MUVI: Mbegu bora za nyanya zitahimili mtikisiko wa masoko

Jamii Africa

WAKULIMA wa nyanya mkoani Iringa sasa wamepata suluhisho la tatizo la kuharibika kwa zao hilo baada ya kuvunwa.

Hii ni baada ya Mradi wa Muunganisho wa Ujasiriamali Vijijini (MUVI) kuwahamasisha kutumia mbegu bora aina ya Aden F1, ambayo matunda yake yanastahimili kukaa kwa zaidi ya siku 30 bila kuharibika baada ya kuvunwa.

“Mbegu hizi chotara zinazalishwa na kampuni ya Mosanto ya Kenya ambapo wakulima tayari wamekwisha ijaribu kwa misimu mitano sasa, inaweza kukaa kwa siku hata 40 bila kupoteza ubora wake,” anasema Wilma Mwaikambo Mtui, Shirika la Mradi wa mkoani Iringa alipoongea na FikraPevu.

Hali hiyo ya kukaa muda mrefu bila kuharibika baada ya kuvunwa itawawezesha wakulima kutafuta soko la uhakika lenye tija pasipo kuhofisa usalama wa bidhaa, tofauti na mbegu nyingine ambazo wamekuwa wakizitumia miaka yote.

Kwa muda mrefu sasa, wakulima wa zao hilo mkoani humo wamekuwa wakilia kutokana na ukosefu wa soko la uhakika, huku kiasi kikubwa cha mavuno yao kikiharibika kabla ya kufika sokoni, hali ambayo inawafanya wapate hasara badala ya tija.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, wakulima na wafanyabiashara wa nyanya katika Kata za Image na Ilula wilayani Kilolo, wamekuwa wakilalamika kwamba ukosefu wa soko unawapa umaskini huku wakipoteza zaidi ya asilimia 70 ya mavuno yao kutokana na kuharibika.

Wakulima hao walisema, kama kungekuwepo na soko la uhakika pamoja na viwanda vya usindikaji matunda, kilimo cha nyanya kingekuwa kimewakwamua wengi kwa vile hilo ndilo zao kuu la biashara mkoani Iringa.

Hili ni soko lisilo rasmi kando ya Mto Mlowa unaotenganisha vijiji vya Iyayi na Uhominyi katika Kata ya Image wilayani Kilolo. (Picha na Daniel Mbega).

Lakini katika kipindi ambacho ujenzi wa viwanda vya kusindika mboga mboga mkoani humo bado unasuasua kutokana na kukosekana kwa wawekezaji wa kutosha, mbegu ya Aden F1 ndiyo inayoweza kuwanusuru wakulima hao pamoja na kukuza uchumi wa Taifa.

Mbali ya uwezo wa kudumu kwa muda mrefu baada ya kuvunwa, Mtui ameiambia FikraPevukuwa, mbegu hiyo ina mavuno mengi zaidi ikilinganishwa na mbegu nyingine, hivyo kuwafanya wakulima waongeze kipato chao na kujinasua katika lindi la umaskini.

Mtui anafafanua kwamba, aina hiyo ya nyanya ambazo zinafaa kulimwa katika majira ya masika, zinaweza kuzalisha karibu mara nne mpaka tano ya aina nyingine katika ubora wa hali ya juu.

“Wakulima waliotumia mbegu hizi msimu huu wamepata mavuno mengi kuliko walivyotegemea, hivyo tunaendelea kuwahamasisha wengine watafute mbegu bora zinazoweza kustahimili mtikisiko wa soko,” anaongeza.

Mtokambali Mgimba, mkulima wa nyanya kutoka Kijiji cha Tanangozi wilayani Iringa, ni miongoni mwa wakulima waliopata mafanikio baada ya kutumia mbegu hiyo ambapo katika msimu huu aliweza kuvuna mamilioni ya fedha.

Mkulima huyo aliwahi kunukuliwa akisema kwamba, awali alikuwa akiishi nyumba ya nyasi, lakini sasa amefanikiwa kujenga ya bati kwa Shs. 6 milioni, pamoja na kununua nyingine ya biashara mjini Iringa huku akiwa anaendelea na kilimo cha kisasa.

“Nyanya zinazotokana na mbegu aina ya Aden F1 zina thamani kubwa tofauti na nyingine, hata kama soko limesheheni nyanya, lakini ukipeleka nyanya hizi lazima utauza kwa haraka na kwa bei nzuri,” anasisitiza Mtui.

Hata hivyo, Mtui anasema, kupatikana kwa mbegu hiyo ni mafanikio makubwa kwa mkulima, kwani ni moja ya malengo saba ya Muvi katika kuwasaidia wakulima kupata mbegu bora kwa wakati na kwa bei watakayoimudu pamoja na kusaidia upatikanaji wa pembejeo.

Anasema wanawajengea uwezo wajasiriamali walio katika minyororo ya thamani ili waweze kuendesha shughuli zao kwa ufanisi na kwa faina, jambo ambalo wamefanikiwa kulifanya kwa kuhamaisha uundwaji wa vikundi ambavyo hatimaye vimeweza kuzaa shirikisho la wakulima wa zao hilo mkoani humo.

“Tunawapa mafunzo, hatuwapi fedha, tunawahamasisha wajiunge katika vikundi na mitandao ya wakulima, halafu tunawaelekeza mbegu bora ya nyanya zinazoweza kuhimili muda mrefu baada ya mavuno, lakini pia tunawashirikisha wadau wengine kama wazalishaji wa mbegu, wazalishaji wa mbolea na kemikali za kupulizia ikiwa ni pamoja na kuanzisha jukwaa la majadiliano la wadau wote,” anaongeza Mtui.

Kwa kuwapatia elimu wakulima badala ya fedha, MUVI wameweza kuwajengea uwezo wakulima hao kwa dhana ya ‘kuwapatia nyavu na kuwafundisha uvuvi, badala ya kuwapa samaki’.

FikraPevu imeelezwa kuwa, katika kukabiliana na changamoto za kilimo cha zao hilo, MUVI wamefanikiwa kuunda vikundi katika wilaya tatu za majaribio – Njombe, Kilolo na Iringa – ambapo jumla kuna vikundi 93 vikiwa na wakulima 4,900.

FikraPevu inatambua kwamba, MUVI wanajitahidi pia kusaidia kuwaunganisha wadau wa kilimo hicho cha nyanya na masoko ya nje, ambapo hivi sasa nyanya zinazozalishwa Iringa, mbali ya kupelekwa katika soko la Dar es Salaam, zinasafirishwa pia Kenya, Zanzibar, Comoro na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huku juhudi za kutafuta masoko katika nchi za Malawi na Zambia zikiendelea.

FikraPevu inatambua kwamba, Mkoa wa Iringa ndio unaongoza kwa uzalishaji wa nyanya nchini Tanzania, ambapo kwa mujibu wa taarifa za maendeleo ya kilimo za mkoa na zile na Shirika la Kilimo Duniani (Fao), mkoa huo unazalisha zaidi ya asilimia 70 ya nyanya zinazoliwa nchini.

Hata hivyo, mratibu huyo wa MUVI anasema kwamba changamoto ya masoko bado ipo, ingawa tayari wamekwishazungumza na kampuni moja ya mkoani Arusha kujenga kiwanda kikubwa cha kusindika mboga mboga ambacho kinaweza kuwa mkombozi kwa wakulima.

“Hawa wawekezaji wamesema watajenga kiwanda kitakachosindika tani 200 za nyanya kwa siku, hii ikiwa na maana kwamba tunalo jukumu kubwa la kuwahamaisha zaidi wakulima wazalishe kwa wingi nyanya ili kukidhi mahitaji ya kiwanda hicho mara kitakapoanza kazi,” alisema Mtui.

FikraPevu inajua kwamba, tayari kiwanda hicho kimekwishajengwa katika Kijiji cha Igwachanya ambapo kinaendelea na uzalishaji ingawa wakulima wanalalamika kwamba bei ya zao hilo iko chini kuliko walivyoahidiwa.

Ofisa Kilimo wa zamani wa Mkoa wa Iringa, Shenal Nyoni, alisema kwamba, katika msimu wa 2011/12, jumla ya tani 115,514 zilivunwa mkoani humo, ingawa taarifa za uchunguzi zinasema ni asilimia tano tu kati ya hizo ambazo zilisindikwa.

Nyoni, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Pembejeo katika Wizara ya Kilimo, Chakula na Maendeleo ya Mifugo, aliwahimiza wakulima kuongeza kasi ya uzalishaji licha ya changamoto mbalimbali zilizopo.

“Kweli tuna uhaba wa viwanda vya usindikaji, ni changamoto kubwa ambayo kwa kushirikiana na wadau wengine tunatafuta namna ya kuitatua,” alisema huku akiyataja miradi kama Muvi, TechnoServe ambalo limehitimisha mradi wake na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kama wadau muhimu ambao wamekuwa wakishiriki harakati za kuwasaidia wakulima.

FikraPevu inaona kwamba, ikiwa wakulima wengi watahamasika kuzingatia kilimo cha kisasa na matumizi ya mbegu bora na pembejeo, hakika tatizo la soko litatatuliwa, ingawa serikali nayo inapaswa kuhamasisha wawekezaji wa viwanda vya usindikaji ili kuongeza thamani ya zao hilo.

1 Comment
  • Nyanya hizo ni za kuchomekea njiti na zinaweza kulimwa kuanzia miezi yenye mvua nyingi kama mbeya kuanzia mwezi wa 12-05 na zinahitaji upulizie Mara ngapi kwa mwezi dawa za kuzui kuungua na vididu?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *