Ni saa 3:00 asubuhi, natoka kwenye nyumba ya kulala wageni iitwayo ‘Kwa Aziz’ kusubiri usafiri wa kunipeleka kwenye mgodi wa wachimbaji wadogo, ulioko Sambaru, umbali wa kilometa 15. Sambaru iko wilayani Ikungi, ilhali Londoni, nilipo, ni Manyoni. Wilaya hizo mbili ziko mkoani Singida.
Kwa mujibu wa wenyeji, panaitwa Londoni kutokana na wingi wa madini ya dhahabu yaliyokuwepo miaka ya nyumba ambapo wenyeji waliamini siku za baadaye kuwa kijiji hicho kingekuja kuwa kizuri sawa na jiji la London, lililopo nchini Uingereza. Hata hivyo, Londoni nilipo inaandikwa Londoni ilhali ile ya Uingereza huandikwa London.
Wakati naendelea kusubiri, mpanda pikipiki niliyeongea naye jana, Juma Salum, anapiga simu akisema atapatikana baada ya saa tano kutoka wakati ule nikiongea naye. Akasema yuko mbali sana. Nikaona sasa “haya yamekuwa mang’ana” – yamekuwa maneno, kama wasemavyo Wakurya.
Najiuliza haraka: Nisubiri kwa saa tano? Napata jibu. Naahirisha safari. Nampigia mpanda pikipiki na kumsihi aje kesho asubuhi nilikofikia. Lakini bado najiuliza: Nitafanya kazi gani leo?
Kwa karibu nasikia mngurumo. Nimeusikia tangu nimefika sehemu hii. Nawauliza wenyeji wangu Khamis Ataka na Gabriel Ntanii, mngurumo wa nini? Wananieleza ni wa mashine. Naambiwa ni umbali wa kama dakika tano hadi saba kwa miguu. Naambiwa sehemu hiyo inaitwa ‘mwaloni,’ yaani sawa na ufukweni mwa bahari, ziwa au mto ambapo wavuvi huuzia samaki.
PICHA: Hizi ndizo mashine za kusaga mawe ya dhahabu
Mwaloni na mashine zitoazo mngurumo? Nikajiuliza. Kana kwamba kuna viwanda vya vyuma? Najibiwa eneo hilo ndilo lenye mitambo ya kusaga mawe ya wachimbaji wadogo. Hawa hawana nyenzo za kisasa za kusagia mawe; hivyo kazi nzito inayofanyika pale inatokana na ubunifu wao.
Wenyeji wananiambia eneo hilo linaheshimika sana kwa kuwa wapo watu waliobahatika kusagiwa mawe, wakachenjua mchanga vizuri; wakapata dhahabu na hivi sasa ni mamilionea huko wanakoishi. Nashawishiwa na nashawishika nifike nikajionee utajiri unavyotafutwa ‘mwaloni.’
Ntanii anajitolea kuambatana nami. Tunajivuta taratibu hadi sehemu hiyo nikiwa na matumaini ya kuona mambo makubwa. Mwalo una mambo. Naanza kushangazwa na aina ya watu ninaowakuta.
Ni mwingiliano wa watu – hawa wakienda huku, hawa kule na hawa wakizunguka humuhumu tu. Ni watu wa rika mbalimbali – vijana, wazee, kinamama wenye watoto, wasichana na wavulana wa umri wa kati ya miaka 18 na 25; na watoto wa umri wa miaka 10 hadi 15. Wote wanasaka riziki. Madalali wa dhahabu wanapishana kwa baiskeli na pikipiki. Kengele za baisikeli na honi za pikipiki zimejaa angani.
Mashine zinazotumika kusaga miamba na mawe zimetengenezwa na wenyeji. Ninaelezwa kuwa utalaamu uliotumika kuzitengeneza unahusisha mashine za kuvuta maji ardhini zilizounganishwa kwa mikanda ili kuziwezesha zizungushe mapipa makubwa mazito ambayo ndani yake huwekwa mawe yaliyochimbwa katika migodi mbalimbali inayozunguka vijiji.
Mwenyeji wangu ananiambia kuwa katika maeneo mengi zinakofanyika shughuli za uchimbaji mdogo wa madini nchini, teknolojia hiyo imezoeleka maana inawarahisishia kazi wachimbaji kupata wakitakacho (dhahabu). Ndani ya kila mashine hizo za kienyeji kuna gololi kubwa na ndogo zaidi ya 100; zenye uzito wa kati ya kilo moja hadi nane. Hizo naambiwa ndizo zinaponda mawe na kuyasaga kuwa mchanga laini kama unga.
Nafika kwa mwendesha mashine aitwaye William Emmanuel (24). Ananiambia kuwa katika kila mashine huweka kilo 50 hadi 70 za mawe ambayo huyasaga kwa dakika 20 hivi hadi yanapokuwa unga. Kisha huutoa unga huo na kumkabidhi mtu aliyempelekea amsagie.
PICHA: William Emmanuel akieleza jinsi mashine za 'kienyeji' za kusaga mawe ya dhahabu zinavyofanya kazi
Hiyo ndiyo kazi kubwa ya kwanza inayofanyika mwaloni. Gharama ya kusaga mawe ni Sh. 6,000 kwa kila mfuko wenye ujazo wa kilo 50, na kwa wastani kila siku anaweza kusaga mifuko 70, hivyo hupata sh. 420,000.
Kuhusu upatikanaji wa mashine hizo, kijana huyo anasema baadhi ya vifaa vya kutengenezea huvipata Singida mjini, ilhali vingine upatikanaji wake ni Dar es Salaam. Ananiambia mabati magumu kwa ajili ya utengenezaji mapipa ni yale yanayotumika kujengea mageti ya nyumba, hivyo hata Singida yanapatikana.
Anasema gololi huzipata Dar es Salaam na ndiko anakonunua mashine zinazowezesha kuzungusha mapipa hayo, yaani zile za kuvuta maji. Ananiambia gharama ya kila mashine anazotumia hadi kukamilika ni sh. milioni 3.2.
Emmanuel anasema ana uzoefu wa miaka sita na kazi hiyo imemuwezesha kupata mafanikio makubwa maishani mwake. Anasema amejenga na anamiliki vitega uchumi vingine kama maduka na gari ndogo ya abiria.
Hatimaye nafika hatua inayoitwa ya “kupata au kukosa.” Hapa wahusika hawataki kuongea. Kila mmoja yuko makini kwa anachokifanya. Na kweli, Wanakataa kuongea nami. Macho yako kwenye mchanga na tope; na hakika mchanga na tope viko kwenye macho yao! Inawachukua saa moja na nusu hivi kumaliza kazi yao.
Hata hivyo wakati wakiendelea na kazi wananitajia majina yao kuwa Abel Ntandu (21) na Aminiel Abdallah (18). Hatua chache kutoka walipo vijana hawa yupo mama mmoja. Huyu ananiambia anaitwa Zena Abdallah na umri wake ni miaka 63.
PICHA: Zena Abdallah akiwa kazini
Naambiwa hapa ndiko kuna idara ya “uoshaji mchanga” – kwa lugha yao. Lakini hapa ndipo mchanga unapokutanishwa na maji na kuchuja kilichomo.
Mwenyeji wangu ananiambia hatua hiyo ni muhimu na kila mtu “huosha” au “huoshewa” mchanga wake kwa tahadhari kubwa, akisema “…parapara yoyote inaweza kumgharimu mhusika – kwa njia ya kupoteza dhahabu kwenye maji na, au katika tope”.
Ni katika ‘idara’ hii kuna mitambo isiyonguruma. Hizi ni meza ambazo upande mmoja miguu yake ni mirefu kuliko upande mwingine. Katika kudadisi naambiwa upande wenye miguu mirefu ndiko anakosimama muoshaji na ni hapo pia humwaga mchanga na maji ambavyo hutiririkia upande wenye miguu mifupi.
