Mwanza: Mahakama yawatia ndani Diwani, Katibu wa CHADEMA

Sitta Tumma

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimepata pigo kubwa baada ya Mahakama kuwaweka ndani Diwani wa Kata ya Kirumba jijini Mwanza, Dan Kahungu pamoja na Katibu wa Chadema Wilaya ya Ilemela, John Anajus kwa kosa la kukaidi amri halali ya mahakama, iliyozuia uchaguzi wa nafasi ya Meya na Naibu wake katika Manispaa hiyo.

Mbali na viongozi hao wa Chadema kupelekwa mahabusu ya Gereza Kuu la Butimba, pia Mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, imeagiza wakamatwe kisha kufikishwa mahakamani Mkurugenzi wa Oganaizesheni wa Chadema taifa, Benson Kigaila na aliyekuwa Meya wa Jiji la Mwanza ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Tendaji ya chama hicho, Josephat Manyerere kwa kosa hilo hilo la kudharau amri ya mahakama.

Amri hiyo ilitolewa hii leo na Hakimu Mkazi Mfawidhi mkoani Mwanza, Angelo Rumisha, kufuatia kesi namba 69/2012 iliyopo mahakamani hapo dhidi ya watuhumiwa sita kutoka chama hicho, ambapo alisema mara baada ya watuhumiwa hao kukamatwa mahakama itatoa hukumu yake kwa pamoja.


Akitoa  amri hiyo, Rumisha alisema mahakama haiwezi kutoa adhabu kwa baadhi ya watuhumiwa, na kwamba agizo la kutaka wakamatwe Manyerere na wenzake ni kutaka mahakama iheshimiwe, mara inapotoa amri zake halali kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kupitia  kesi hiyo yenye namba 69/2012, Rumisha aliwataja wengine wanaotakiwa kukamatwa na jeshi la polisi kisha kufikishwa mahakamani hapo ni pamoja na Mkurugenzi huyo wa Oganaizesheni ya Chadema taifa, Kigaila, Katibu wa mwenezi wa Chama hicho wilaya ya Ilemela, Kalod Majura pamoja na mkuu wa Mdhamini wa Chadema.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na wakili wa upande wa mlalamikaji mahakamani hapo, Salum Magongo kwamba watuhumiwa wote kwa pamoja walishiriki  kikao cha kutangaza uamzi wa kumfukuza udiwani, Henry Matata wa Chadema (kata ya Kitangiri), kabla pingamizi lililokuwa limewasilishwa mahakamani na diwani huyo halijatolewa maamuzi na mahakama.

"Mteja wangu Henry Matata aliweka pingamizi mahakamani baada ya Kamati Tendaji ya Chadema kutangaza kumvua uanachama kinyume cha taratibu. Lakini watuhumiwa wote wa kesi hii walishiriki kuvunja sheria kwa kumtangaza kumfukuza udiwani", alidai mahakamani hapo wakili Magongo.

Aidha, Wakili huyo aliendelea kudai kuwa, kwa kufanya hivyo washtakiwa hao walipuuza amri halali ya mahakama iliyotolewa na mahakama Septemba 15 mwaka huu, kinyume cha sheria na taratibu.

Hata hivyo, hakimu Rumisha aliamuru diwani huyo wa kata ya Kirumba, Kahungu pamoja na Anajus waende mahabusu katika gereza la Butimba, hadi hapo watuhumiwa wengine watakapokamatwa na jeshi la polisi kisha kuhukumiwa kwa pamoja.

Wadadisi wa mambo wanadai kwamba, kosa la kupatikana kudharau amri halali ya mahakama adhabu yake ni kwenda miezi sita, au kulipa faini, hivyo viongozi hao wa Chadema huenda wakahukumiwa kutumikia adhabu kadri itakavyoamriwa na mahakama.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – FikraPevu, Mwanza

1 Comment
  • chadema wajifunze kuonya wanachama wake vinginevyo watafukuza wanachama wote tunatambua kwamba hakuna binadamu aliyekamilika, hii itasaidia kukiweka chama katika muonekano bora zaidi hata nje ya nchi lakini kama kuina mamluki toka ccm au pamoja na vyama vingine basi hawana budi kufukuzwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *