Kuna mtazamo wa baadhi ya watu kuwa mtoto yeyote ambaye anasoma hajakomaa kiakili kiasi cha kuweza kuhusishwa kufanya maamuzi muhimu katika shughuli za familia na jamii. Dhana hiyo inajikita zaidi kumtengenezea mtoto mazingira ya kuwa mtu wa kupokea maelekezo ya mambo anayotakiwa kufanya pasipo kuhoji.
Wanaenda mbali zaidi na kufikiri kwamba watoto wanatakiwa kuwepo shuleni kwa ajili ya kusoma tu na hawapaswi kushiriki katika shughuli zingine za shule ikiwemo utawala na kufanya maamuzi muhimu ya maendeleo ya shule.
Mtazamo huo unaweza usiwe sahihi kwasababu mtoto naye ni binadamu kamili anatakiwa kuwajibika, kufikiri na kushiriki katika maamuzi ya shule. Ni wajibu wa jamii kumpa nafasi ya kutoa maoni yake.
Mkataba wa kimataifa wa Haki za Watoto ambao Tanzania imeridhia, unatambua haki ya watoto kushiriki katika masuala yote yanayowahusu. Mambo yanayowahusu ni pamoja na elimu ambayo wanaipata shuleni. Wanawajibika kuwa sehemu ya maamuzi ya kiutawala wawapo shuleni ili kuhakikisha maslahi yao yanazingatiwa.
Kwanini wanafunzi washirikishwe kwenye utawala wa shule
Wataalamu wa Saikolojia ya mtoto wanaeleza kuwa wanafunzi wana uwezo mkubwa wa utambuzi, wanafahamu kinachoendelea shuleni. Wana uwezo wa kutoa mawazo kwa vitendo na kuleta mabadiliko katika sera na kanuni zinazoongoza shule.
Mfano, wanatambua walimu ambao hawaingii darasani, wakipewa nafasi kujieleza itasaidia kupunguza utoro kwa walimu ambao hawatekelezi wajibu wao.
Watoto wanajifunza kwa vitendo, kuwashirikisha katika maamuzi kunawapa ujuzi wa maisha na jinsi ya kufanya ulinganifu wa mambo mbalimbali, kutetea hoja na kutoa mapendekezo muhimu ya maendeleo.
Pia kunaongeza umiliki wa wanafunzi katika shughuli za shule. Wanafunzi walioshirikishwa katika kubuni jambo, wana nafasi kubwa ya kulielewa, kuona umuhimu wake na kujitolea. Mathalani sheria na miongozo iliyobuniwa kwa ushiriki wa wanafunzi ina nafasi kubwa ya kukubalika na kuheshimika.
Kutokana na umuhimu wa kuwashirikisha wanafunzi katika shughuli za utawala wa shule, Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) inawapa wanafunzi haki ya kusikilizwa na fursa ya kuboresha shule. Wanafunzi pia watahitaji kuwajibika, wanahitaji kufikiri, kutenda haki, kuheshimu na kuwajumuisha wale ambao kwa kawaida sauti zao hazisikiki.
Wanafunzi na utawala wa shule
MMEM imeweka utaratibu wa ushiriki wa wanafunzi katika utawala wa shule. Mchakato wake unaanzia kwenye Baraza la Wanafunzi na kisha Baraza la Shule na utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa na uongozi wa shule.
Utaratibu huo unaeleza kuwa, wanafunzi wawili kutoka katika kila mkondo (mvulana 1 na msichana 1) watachaguliwa na wenzao kuwa wajumbe wa Baraza la wanafunzi. Uchaguzi utaanzia darasa la 3, ikiwa wanafunzi wa darasa la 1 na 2 watachukuliwa kuwa ni wadogo mno.
Pia nafasi 2 hadi 4 za “viti maalumu” vya ziada zinaweza kutolewa kwa watoto wenye ulemavu au wenye mahitaji maalumu.
Jukumu la wanafunzi waliochaguliwa ni kuwakilisha matakwa ya wanafunzi wenzao katika Baraza la Wanafunzi na kupeana taarifa na wenzao darasani zinazotoka katika Baraza la Wanafunzi. Wawakilishi wa wanafunzi wanawajibika kupitia mkutano rasmi wa darasa unaoitishwa mara moja kwa mwezi.
Mkutano wa Baraza la Wanafunzi utahudhuriwa na mwalimu au mshauri mkuu wa wanafunzi kama mtazamaji. Kazi ya mwalimu huyo ni kuwezesha na kuendeleza uwezo wa wanafunzi na kuwa kama nguzo ya kupitishia taarifa kati ya wanafunzi na utawala wa shule. Lakini viongozi wa Baraza la Wanafunzi pia wanaweza kuwasiliana wenyewe na uongozi wa shule.
Kwa pamoja, wawakilishi wa Baraza la Wanafunzi, walimu na mikutano ya kamati ya shule watahudhuria mkutano wa Baraza la shule kila mwezi ili kujadili masuala muhimu ya maendeleo ya shule.
Baraza la shule limewekwa mahususi kwajili ya kupeana taarifa na kujadiliana kuhusu masuala muhimu miongoni ya jumuiya nzima ya shule. Wazazi ambao ni wajumbe wa kamati ya shule wataalikwa kushiriki katika Baraza na litaandaliwa na kuendeshwa kwa ushirikiano wa Mwalimu Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza la Wanafunzi.
Ni muhimu kwa wazazi na jamii kuwapata wanafunzi fursa ya kushiriki katika shughuli za jamii tangu wakiwa wadogo ili kutambua vipaji walivyonavyo na kuwajengea uwezo kufanya maamuzi sahihi ya maisha yao wakiwa watu wazima.