Mwalimu wa kwanza Tanzania wa daraja la A(Grade A) ambaye pia alikuwa ni padre wa jimbo kuu katoliki la Songea padre John Fratera Gama amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Marehemu padre Gama amefariki katika hospitali ya misheni Peramiho iliyopo kilometa 24 kutoka mjini Songea ambako alikuwa amelezwa kutokana na kusumbuliwa na magonjwa ya moyo na kisukari.
Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea mhashamu Norbert Mtega amesema kuwa marehemu padri padre Gama atakumbukwa na watanzania wengi hasa kutokana na vipaji vyake ikiwemo kuwa miongoni mwa walimu wanne wa kwanza wa Tanzania waliopewa daraja la daraja A(Grade A) katika chuo cha uliamu Tabora mwaka 1944.
“Wananchi wa kawaida, Mapadre wengi na wahashamu maaskofu kadhaa wa ukanda wa kusini wamelelewa na kufundishwa naye,amekuwa mwamba wa taaluma hasa katika fani za falsafa na lugha ya kilatini alioweza kuwafundisha wanafunzi wake kwa umahiri mkubwa’’, alisisitiza mhashamu Mtega.
Mwalimu wa kwanza wa daraja la A (Grade) Tanzania marehemu padre John Frateri Gama
Aliongeza kuwa padre Gama alipenda kujiendeleza kitaaluma na alifarijika kuwawezesha watanzania wengine kitaaluma kutokana na kuamini kuwa elimu bora ni pato la kuwa na walimu bora hali ambayo ilileta mafanikio makubwa kiutendaji katika kanisa, taasisi za umma na watu binafsi
Historia ya maisha yake inaonyesha kuwa afya yake ilizidi kutetereka kuanzia mwaka 2011 kutokana na kuzidiwa na tatizo la kisukari ambalo lilidhoofisha mwili wake na kuathiri mguu wake wa kushoto uliowalazimisha madaktari kuukata mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu kwa lengo la kuokoa maisha yake.
Marehemu padre Gama ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 88 na miaka 56 ya upadre hadi mauti yanamkuta alikuwa anatoa huduma kama mchungaji na muhudumu wa kiroho katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma ya mjini Songea.
Marehemu padre Gama alizaliwa Luyangweni wilayani Songea mwaka 1926,elimu ya msingi alipata kati ya mwaka 1933 hadi 1937 katika shule za msingi Likuyufusi na Mshangano,elimu ya sekondari kati ya mwaka 1938 hadi 1943 sekondari ya Malangali na mafunzo ya ualimu aliyapata mwaka 1944 katika chuo cha ualimu Tabora na kutunukiwa cheti cha ualimu daraja la A.
Masomo ya seminari aliyapata kati ya mwaka 1945 hadi 1950 seminari za Kigonsera na seminari kuu Peramiho ambapo chuo kikuu alisoma kati ya mwaka 1965 hadi 1967 Roma Italia katika chuo kikuu cha Angelicum na kutunukiwa masters ya falsafa.
Padre Gama pia mwaka 1967 hadi 1968 alisoma chuo kikuu cha Makerere nchini Uganda na kupata stashahada ya ualimu na mwaka 1977 alisoma chuo cha Chama Cha Mapinduzi Kivukoni jijini Dar es salaam alitunukiwa stashahada ya siasa ya ujamaa.
Misa ya mazishi ya mwalimu na padre Gama ilifanyika katika kanisa la kiaskofu la mtakatifu Mathias Kalumba jimbo kuu la Songea ambayo ilioongozwa na Askofu mkuu Norbert Mtega ambapo mazishi yaliohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Songea yalifanyika katika makaburi ya parokia ya Matogoro nje kidogo ya mji wa Songea.
Heri aliye maskni wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wake. Mungu alitoa Mungu ametwaa jina lake libalikiwe, father tulikupenda sana ila Mungu amekupenda zaidi. Poleni watanzania wote kwa msiba huu mkubwa.