Na Juma Ng’oko, Mwanza
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja amesema mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM) hana hekima na pia uelewa wake ni mdogo kuhusu vipengere vya katiba ya Chama hicho tawala.
Mgeja ametoa kauli hiyo kwa njia ya simu, ikiwa imepita siku moja tangu Lembeli alipowaambia Waandishi wa habari Jijini Dar es salaam Aprili 26 mwaka huu kwamba bado kuna viongozi wa CCM wakiwemo wa ngazi ya mkoa wa Shinyanga ambao wanapaswa kujivua gamba kutokana kile alichodai kuwa ni mawakala wa mafisadi wakubwa nchini.
“Mimi sipendi kuzua malumbano yasiyo ya lazima na ambayo hayana tija kwa chama; ingawa sijui kama huyu mwanachama mwenzangu anazungumza maneno kama hayo akiwa kama Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi au kama nani!” alihoji Mgeja wakati alipohojiwa na Fikra Pevu kwa njia ya simu.
Kwa mujibu wa Mgeja, CCM siyo kampuni na kwamba si kila mwanachama ndani ya chama hicho anapaswa kuzungumza masuala ya chama kupitia vyombo vya habari.
“CCM siyo kampuni, bali ni chama ambacho kina wasemaji wake kwa mujibu wa katiba ya nchi bhwana! …inawezekana huyu jamaa yetu (Lembeli) haifahamu vizuri katiba ya chama ndiyo maana inafikia hatua ya kuzungumza bila utaratibu” alidai Mgeja .
Alifafanua kwamba Katiba ya CCM imeainisha majukumu, wajibu wa kiongozi pamoja na njia za kuzungumzia masuala yanayohusu chama hicho.
Mwenyekiti huyo alidai kauli iliyotolewa na Lembeli kwamba ni vema kamati ya siasa ya mkoa wa Shinyaga ijivue gamba haina maslahi kwa chama wala taifa, kwa vile ni mtazamo hafifu alionao mheshimiwa Lembeli.
Akizungumizia shutuma kwamba uongozi wa CCM mkoa wa Shinyanga ndio umesababisha baadhi ya majimbo yachukuliwe na vyama vya upinzani katika uchaguzi mkuu uliopita, Mgeja alidai kuwa wenye haki ya kuibua hoja hiyo ni wajumbe wa kamati za siasa za wilaya mkoani humo.
Alidai kuwa katika kikao cha tathmini ya uchaguzi kilichofanyika hivi karibuni mkoani humo hakuna wilaya hata moja iliyotoa hoja ya aina hiyo.
Aliendelea kusisitiza kuwa mbunge ni mtu mdogo sana ambaye hapaswi kujadili mstakabali wa chama hicho.
“…mimi ni kiongozi wa kimkoa, yeye kama mbunge ni mdogo sana ambaye kutoa kauli hiyo ni sawa na kuchezea sharubu” alisisitiza mwenyekiti huyo huku akiahidi kuitisha kikao na waandishi wa habari ili aweze kutoa ufafanuzi kuhusiana na shutuma zinazomkabili.
Hata hivyo, Mgeja hakuwa tayari kutaja kwamba ni wapi atakutana na waandishi wa habari ili aweze kupata fursa ya kujibu tuhuma zinazomkabili.
Aprili 26 mwaka huu, Lembeli akiwa Jijini Dar es salaam alisema kuwa CCM ukiwemo uongozi wa chama hicho mkoani Shinyanga wanapaswa kujiuzulu kwa madai kwamba kimejaa mawakala wa mafisadi.
Alisema kamati ya siasa ya mkoa wa Shinganga inayoongozwa na Hamisi Mgeja, nayo inapaswa kujivua gamba kwa sababu kimeshindwa kutimiza wajibu wake.
Kwa mujibu wa Lembeli, Mgeja pamoja na wajumbe wa kamati ya siasa wamechangia baadhi ya majimbo kutwaliwa na wabunge kupitia vyama vya upinzani mkoani humo.
Alidai kwamba hali hiyi imesababisha wananchi wasiwe na imani na chama pamoja na serikali yao.
Mbunge huyo alisema ushahidi uko wazi kuwa mkoa wa Shinyanga ndio uliokuwa ngome kuu ya Chama Cha Mapinduzi, sasa umegeuka kimbilio la vyama vya upinzani ambapo vyama hivyo vimefanikiwa kuvuna kura za kishindo katika nafasi za ubunge wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31 mwaka jana.
Aliyataja majimbo yanayowakilishwa na wabunge kutoka vyama vya upinzani mkoani Shinyanga kuwa ni jimbo la Bariadi Mashariki, Maswa mashariki, Maswa Magharibi, Bukombe pamoja na jimbo la Meatu.
Lembeli alisema kupotea kwa majimbo hayo kumesababishwa na ufisadi uliopo miongoni mwa viongozi wa CCM mkoani Shinyanga.
ALIONGELEA ARUSHA NA SI DAR KAMA ULIVOANDIKA NDUGU YANGU