Mpwapwa: Madarasa mawili yatumia chumba kimoja kusomea

Kulwa Magwa

KILOMETA 64 kusini mwa mji wa Mpwapwa ndipo ilipo shuke ya msingi, Lufusi katika kata ya Lumuma, ambayo inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa, suala ambalo husababisha chumba kimoja kitumiwe na madarasa mawili.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Hemelin Mnange, anasema tatizo hilo lilitokana na madarasa mawili kuanguka mwaka jana (2012). Kabla ya kubomoka kwa vyumba hivyo, shule hiyo ilikuwa na vyumba sita.

Mnange anasema baada ya kubomoka kwa vyumba hivyo kutokana na uchakavu pamoja na kuezuliwa kwa mapaa na upepo, uongozi wa shule na kijiji uliazimia kuzidondosha kabisa kuta zake ili kuepusha hatari ambayo ingetokea iwapo zingeanguka zenyewe.

shule-mpwapwa

PICHA: Shule ya Msingi Lufusi inavyoonekana

Anasema baada ya hatua hiyo, darasa la tatu na nne ilibidi yachanganywe kwenye chumba kimoja, suala ambalo linasababisha wanafunzi kutofuatilia vizuri vipindi darasani wanapofundishwa na walimu wao.

Mwalimu huyo anasema, wanafunzi wa madarasa mawili tofauti husomea katika chumba kimoja huku wakiwa wamegeuziana migongo.

Wakati mwingine, anasema mwalimu huyo, vipindi hugongana na kuwalazimu walimu wawili kuwa ndani ya chumba hicho.

“Kutokana na hali hiyo, tulikaa na diwani tukakubaliana kukusanya mawe na tufyatue matofali kujenga madarasa mapya.

Mpango huo unaendelea tukiwa tumekusanya mawe ya kutosha. Tunachosubiri ni kuanza kwa kazi yenyewe,“ anasema.

Anasema licha ya kukusanya mawe muda mrefu, shughuli ya ujenzi haijaanza suala ambalo linatia shaka kuwa hata mwaka huu (1012), wanafunzi hao wataendelea kuchangia chumba kimoja kwa masomo yao.

“Walipomaliza darasa la saba mwaka jana (2011), wanafunzi waliopo waliendelea kusoma vizuri maana tuna vyumba vinne vya madarasa vya kudumu na kimoja cha muda,” anasema.

mwalimu-mkuu-lufusi

PICHA: Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Hemelin Mnange

Mwalimu huyo anasema chumba kisichokuwa cha kudumu walichonacho wanakitumia kwa tahadhari, maana kimechoka na wakati wa mvua au upepo mkali hulazimika kuwaondoa darasani wanafunzi wanaokitumia ili kuepusha maafa.

Kuhusu walimu, Mnange anasema wako watano wanaofundisha madarasa manane likiwemo lile la awali, idadi ambayo haitoshi kutokana na mzigo wa ufundishaji walionao kwa kuwa kila inapotokea dharura wanafunzi huathirika kwa kukosa vipindi.

“Hili nalo ni tatizo kwani hata mwalimu wa darasa la awali hatuna baada ya aliyekuwepo kuacha kazi kutokana na kutopata malipo yake ipasavyo.

Mwalimu wa awali anapaswa kulipwa kutokana na michango ya wazazi, na tatizo hilo lilijitokeza kutokana na kuwepo kwa wazazi ambao walikuwa hawatoi michango na hivyo kusababisha kuondoka kwa mwalimu huyo,” anasema.

Wakazi wa kijiji hicho, Masoud Ilangia, Mopilio Mwachali, Jeremiah Kanemela na Edward Msumali wanasema kipato kidogo cha wakazi wa sehemu hiyo ndicho kilichokwamisha kukodi gari la kusomba mawe kutoka mahali walipokusanyia.

Wanasema tayari wamekusanya mawe mengi ambayo yanaweza kujenga vyumba zaidi ya vinne shuleni hapo.

Wakazi hao wanasema kitendo cha watoto kuchangia chumba kimoja, kimekuwa kikiathiri uelewa wao kwa kuwa hukosa umakini wa kufuatilia wanachofundishwa na walimu wao.

“Inawezekana kabisa hata katika matokeo ya watoto huko waendako yakawa mabaya iwapo tatizo lililopo halitatatuliwa haraka,“anasema Mopilio.

Hata hivyo, Mwalimu Mnange anasema licha ya wanafunzi hao kuchangia darasa, maendeleo yao kimasomo hayajaathirika sana. Hata hivyo anasema athari za kisaikolojia zinaweza kujitokeza siku za usoni pamoja na kwamba hazijajitokeza kwa sasa.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Beatus Sendwa, anasema wameanza maandalizi ya ujenzi wa vyumba na kwamba, wanakijiji walihamasishana kukusanya mawe milimani, lakini hawajapata usafiri wa kuyafikisha shuleni.

mwenyekiti-lufusi

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lufusi, Beatus Sendwa

Anasema, wanaendelea kutafuta usafiri na kwamba mara watakapopata, ujenzi utaanza sambamba na ufyatuaji wa matofali ya kuchoma.

Sendwa anasema upatikanaji wa usafiri katika kijiji hicho ni tatizo kubwa kwa maendeleo na umesababisha hata mpango wa kijiji wa kujenga duka kukwama kutokana na kushindwa kusafirisha mawe waliyokusanya milimani.

Naye Diwani wa Kata ya Lumuma, Joklan Cheliga, anasema vyumba hivyo vilipoanguka, aliwamasisha wakazi kukusanya mawe, lakini tatizo lililojitokeza ni mwamko mdogo wa baadhi ya wananchi katika utekelezaji wake.

“Mimi mwenyewe nimeamua kutumia nguvu ya ziada na baada ya masika kumalizika nitaanza kukusanya mawe na matofali ya kuchoma. Hayo mambo nitayaanza mwezi wa tatu (Machi), ili serikali ya wilaya itusaidie hatua za mwisho za upauaji,” anasema.

Hata hivyo, Mratibu wa Elimu kata ya Lumuma, Bathlety Mfugale, anasema kwa kushirikiana na viongozi wenzake wa kata na kijiji, wanapanga kupeleka ombi maalumu wilayani ili serikali iweze kulipa kipaumbele suala hilo, ikizingatiwa kwamba mvua za masika ziko karibu kuanza kunyesha.

“Diwani wetu anafanya juhudi zake kuhakikisha ufumbuzi unapatikana, sisi pia tunafikiria kuiomba halmashauri isaidie ikiwezekana kwa kutupatia usafiri kusafirisha hayo mawe mpaka shuleni,“anasema.

Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Elimu wa wilaya hiyo, Emmanuel Elinazi, anasema tatizo linaloikabili shule hiyo na idara ya elimu wilayani humo ni ufinyu wa bajeti.

Na kutokana na tatizo hilo, amesema ametoa wito kwa wanakijiji kuongeza juhudi ili nguvu ya serikali itakapotolewa isaidie kumalizia.

“Suala ni kwa wananchi kuhamasishwa ili wafanikiwe kutatua tatizo hilo. Ukizungumzia wanafunzi kusoma wamegeuziana migongo hilo lipo sehemu nyingi za nchi yetu,”anasema Elinazi.

Lakini alipoulizwa na gazeti hili kuhusu tatizo hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya wilaya ya Mpwapwa, Fanuel Senge, alisema hata shule yenyewe haijui.

“Hata huko Lufusi penyewe mimi sijawahi kufika maana ni mgeni. Lakini kama kuna wanafunzi wanasomea kwenye chumba kimoja ni kosa na walimu walipaswa kuweka utaratibu mzuri ili wasome vizuri ikiwezekana kwa awamu,”alisema Senge bila kufafanua utaratibu upi ungewekwa.

Shule ya msingi Lufusi ilianzishwa mwaka 1997 na hivi sasa ina wanafunzi 222. Kila mwaka, shule hiyo huandikisha wastani wa wanafunzi 35 wa darasa la kwanza.

Uhaba wa vyumba ulioko katika shule ya Lifusi ni sawa na ule wa shule ya Mitolonji, iliyopo Namtumbo, mkoani Ruvuma, ambayo ina upungufu wa vyumba vitatu suala linalowalazimu wanafunzi wa madarasa manne kuchangia vyumba viwili kwa wakati mmoja. Shule hiyo ina wanafunzi 219.

Kwa mujibu wa ibara ya 11 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imeitaja elimu kuwa miongoni mwa haki za msingi za binadamu, ambapo imelikabidhi suala hilo mikononi mwa serikali kupitia kifungu cha (3) ili ihakikishe kuwa kunakuwa na fursa na mazingira sawa ya utoaji na upatikanaji wa elimu.

Aidha rasimu ya pili ya sera ya elimu ya mwaka 2010, toleo jipya la Machi 2011, inasema elimu ya msingi inakusudiwa kumwezesha kila mtoto kupata maarifa, mwelekeo, ujuzi na stadi za msingi za kusoma, kuandika, kuhesabu, kubaini na kutambua changamoto zilizopo katika mazingira na mbinu za kukabiliana nazo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *