Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amesimamisha utoaji wa hati za kusafiria za makundi ya vijana wanaosafiri kwenda nje ya nchi kwa kuwa wananyanyaswa na kutumikishwa kwenye kazi hatarishi na ameviagiza vyombo vya dola kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watu wote wanaohusika na ukatili huo.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari, Waziri Nchemba amesema wamepata taarifa kuwa vijana wanaosafiri kwenda kufanya kazi nje ya nchi wanatumikishwa kwenye kazi zingine ambazo hawajaingia mkataba.
“Tumepata taarifa hizo za mateso ya watu wetu wanapokwenda nje ya nchi kwa kazi tofautitofauti wengine wakifika kule wananyang’anywa pasipoti zao wanatumikishwa kitumwa, wengine wananyanyaswa kikatili lakini wengine wanalazimishwa kuelekea kwenye mielekeo ambayo hawakuwa na nia nayo”, amesema Waziri Mwigulu.
Amebainisha kuwa alikutana na mawaziri wa wizara zingine wanaohusika na ulinzi wa raia na kukubaliana kila wizara kuchukua hatua ya kuwanusuru watanzania hao ambao wanapitia mateso mbalimbali wakiwa nje ya nchi.
“Tumefanya mawasiliano na wizara zote zinazohusika na tumekubaliana kuchukua hatua kila mmoja kwenye wizara yake. Sisi kwenye wizara yetu nitoe tamko na kueleza kwamba nasimamisha pasipoti za jumla kwa makundi ya vijana ambao wamekuwa wakikutana na mikasa hiyo ya kunyanyaswa, kutumikishwa, kuteswa kikatili”, amesema Waziri Nchemba.
Ameongeza kuwa watanzania hao wamekuwa wakiwekwa rehani , kunyang’anywa hati za kusafiria na wengine kutumikishwa kwenye biashara ya madawa ya kulevya, “Na wengine kuwekwa ‘bond’ zikiwemo fedha za madawa ya kulevya, kwahiyo nasimamisha utoaji wa pasipoti kwa makundi ya watu”.
Ameviagiza vyombo vya dola kuwatafuta na kuwafikisha mahakamani watu wanaohusika na usafirishaji wa watanzania nje ya nchi ambapo wakifika huko huwaingiza kwenye biashara ya utumwa.
“Lakini wanaohusika na shughuli hizi waendelee kutafutwa, wakamatwe wafike kwenye mkono wa sheria ili sheria iweze kufuata mkondo wake”, ameagiza Waziri Nchemba.
Pia ameagiza kukamatwa kwa watu wanaotoa vibali vya wageni wanaoingia Tanzania lakini wakifika nchini wanafanya kazi tofauti na zile zilizoainishwa kwenye vibali hivyo.
Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko mengi yanayoripotiwa kwenye vyombo vya habari ya watu ambao wanatumikishwa na kuteswa katika nchi za Oman, China pamoja Saudia Arabia.
Human Rights Watch Wanena
Novemba 14 mwaka jana, maafisa wa serikali ya Tanzania jijini Dar es Salaam waliwazuia Human Right Watch kufanya mkutano na waandishi wa habari kuzindua ripoti juu ya unyanyasaji wa watumishi wa ndani wahamiaji wa Kitanzania walioko Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Ripoti hiyo yenye kurasa 100 ilieleza kuwa, “Watumishi wa ndani wa Kitanzania wanaofanya kazi Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wanakumbana na saa nyingi za kazi, kutokulipwa mishahara, na unyanyasaji wa kimwili na kijinsia. Sheria kandamizi za udhamini wa visa katika nchi hizo na mapungufu katika sera za Tanzania zinawaacha wanawake kupambana na unyonyaji”.
“Watumishi wa ndani wengi wa Kitanzania walioko Oman na UAE wanafanyishwa kazi kupita kiasi, wanalipwa pungufu, na wananyanyaswa nyuma ya pazia,” anasema Rothna Begum, Mtafiti wa haki za wanawake Mashariki ya Kati na Human Rights Watch katika ripoti hiyo .
“Wafanyakazi ambao walikimbia waajiri wanyanyasaji au mawakala walituambia polisi au maofisa wa balozi zao waliwalazimisha kurudi, au iliwabidi waacha mishahara yao na kupoteza miezi kadhaa kukusanya fedha kwa ajili ya tiketi kurudi nyumbani.”
Hata hivyo, Human Rights Watch inashauri kuwa Tanzania haina budi kupitisha mikakati maalumu kuzuia na kukabiliana na unyanyasaji, ikiwa ni pamoja kanuni kali na uangalizi wa uajiri, programu za mafunzo ya haki, na msaada wa kujitosheleza kutoka katika balozi ikiwa ni pamoja na kulipa gharama za tiketi kurudi nyumbani.