MWAKILISHI na Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Raia Mwema mjini Arusha Paul Sarwat akiwa na mke wake wamenusurika kupoteza maisha baada ya gari yao aina ya Suzuki Vitara kugongwa na kuharibika vibaya.
Akizungumza na FikraPevu kwa njia ya simu muda si mrefu, Sarwat amesema, ajali hiyo ilitokea majira ya Saa 3 usiku wa kuamkia leo akiwa anarejea nyumbani na mke wake.
Mwandishi huyo anayeishi maeneo ya Kwamrefu barabara ya Moshi – Arusha alidai akiwa anaendesha gari yake mara alihamaki kuona gari aina ya Toyota Land Cruiser ikilazimisha kuzipita gari nyingine bila utaratibu.
“Hiyo gari iliyotugonga ilianza kugonga magari mengine kama matatu ndio ikatufikia na sisi. Gari imeharibika kweli ila mimi naendelea vizuri,” alisema Sarwat na kuongeza:
“Mke wangu ameenda Hospitali ya Mount Meru kuangaliwa miguu, kifua na mbavu kwani alikuwa analalamika maumivu. Tunamshukuru Mungu tumetoka wazima,” alisema.
Hata hivyo alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Thobias Andengenye ili kuzungumzia ajali hiyo hakuweza kupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa.
Sarwat, ndiye mwandishi aliyechunguza na kuandika habari za wizi wa wanyamapori hai na baadae habari hii kuibua mjadala mkali.
Ni takribani mwezi mmoja sasa tangu Naibu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Daniel Mwakiteleko apoteze maisha kutokanana ajali ya gari iliyotokea jijini Dar es Salaam.
Nadhani hiyo itakuwa ni ajali ya kawaida kama zilivyo ajali nyingine. Nawapa pole wote waliopata ajali hiyo. Mungu awasaidie waweze kupata nafuu upesi na kurejea katika majukumu yao ya kila siku.
Kama tutajenga hisia ya hujuma, sidhani sana kama tutakuwa tuko sawa, ingawa nalo laweza kuwa moja ya sababu za ajali. Nashukuru kwamba wote ni wazima, naamini watatibiwa na watapona.