Nasogea karibu kuangalia zaidi jinsi mitambo hiyo ilivyo na inavyofanya kazi. Naona gunia lililofunikwa na kitambaa laini. Mwenyeji ananiambia gunia lililopo chini ya kitambaa ni mahususi kuchuja mchanga na kitambaa cha juu ndicho kinachobakiza chembechembe za dhahabu, iwapo zimo ndani ya mchanga na maji. Pia kitambaa hicho kinahifadhi mchanga laini unaoaminika kuwa na madini.
Naangalia kwa makini hatua kwa hatua. Kila hatua ina umakini wake, kuanzia kumimina mchanga juu ya kitambaa, kuumwagia maji na jinsi ya kuondoa udongo kuutofautisha na mchanga laini. Wanamaliza kazi. Naanza kuongea nao mmoja baada ya mwingine.
Ntandu anasema, amefanya kazi ya uchimbaji madini kwa miaka mitatu, ambapo inamwezesha kupata pesa za kula na kuendesha maisha yake.
Anasema, fedha anazopata pia huwatumia wazazi wake ambao wanaishi kijiji cha Lagangabilili, Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu. Huko vilevile anamiliki mifugo na biashara ya duka kijijini. Alifika Londoni, mwaka jana akitokea machimboni Geita baada ya kusikia sehemu hiyo dhahabu zilikuwa zinapatikana kwa wingi.
Tofauti na Ntandu, Abdallah ameanza kazi hiyo miezi mitatu iliyopita baada ya kumaliza elimu ya sekondari. Hata hivyo, anasema kazi hiyo imeanza kumpa matumaini ya maisha, maana amenunua mabati na tayari mafundi wanaendelea kufyatua tofali ili aanze ujenzi kijijini kwao.
Kwa upande wake, Zena ananiambia ni mzoefu, pengine kuliko wengi waliopo sehemu hiyo. Anasema huu ni mwaka wake wa 15 anafanya kazi ya kuokota mabaki ya mawe migodini yanayoachwa na wachimbaji wadogo. Kazi hiyo humuingizia wastani wa sh. 260,000 kwa wiki na inamwezesha kumsomesha binti yake chuo kikuu.
Hata hivyo, anasema huu utakuwa mwaka wake wa mwisho kufanya kazi hiyo, maana binti yake anamaliza masomoni. Licha kusomesha wanawe, amenufaika na kazi kuwaozesha wengine maana mumewe alifariki miaka mingi iliyopita.
Hatua inayofuata baada ya hizo mbili katika mwalo wa Londoni, ni ile ya uchenjuaji mchanga laini, uliotokana na kazi ya awali. Hii pia naambiwa ni hatua muhimu na mara nyingi hufanywa na watu waliobobea, maana hapo ndipo dhahabu inapodhihirika kuwa katika mchanga; na ni hapo pia mtu anaweza kuambulia patupu.
Kazi hiyo inafanyikia ndani ya vibanda ambako kuko kimya kidogo kuliko vurumai za sehemu nyingine; na mwenyeji wangu ananiambia kuwa humo ndimo inafanyika hatua ya mwisho ya “kusaka mali” na kwamba wanaofuatilia sharti wawe wahusika – walioleta mawe au mchanga.
Nabahatika kuingia katika kibanda na hapo niliowakuta wanataka kujua uwepo wangu mahali hapo, nami nawajibu kuwa najifunza na nimefika kujua wanavyofanya kazi zao. Tukazungumza haya na yale huku tukipiga picha mbalimbali tukimuangalia mchenjuaji, Masanja Mahende (31), akifanya vitu vyake.
PICHA: Mahende Masanja akiwajibika katika kazi yake ya uchenjuaji wa madini ya dhahabu
Hapa niliuliza: “Kwa nini wenye mchanga wasifanye kazi hii wenyewe maana naona ni rahisi?” Swali lilizaa kishindo. Kijana mmoja akanijibu haraka, “Acha utani bwana ee!”
Anasema, “Ukitaka kutania basi jitie unajua, halafu mali ya mtu iishie kwenye maji. Utakoma!” Nikanyamaza na kuendelea kuangalia kinachofanyika, ambapo baadaye nikaja kubaini kwamba hiyo ndiyo kazi ngumu ya kusaka dhahabu kwa kuwa kuichenjua ndoo moja, mhusika anatumia zaidi ya saa mbili. Naambiwa pia malipo ya mchenjuaji si haba; analipwa Sh. 5,000 kwa kila ndoo.
Ni katika hatua hiyo mchenjuaji huchenjua kama afanyavyo mpishi wa wali anapoosha mchele wake. Wakati wapishi majumbani hutumia sufuria au beseni ndogo, wale wa mwaloni wanatumia makalai mawili. Wanatumia makalai kwa kuwa wanaamini ni rahisi kunasa dhahabu pale wanapoweka ‘mekyuri’ (zebaki) ili kuikusanya kwenye maji.
Baadaye, Mahende anakuja kuniambia kuwa kazi hiyo ameizowea maana ameanza kuifanya tangu akiwa na umri wa miaka 22, na kwamba ameifanya katika maeneo tofauti ya uchimbaji madini.
“Nilianzia Geita, nikaenda Kahama kisha nikatua sehemu za Nzega. Zamani nilikuwa mchimbaji kabla ya kuibukia katika uoshaji. Naifurahia kazi yangu maana inanipatia kipato kizuri, na kwa siku nikikosa naweza kuambulia sh. 70,000 ila kwa wiki ni wastani wa sh. 300,000. Hizo sikosi,” anasema.
Baada ya kujionea ‘maajabu’ hayo kwa upande wangu, mwenyeji wangu ananisogeza nyuma ya kibanda hicho kuangalia uchomaji dhahabu unavyofanyika. Hapa si kibandani, ni nje na pia hatua hiyo inafanywa kienyeji kuondoa ‘mekyuri’ kwenye dhahabu. Hiyo naambiwa ni kazi ndogo na “mtu yeyote anaweza kuifanya.”
PICHA: Baadhi ya vitendea kazi vinavyotumiwa katika mwalo wa dhahabu wa Londoni, mkoani Singida
Mpaka wakati huo, nimekaa mwaloni kwa takribani saa sita, nikishuhudia vijana na watu wazima wakihangaika kusaka dhahabu. Kwa mujibu wa mwenyeji wangu, vijana wawili tuliokuwa tukifuatilia zaidi shughuli yao, mmoja alipata dhahabu yenye uzito wa gramu 18 na mwingine aliambulia gramu nane (8). Zena aliondoka zake bila kujua alichoambulia. Naambiwa bibi huyo ni msiri, hapendi watu wajue anachopata.
Kwa bei ya dhahabu mwaloni, vijana hao walikuwa na uhakika wa kulala na Sh. 1,820,000 mifukoni baada ya kuuza kila gramu kwa Sh. 70,000. Nawaangalia mara mbilimbili. Mwenyeji wangu ananieleza, “…mtu kupata kiasi hicho cha fedha ni suala la kawaida sehemu hii”.
Upande wa soko? Hilo naambiwa limejaa tele! Wapo wanunuzi wengi ambao wamezigawa fedha zao kwa mawakala na madalali wanaowakusanyia dhahabu. Wanunuzi hao wananunua madini ya kiasi chochote cha fedha, hiyo ikiwa na maana kuwa fedha zipo hata kama hakuna benki ya kuzitunzia sehemu hiyo.
Rajab Kitima ni mnunuzi wa dhahabu. Ingawa hataki kutaja mtaji wake, anasema ana fedha nyingi anazowapa ‘vijana’ wake sita wamkusanyie dhahabu, kisha huwalipa posho.
Kitima ananiambia anaponunua dhahabu na kutimiza lengo analojiwekea, husafiri hadi Dar es Salaam au Nairobi kuuza, maana huko ndiko kwenye masoko mazuri. Kwa Londoni, kila gramu moja hununua sh.70,000, lakini kwa Nairobi huuza kwa sh. 135,000 au zaidi, na kwa Dar es Salaam bei yake ni sh. 95,000 ama zaidi.
Siku yangu inakuwa imemalizika nikiwa nimeitumia kujifunza mambo mengi kuhusu mwalo wa dhahabu. Pia napata jibu kwa nini mahali hapo panaitwa ‘mwaloni’. Kumbe ni mwalo wa dhahabu!.
Hata hivyo kazi zinazofanyika mahali hapo zina manufaa gani kwa taifa? Najiuliza. Je serikali inapata kodi yoyote? Maswali hayo namtupia Katibu wa Wilaya ya Ikungi wa Chama Cha Wachimbaji wa Wadogo, Pili Said, ambaye pia ni mchimbaji sehemu hiyo.
“Huku tunachimba tu, lakini wamiliki wa leseni ndio wanaolipa kodi pamoja na mrahaba maana wao ndio wanafahamika serikalini, lakini wengine kama wachimbaji wadogo wa migodi na wanaookota mabaki ya mawe kwenye migodi hawalipi kitu. Hao hawatambuliwi na serikali maana leo wapo hapa na kesho hawapo, “anasema.
Maelezo hayo ya Pili yananisukuma nimsake Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) mkoa wa Singida, Jumbe Samson, kujua kwa nini watu ‘wavune’ pesa ilhali hakuna ofisi ya TRA sehemu hiyo kukusanya mapato?
“Hatuna mchimbaji mdogo anayelipa kodi, maana hawa (wachimbaji wadogo) ni sawa na ‘informal sector’ (sekta isiyo rasmi) ambapo hakuna sera yoyote ya nchi inayowabana walipe kodi. Sana sana ili tuweze kuwabana walipe ni mpaka wanapofikia hatua ya kuwekeza katika shughuli zenye rekodi kama nyumba, gesti au maduka, hapo ndipo tunaweza kuwatoza kodi, “anasema.
Anasema wanajua wachimbaji hao wanapata fedha nyingi, lakini hawana njia ya kuwabana walipe kodi kwa vile shughuli zao hazina rekodi na pia zimetawaliwa na usiri, mambo ambayo huwafanya wakose mahali pa kuanzia.
Samson ananiambia changamoto hiyo ni sawa na ile wanayokumbana nayo watu wa Wizara ya Nishati na Madini kupata takwimu sahihi ili waweze kutoza mirahaba kwa wachimbaji wakubwa na wanaomiliki leseni za uchimbaji. Hizo ni changamoto nazoambiwa utatuzi wake unasubiri watunga sera na serikali yenyewe kuzishughulikia.
Ama kweli haya ni maajabu, hawa watu wanajitafutia riziki wenyewe lakini mwisho wa siku utaambiwa wanapaswa kuondoka sehemu hiyo na eti mwekezaji ambaye ana helaa nyingi kapatikana kwa ajili ya kuwaletea maisha bora. Ni vyema serikali ikawawekea mazingira mazuri ili mwisho wa siku nao waje wawe bora kimaisha.
Tanzania hii ni ya Watanzania na siku zote itabaki kuwa yetu. Hawa ni watu wanaohitaji usaidizi mkubwa wa serikali kuwaendeleza. Naishia hapa kwa sasa, lakini wamiliki wa mtandao huu nawaomba whamasishe habari za aina hii ambazo zinatoa picha kwa jamii kuwa, kumbe kuna shughuli ambazo zipewa mgongo na serikali ambazo zina msaada mkubwa katika ukuaji wa taifa letu.
Good experience Kulwa, keep it up!
Shukran Juma, nashukuru kwa kunipa moyo!