Taarifa hiyo ilitolewa jana Jijini hapa na Afisa wa Doria katika ofisi ya Uvuvi mkoani Mwanza, Juma Makongoro wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu.
Alifafanua kuwa samaki waliokamatwa walivuliwa huku wakiwa na urefu wa chini ya inchi 50, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria za uvuvi.
” Ni kweli kwamba Mei 10 mwaka huu majira ya saa 10 jioni tulikamata basi lenye namba za usajili T275 BLE likiwa na tani 2.5 za samaki wachanga aina ya sangara’ alisema Makongoro.
Alisema basi hilo lilikamatwa katika barabara kuu lami, Musoma – Mwanza na kwamba libambwa wakati likiwa katika eneo la Igoma Jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa Makongoro, gali hilo lilikuwa likitokea Musoma kuelekea Jijini Mwanza.
Makongoro aliwataja wafanyabiashara waliokuwa wakisafirisha samaki hao kuwa ni Hamisi Jackson(25) mkazi wa Nyakato Jijini Mwanza, William Maige (40) mkazi wa Igoma pamoja na Mashiku Buzuka(42) mkazi wa Nyashimio wilayani Magu.
Afisa huyo alisema licha ya kupakia samaki, basi hilo lilikuwa limebeba wasafiri zaidi ya 60.
Alisema watu hao walikamatwa kutokana na taarifa za siri zilizotolewa na wasamaria wema.
Mwezi jana kikosi hicho kiliteketeza makokoro, nyavu pamoja na zana mbalimbali za uvuvi haramu vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 5.