katika mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam ambako wakulima wanaweza kuuza huko ili kujipatia bei nzuri itakayosaidia kuinua kipato.

Msimamo wa Naibu waziri unaonekana kutofautiana na ule wa awali uliotolewa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage mwaka jana ambapo aliahidi kuwatafutia wakulima soko la mbaazi kwa nchi zingine kutokana na nchi ya India kuzuia uingizwaji wa zao hilo kutoka Tanzania.

India ilisitisha uungizwaji wa zao hilo tangu mwaka jana kwa kile kinachodaiwa kuwa imezalisha ziada ya mbaazi nchini humo kwa zaidi ya asilimia 30.

Lakini tangu wakati huo hakuna majibu ya uhakika kutoka Serikalini yaliyotolewa kuwakwamua wakulima katika mdororo wa bei ya zao hilo ambalo linategemewa na wakulima wengi hasa wa mikoa ya Arusha na Manyara kama zao la biashara.

Aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Chakula, William Ole Nasha  akihojiwa na wanahabari mwaka jana alikiri India kusitisha manunuzi ya mbaazi na kwamba Serikali inaendelea kutafuta njia mbadala kuwasaidia wakulima.

“Ni ukweli kwamba India ambao ndiyo wanunuzi wakubwa wa mbaazi ya Tanzania wamesitisha kufanya hivyo kutokana na uzalishaji kupanda kwa asilimia 30 nchini humo hivyo kwa sasa hatuna jinsi ya kufanya kuwasaidia wakulima wetu isipokuwa kubuni njia mpya ya kuwasaidia katika msimu ujao wa kilimo”, alinukuliwa Ole Nasha na kuongeza kuwa,

“Moja ya Mbinu hiyo ni kuanza kuwahamasisha watanzania kuanza kutumia mbaazi kama chakula ili kupanua soko la ndani badala ya kutegemea soko la nje”.

                                   Mbaazi ikiwa shambani kabla ya kuvunwa

Bei ya Mbaazi iliimarika katika msimu wa mwaka 2015 ambapo kilo moja ilikuwa ikiuzwa kwa sh. 2,800 hadi 3,000 (sawa na 280,000/300,000 kwa gunia la kilo 100) ambapo ilikuwa neema kwa wakulima na msimu uliofuata wa 2016 uzalishaji uliongezeka zaidi lakini matatizo ya soko yakaanza kujitokeza.

Mpaka kufikia msimu wa 2017, inasemekana bei ilishuka hadi sh. 150 kwa kilo kutokana na mabadiliko ya bei ya kimataifa na kuathiri wakulima wengi wao zao hilo nchini.

Tanzania ni moja ya nchi za Afrika zinazozalisha kwa wingi mbaazi, ambapo asilimia 95 ya zao hilo ilikuwa inauzwa nchini India na sehemu ndogo iliyobaki inatumika kwa chakula.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *