Mwanza: Vifaa vya upasuaji vyakosa kazi, vyafungiwa stoo licha ya kuwepo kwa jengo na watendaji

Jamii Africa

WAKATI Serikali ikitumia fedha nyingi kuboresha na kusogeza karibu na wananchi huduma ya afya, vifaa vya upasuaji katika Kituo cha Afya cha Igoma jijini Mwanza, vimefungiwa ndani bila kufanya kazi husika.

Mbali na kufungiwa ndani ya chumba vifaa hivyo, jengo la upasuaji illilojengwa na kukamilika mwaka 2015 katika kituo hicho cha afya limebadilishiwa matumizi ikiwa ni pamoja na chumba kimojawapo kugeuzwa kuwa stoo ya kutunzia vifaa mbalimbali vya kituo hicho.

Kukosekana kwa huduma ya upasuaji kituoni hapo kunahatarisha usalama wa wananchi hususan mama wajawazito.

Baadhi ya watumishi wa kituo hicho kinachodaiwa kuhudumia watu 150 kwa siku moja wanasema, wastani wa watu 10 hadi 15 hukosa huduma hiyo kila mwezi, kwa sababu chumba cha upasuaji kilichopo hakifanyi kazi.

Kwa mujibu wa uchunguzi, wagonjwa husafirishwa umbali wa zaidi ya kilometa 10, kwenda Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana ya Butimba, kwa ajili ya upasuaji.

 

Wananchi wataka viongozi watimuliwe kazi

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Igoma waliozungumzia kero hiyo, wanasema kitendo cha kukosekana huduma ya upasuaji kwenye kituo hicho kinahatarisha zaidi maisha ya mama na mtoto.

“Viongozi wanavuta vitambi tu bila kujali maisha ya wagonjwa. Haiwezekani jengo lipo, vifaa na madaktari wa upasuaji wapo halafu huduma haipo.

“Waziri wa Afya (Ummy Mwalimu) aje awatumbue viongozi wanaokwamisha kuwapo upasuaji katika kituo hiki,” anasema Helen Maduhu, mkazi wa Kata ya Igoma.

Wanawake wengine waliohojiwa juu ya kukosekana huduma hiyo muhimu ya upasuaji kwenye Kituo cha Afya cha Igoma ni Ester Emmanuel, Joyce Musa, Stephania Herman, Minza Josee, Edna Samuel na Christina Ndoto.

“Bila Mungu wakati mtu anasafirishwa kupelekwa Hospitali ya Sekou Toure au kule Butimba, adiko kusika nulu ndama aho, ocha mnhu,” anasema Christina akimalizia kwa lugha ya Kisukuma akimaanisha kwamba, bila msaada wa Mungu mtu hafiki mbali atakuwa amefariki dunia.

Sauti ya Minza Josee

Baadhi ya wagonjwa wanashauri uongozi wa kituo hicho cha afya na mamlaka ya Jiji la Mwanza, uwajibike kutatua changamoto hiyo, ili kunusuru maisha ya watu.

Serikali ilishatumia zaidi ya Shs. 65 milioni kujenga jengo hilo; hiyo ni kwa mujibu wa Adam Chagulani, aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo mwaka 2015.

Kwa mujibu wa uchunguzi, jengo hilo la upasuaji lilijengwa kwa fedha za Mfuko wa Afya (Basket Fund). Mchoro wa jengo ulitolewa na Wizara ya Afya.

“Jengo lilijengwa ili upasuaji wa dharura ufanyike hapa. Kinachokwamisha ni baadhi ya viongozi waliopo hawawajibiki,” anasema Chagulani.

 

Madhara ya ukosefu huduma bora

Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Julai mwaka 2012 zinasema, Tanzania ni kati ya nchi 10 zinazoongoza kwa vifo vya wanawake wajawazito.

Kitabu cha masuala ya afya kilichotolewa na Serikali na kutiwa saini na aliyekuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wakati huo, Regina Kikuli, kinasema, nchi hizo 10 zinachangia kiasi cha kati ya asilimia 61 na 66 ya vifo vya wanawake na watoto wachanga duniani.

“Hapa Tanzania, kila akina mama 100,000 wanaojifungua 454 hufariki dunia. Katika kila watoto 1,000 wanaozaliwa hufariki dunia (Utafiti wa idadi ya watu na afya Tanzania 2010).

“Asilimia 17 ya wanawake wajawazito hufariki dunia kwa shinikizo la damu linalosababishwa na ujauzito/kifafa cha mimba,” inaeleza sehemu ya Kitabu hicho cha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii cha mwaka 2012.

Hakuna taarifa za watu kupoteza maisha kwa sababu ya kukosa huduma ya upasuaji kwenye Kituo cha Afya cha Igoma, ingawa vifo vinaweza kutokea iwapo Serikali haitachukua hatua za haraka.

Baadhi ya madaktari wa Kituo hicho cha Afya cha Igoma wanasema kwa sasa jengo hilo linatumika kutoa huduma kwa watu wanaoishi na virusi vinavyosababisha maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi (H.I.V), Kifua Kikuu (TB) na wazee.

Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Igoma, Dk. David Rwezaula, alipoulizwa akasema: “Mimi siyo msemaji, mtafute Mganga Mkuu wa Jiji atakueleza. Lakini kuna marekebisho fulani yanatakiwa kufanyiwa."

Mganga Mkuu wa Jiji la Mwanza, Dk. John Andrew, amethibitisha kutokuwapo kwa huduma hiyo ya upasuaji Kituo cha Afya Igoma.

Mganga Mkuu- Jiji la Mwanza (DMO), John Andrew

Alipotakiwa kueleza sababu ya kutokuwapo huduma hiyo ya upasuaji, licha ya miundombinu kuwapo, Dk. Andrew anasema:  “Hilo jengo halina chumba cha kumwandalia mgonjwa kabla ya upasuaji. Hakuna pia chumba cha kuzindukia mgonjwa, baada ya kufanyiwa upasuaji.”

Hata hivyo, mwandishi wa makala haya, amethibitisha kutokuwapo vyumba hivyo.

 

Nini kifanyike?

Wananchi na wadau wa afya Kata ya Igoma, wametoa siku 30 kwa uongozi wa Jiji la Mwanza, huduma ya upasuaji kwenye kituo hicho cha afya iwe imeshaanza, la sivyo wataitisha maandamano.

Wanataka pia viongozi waliosababisha kukwama kwa huduma hiyo wawajibishwe kwa mujibu wa sheria, ili liwe fundisho kwa wengine.

Diwani wa Kata ya Igoma, Musa Magabe, yeye anasema: “Tunataka huduma ya upasuaji ianze haraka. Haiwezekani wananchi wahangaike kutafuta huduma, jengo lipo na vifaa vya upasuaji vimefungiwa tu ndani ya chumba.”

Asilimia 90 ya wananchi wa Kata ya Igoma waliohojiwa wanataka uongozi wa Jiji la Mwanza kutenga fedha, kuhakikisha huduma ya upasuaji inaanza haraka kwenye kituo hicho cha afya.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *