WAKAZI wa Kata ya Mindu katika Manispaa ya Morogoro wanapata huduma za afya chini ya mti kutokana na ukosefu wa jengo la zahanati na kituo cha afya.
FikraPevu imeshuhudia akinamama wakiwa wameketi chini ya mti uliogeuzwa zahanati wakiwa na watoto wao migongoni, wengine wakiungua jua wakisubiri kupatiwa huduma ya kliniki kutoka kwa wahudumu wa afya.
Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, huduma inayotolewa mahala hapo ni kliniki kwa watoto na elimu ya lishe.
Dari katika zahanati ya Madanganya mjini Morogoro.
Akinamama hao wenye watoto walionekana wakiweka mezani kadi za kliniki za watoto kila wanapofika, kisha huitwa majina ili kupatiwa huduma.
FikraPevu imebaini kwamba, pamoja na serikali kuongeza Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2016/2017, bado huduma za afya nchini zimeendelea kuwa duni katika maeneo mengi.
Kata ya Mindu, kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, ina wakazi zaidi 8,000, shule za msingi 4, zahanati moja ya Madanganya ambayo haikidhi mahitaji ya wananchi kutokana na umbali uliopo.
Kilio cha wananchi
Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kuwa kwa miaka 10, wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakiomba kujengewa zahanati bila mafanikio.
Mkazi wa Mindu, Lysia Kanuti, anasema wamekuwa wanapewa ahadi nyingi kutoka kwa viongozi lakini hakuna utekelezaji wowote uliofanyika.
“Kwa muda mrefu huduma zinatolewa chini ya mti, akinamama na watoto wanaungua jua, lakini hakuna ufumbuzi wowote wa changamoto hii,” alisema Kanuti na kuongeza kwamba, kutoka mahali wanapoishi hadi ilipo zahanati ya Madanganya ni umbali wa kilometa nane.
Kanuti ameiomba halmashauri, serikali kuu na wadau wengine wa maendeleo kuwasaidia ujenzi wa zahanati, ili kupunguza adha wanayoipata ya huduma ya afya.
“Natumia usafiri wa pikipiki kutafuta huduma za afya, ni hatari mama mjamzito kutumia usafiri wa pikipiki na baiskeli, si salama kwa afya ya binadamu,” anasema Salome, mkazi wa eneo hilo, wakati akizungumza na FikraPevu.
Salome anasema wanashindwa kufanya shughuli za uzalishaji kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta huduma za afya, hivyo kujikuta wako nyuma kimaendeleo.
Mkazi wa Mtaa wa Kasanga katika Kata hiyo ya Mindu, Marietha Yusuph, anasema anatembea umbali wa kilomita nne kutafuta huduma ya kliniki kwa mtoto ambayo hutolewa mara moja kwa mwezi katika eneo lao.
“Tunapata huduma ya afya chini ya mti, mvua ikinyesha tunaingizwa kwenye jengo la Ofisi ya Kata, ila kipindi cha jua tunakaa chini ya mti tukisubiri huduma,” ameiambia FikraPevu.
Anasema changamoto kubwa inayomkabili hasa ni mtoto akiugua usiku, hakuna zahanati ama kituo cha afya karibu, humlazimu kutumia kiasi cha Shs. 20,000 kumpeleka mtoto Kituo cha Afya cha Mafiga kilichopo kiliometa 20.
Winfrida Mkwinda anashauri vituo vya afya viwe na uwezo kutoa huduma za uzazi ili kupunguzia hospitali za rufaa mzigo kuhudumia wagonjwa wengi.
Akizungumza na FikraPevu, amesema huduma zote zikiwa zinapatikana katika vituo vya afya kunapunguza wingi wa wajawazito kujifungulia njiani, ambapo katika kipindi cha miezi sita iliyopita akinamama watatu wamejifungulia njiani.
Mkazi wa Mtaa wa Lugala katika Kata ya Mindu, Hawa Hamisi, anasema changamoto wanayopata katika vituo vya afya ni foleni kubwa inayotokana na upungufu wa watoa huduma, hususan vituo vilivyopembezoni mwa mji.
Akizungumza na FikraPevu, Hawa anasema usikivu wa watoa huduma umekuwa ukilalamikiwa, lakini hakuna ufumbuzi wa tatizo hilo, hasa la wahudumu hao kutoka kauli chafu kwa wagonjwa.
Aidha, amesema ni vyema huduma ya mama na mtoto ipewe kipaumbele kwenye vituo na zahanati za kata ambako ndiko kwenye watu wengi wenye kuhitaji kupatiwa huduma hiyo.
“Serikali inatakiwa kubadili utendaji wa utoaji wa huduma za afya katika zahanati, ili siku za Jumamosi na Jumapili utoaji wa huduma uwepo. Hiyo itasadia kupunguza foleni za wagonjwa siku za wiki,” anasema.
Wataalam wa afya
Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Madanganya, Theresia Kilua, anasema jengo la zahanati hiyo limepata ufa na uongozi wa halmashauri umewataka kutumia nyumba ya watumishi kutoa huduma za afya.
Kilua ameiambia FikraPevu kwamba, ni miezi mitatu sasa tangu kuhama kwenye jengo hilo la kituo cha afya kilichojengwa kwa nguvu za wananchi kutokana na ubovu.
Anasema mazingira ya kazi ni magumu kutokana na jengo wanalotumia hivi sasa kujengwa kwa mfumo wa nyumba ya kuishi na siyo kwa kutolea huduma za afya.
Kutokana na mazingira ya kata ya Mindu, anasema hulazimika kupanga ratiba ya kutoa huduma ya vipimo, kliniki kwa watoto katika mitaa, na huduma hiyo inajulikana “huduma ya mkoba”.
Pia ameiambia FikraPevu kuwa katika kutoa huduma ya mkoba kinachofanyika ni vipimo kwa watoto, na kutoa ushauri kwa wajawazito na elimu ya lishe.
“Huduma ya mkoba inasaidia wananchi wanaoishi mbali na vituo kupunguza gharama za kusafiri kutafuta huduma ya afya,” amesema.
Alisema kwamba, chini ya utaratibu huo, wamekuwa wanatoa huduma kwa wananchi zaidi ya 600 kwa siku, ambapo huduma hiyo hufanyika mara moja kwa mwezi kwa kila mtaa.
Kwa upande mwingine, Kilua ameiambia FikraPevu kwamba, baadhi ya akinamama ni wavivu kupeleka watoto kliniki, hata wao wenyewe kufika kupata vipimo na kwamba huduma ya kuwafuata wananchi walioko mbali na vituo vya afya imewasaidia.
“Changamoto kubwa katika Zahanati hii ya Madanganya ni ukosefu wa maji safi na salama. Tunatumia maji ya visima na hatuna nishati ya umeme,” amesema Kilua.
Ofisa Afya wa Kata ya Mindu,Yahya Ibrahimu, anasema changamoto kubwa iliyopo ni ukosefu wa Vituo vya Afya na Zahanati za ndani ya Kata hiyo.
“Kutokana na changamoto ya ukosefu wa zahanti, huduma ya kliniki kwa watoto hulazimika kutolewa chini ya mti katika Mitaa ya Kasanga na Lugala kila baada ya siku 40,” anasema.
Ibrahimu ameiambia FikraPevu kuwa idadi ya watu katika Kata ya Mindu inaongezeka kila siku hivyo huduma za kijamii zinapaswa kuongezwa na kupewa kipaumbele.
Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, Kata ya Mindu ina zahanati moja tu ya Madanganya ambayo ni mbovu, lakini inahudumia mitaa nane, huku zikihitajika zahanati nne kukidhi mahitaji.
Yahya anasema, huduma ya afya kutolewa sehemu zisizo maalumu kiafya, na kushauri jamii kuchangia katika ujenzi wa vituo vya afya, na serikali iwaunge mkono kwa lengo la kutatua kero ya afya nchini.
Anaongeza kuwa, watumishi wanaotoa huduma za afya hawatoshi, hivyo wanaishia kutoa huduma kwa wananchi walioko karibu wakati wale wa mbali hawapati huduma zinazostahili, hasa kipindi cha chanjo za kitaifa.
Mratibu wa huduma za Chanjo Manispaa ya Morogoro, Hidaya Omary, anasema wanalazimika kutoa huduma ya mkoba kutokana na ukosefu wa vituo vya afya na zahanati karibu na wananchi.
Hidaya anasema watoa huduma ya mkoba katika maeneo ambayo hayana zahanati wanapewa usafiri ili kuweza kuwafikia wananchi kwa wakati.
Diwani, Mbunge wanasemaje
Diwani wa Kata ya Mindu, Hamisi Msasa, anasema changamoto ya ukosefu wa huduma ya afya ni ya muda mrefu, na kwamba wamejitahidi kuweka mikakati ya kukabiliana nayo.
Ameiambia FikraPevu kwamba, katika kuweka huduma za afya karibu na wananchi na kuepuka wananchi kupata huduma hiyo chini ya mti wamejipanga kujenga zahanati itakayo hudumia wakazi wa Mtaa wa Kasanga na Mgaza.
Akaongeza kuwa kutokana na changamoto hiyo ujenzi wa zahanati hiyo umeshaanza na kufikia kiwango cha msingi.
“Kupitia vikao tulipendekeza zahanati ijengwe mitaa ya Kasanga na Mgaza kutokana kuwa na wakazi zaidi ya 4,000, na hakuna huduma ya afya karibu na makazi yao,” anasema.
Msasa anasema kuwa ujenzi wa zahanati hiyo ya Kasanga na Mgaza unakadiriwa kugharimu kiasi cha Shs. 64 milioni hadi kukamilika kwake.
Aidha, anasema katika Bajeti ya 2017/2018 Kata ya Mindu imetengewa kiasi cha Shs. 100 milioni katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Hata hivyo, katika fedha zilizotengwa hakuna kiasi chochote kilichoingia kwenye akaunti ya Kata.
“Changamoto kubwa ni uhaba wa fedha za kukamilisha ujenzi wa mradi huo, wananchi wamekuwa wavivu kuchangia, rasilimali fedha tunategemea kutoka kwa wadau na halmashauri,” anasema.
Msasa ameiambia FikraPevu kwamba, katika ujenzi wa zahanati hiyo Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood, ametoa matofali 1,600 ya kuanzishia ujenzi na kwamba ataendelea kusaidia.
Tunachokijua
Huduma ya afya haipaswi kutolewa katika maeneoyasiyo na usalama kama chini ya miti hata kama lengo ni kuwafikia wananchi wote, badala yake serikali inapaswa kujenga ya zahanati.
FikraPevu inafahamu kwamba, Sera ya Taifa ya Afya ya Mwaka 2007 inaelekeza kuwa Serikali itasogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa kuwa na zahanati kwa kila kijiji na kituo cha afya kwa kila kata na hospitali kwa kila wilaya.
Hata hivyo, licha ya wananchi wengi kuitikia wito wa kuchangia maendeleo kwa kujitolea nguvukazi na michango mbalimbali kwa ajili ya huduma za afya, majengo mengi ya zahanati za vituo vya afya yameshindwa kukamilishwa na serikali na hivyo kubaki kama mapagala.
Aidha, hata yale yaliyokamilika, yanashindwa kutoa huduma kutokana na ukosefu wa watumishi, nyumba za watumishi, dawa na vifaatiba.