Neema yapotea, makaa yaleta balaa

Kassian Nyandindi

WANANCHI wa Kijiji cha Liyombo kata ya Ruanda wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wameonyesha wasiwasi wao juu ya kudaiwa kutoroshwa kwa makaa ya mawe pamoja na ulipwaji wa  fidia watakazo pata kwa mali zao, baada ya kufahamika kuwa kijiji hicho kimejengwa juu ya mwamba wa makaa ya mawe ambayo yanatarajiwa kuanza kuchimbwa kabla ya mwisho wa mwaka huu iwapo taratibu za vibali kwa mwekezaji zitakamilika.

Baadhi ya wakazi  wa  kijiji hicho kilichopo katika kata ya Ruanda ambao ni Elia Hyera,John Mbepera na Joakimu Nchimbi wakizungumzia suala hilo wametoa wito kwa serikali kusimamia na kuhakikisha wanalipwa fidia pamoja na kuwa makini na kufuatilia sampuli za makaa hayo zinazopelekwa nje ya nchi kwa madai ya kwenda kufanya utafiti wa ubora wa makaa ya mawe kabla ya kuanza kuchimbwa.

“Hawa wawekezaji wamechukua sampuri tani 1000 na kupeleka nchini Afrika ya kusini kwa njia ya ,meli kupitia bandari ya Ndumbi ziwa Nyasa, kwa ajili ya utafiti wa awali,halafu wanasema bado zinatakiwa tani 10,000 ili kukamilisha utafiti na kuwaridhisha wanunuzi wa makaa hayo nje ya nchi,sisi wananchi wanatuchanganya mara wanasema majibu yanaonyesha kuwa mkaa huo ni bora hatujui tena tani nyingine za nini,wizara ya madini inatakiwa kusimamia hali hii isije ikiwa ni janja ya nyani’’,alitahadharisha Elia Hyera.

Kampuni ya Tancoal Energy Limited (TANCOAL) , shirika la Taifa la maendeleo ( NDC), pamoja  na Pacific Corporation ya Afrika Mashariki (PCAM), walianza utafiti wa kuchimba makaa ya mawe katika  kijiji cha Liyombo ambapo utafiti umebaini eneo hilo kuwa na mkaa wa kutosha  na wenye ubora. Utafiti huo ulianza  April mwaka 2008 kwa kuangalia wingi wa makaa ya mawe,unene wa mwamba na ubora wa makaa hayo

Katika makala haya napenda kuelezea juu ya uharibifu wa mazingira unaofanywa katika eneo la Bandari ya Ndumbi kata ya Mbaha iliyopo Ziwa Nyasa, wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma.

 

Bandari hiyo imekuwa ikitumika na Kampuni ya Tancoal Energy kusafirisha mkaa wa mawe kwenda nchi ya Malawi, ambapo makaa hayo huchimbwa na kampuni hiyo katika mgodi wa Ngaka uliopo kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilaya ya Mbinga mkoani humo.

Mradi huo wa makaa ya mawe unamilikiwa na kampuni ya ubia ya Tancoal Energy ambayo asilimia 30 ya hisa zake zinamilikiwa na serikali, kupitia shirika la maendeleo la Taifa NDC na asilimia 70 ya hisa zinamilikiwa na mwekezaji wa kampuni ya Intra Energy.

Uchunguzi umebaini pia mazingira hususani makazi ya watu yaliyopo karibu na bandari hiyo yapo katika hali tete kutokana na uchafuzi wa mazingira ikiwemo vyanzo vya maji, kujenga vyoo na mifereji ya kupitisha taka vimiminika katika eneo hilo.

Kufuatia hali hiyo malalamiko ya hapa na pale yamekuwa yakijitokeza miongoni mwa wananchi na kuiomba serikali kuingilia kati ili kuweza kumaliza kero hiyo kutokana na mazingira ya nyumba zao kuzungukwa na vumbi kali na kusababisha watoto kuugua mafua na kikohozi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao ambao walitaka majina yao yasitajwe, wanasema wamekuwa wakiathirika na vumbi la mkaa huo ambapo limekuwa likiwapa shida pale magari makubwa (Malori) ambayo husafirisha toka kwenye huo mgodi ambako yanachimbwa, wakati mwingine maturubai ambayo yamekuwa yakitumika kufunika katika magari hayo hayafunikwi vizuri, kiasi ambacho vumbi hilo limekuwa likitimka na kuelekea katika makazi yao baadaye kuwa kero kwao.

 

Wamesema malalamiko hayo ni ya muda mrefu licha viongozi husika kwenda katika eneo hilo, lakini hakuna hatua za haraka zilizochukuliwa katika kunusuru hali hiyo ili isiweze kuendelea kutokea.

 

Kadhalika walibainisha kuwa baadhi yao ambao walikuwa na makazi karibu na bandari hiyo baada ya kufikisha kilio hicho katika ngazi za serikali, ndipo hatua ilichukuliwa kwa kuwahamisha na kuwalipa fidia ili wasiweze kuendelea kupata adha hiyo.

Wamesema pamoja na kuhamishwa na kupelekwa mbali kidogo na eneo hilo la bandari, huko walikopelekwa licha ya kuahidiwa kupewa huduma za msingi ikiwemo kuchimbiwa visima vya maji safi na salama ni muda mrefu umepita hakuna utekelezaji uliofanyika hadi sasa na wao wanaendelea kupata shida.

Kwa ujumla vumbi la mkaa wa mawe limekuwa likiendelea kuzalishwa kwa kiasi kikubwa katika eneo la bandari ya Ndumbi, kutokana na shughuli ya upakiaji na usafirishaji wa makaa hayo wataalamu husika kutozingatia taratibu za kuzuia lisisambae katika makazi ya watu.

Eneo hilo  la bandari hakuna hata vyoo vilivyojengwa kwa ajili ya wafanyakazi, mifereji kwa ajili ya kupitisha maji machafu yanayotoka kwenye eneo hilo ili yasiende kuchafua maji ya mito na ya ziwa Nyasa ambayo hutumika na wananchi katika shughuli za maisha yao ya kila siku.

Badala yake hali hiyo imeendelea kudumu kwa muda mrefu na huenda ikaleta madhara makubwa hapo baadaye katika jamii, ambayo muda mwingi hutumia maji ya mito na ziwa hilo katika shughuli zao za maisha ya kila siku.

Pamoja na mambo mengine watu wameendelea kuelekeza lawama kwa uongozi wa wilaya ya Nyasa, ambapo wengine wanahofia huenda vumbi hilo likaathiri hata viumbe hai wakiwemo samaki ambao huishi katika ziwa Nyasa.

Pia imebainika kwamba vumbi kali la mkaa huo limekuwa likienea katika vijiji vilivyokuwa hata jirani na mgodi huo ulipo hasa pale yanaposafirishwa kwenda katika bandari hiyo ya Ndumbi iliyopo ziwa Nyasa, Kiwira mkoani Mbeya na kiwanda cha kuzalisha saruji Tanga kilichopo mkoani Tanga, huenda hali ya kiafya kwa wananchi wale ikawa hatarini endapo hatua husika hazitachukuliwa kwa uharaka.

Mpango wa utunzaji wa mazingira na kujali afya za watu ni utaratibu wa kutathmini na kupendekeza namna mbalimbali ya matumizi muhimu ili kuinua hali za maisha ya wananchi kuwa salama, kupunguza umaskini na matatizo  yanayoweza kujitokeza hapo baadaye katika eneo husika.

Usimamizi na matumizi bora ya rasilimali hizo tokea enzi za mababu zetu imekuwa ikielezwa ni njia pekee ya kutatua migogoro, katika jamii,  kaya au kabila fulani liweze kuepukana na matatizo ambayo mara nyingi huleta kero kubwa.

Katika baadhi ya maeneo hapa nchini, ukipita utaona au kushuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira unavyofanywa, na kusababisha usalama mdogo wa maisha ya wananchi ikiwemo hata kuporomoka kwa uchumi.

Uharibifu huo huwa wa namna moja au nyingine ambao hufanywa na binadamu, hali hii inachangia kuwepo kwa mabadiliko ya tabia nchi na kuifanya jamii ianze kutanga tanga hapa na pale kutafuta huduma zao za  msingi.

Theluthi mbili ya bara la Afrika, lipo katika hatari ya kuenea kwa hali ya jangwa ambapo zaidi ya asilimia 60 ya eneo lote nchini, limeathiriwa na uharibifu wa mazingira hivyo yatupasa sasa kuchukua tahadhari mapema ili kuweza kudhibiti hali hiyo isiweze kuendelea kujitokeza.

Utunzaji wa mazingira ni kitu pekee ambacho kimekuwa kikipewa kipaumbele siku zote, kutokana na ukweli kwamba ndiyo muhimu katika kuendeleza maisha ya kila siku ya kiumbe chochote kilichokuwa hai hapa duniani.

Mkurugenzi mtendaji wa maendeleo ya wilaya hiyo, Shaibu Nnunduma hakuweza kupatikana ofisini kwake kwa madai kwamba yupo safarini, ili aweze kuzungumzia malalamiko hayo ambapo hata simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

Meneja wa Mgodi wa Makaa ya Mawe Tancoal Energy, Isaac Mamboleo alipohojiwa na mwandishi wa makala haya alikiri kuwepo kwa matatizo hayo na kusema wapo katika mchakato wa kuyatatua ikiwemo suala la udhibiti wa vumbi hilo lisiweze kusambaa katika makazi ya watu.

“Hivi karibuni Baraza la Taifa na usimamizi wa mazingira lilikuja kwetu na kuangalia mazingira haya baada ya kuona kuna matatizo walitufungia kwa siku saba tusiendelee na shughuli yeyote ya usafirishaji wa makaa hadi tutakapotekeleza mambo haya ya msingi ambayo wanalalamika, lakini hivi sasa ninavyosema kazi ya kuyatatua tumeanza na kibali kimetolewa cha usafirishaji tutaendelea na kazi ya kuyasafirisha huku mchakato wa kukamilisha matatizo yaliyopo ukiendelea”, anasema Mamboleo.

Kana kwamba haitoshi ni jambo la kusikitisha na kushangaza kuona Meneja huyo akisema kibali wamepewa cha kazi ya usafirishaji huo wakati mchakato wa kukamilisha matatizo hayo ya wananchi ukiendelea, binafsi nasema hali hii inaonesha wazi kuna mkono wa mtu ndani yake ambaye huwafanya Tancoal Energy kutamba kifua mbele kwamba wataendelea na kazi ya usafirishaji huo huku matatizo hayo yakiendelea kutesa wananchi ni vyema sasa serikali ikachukua hatua madhubuti mapema ili kuweza kumaliza kero hizo ambazo zinaendelea kutesa wanakondoo hawa wa Mungu ambao hawana hatia.

Sote tunafahamu Tanzania ni nchi ambayo imejaliwa rasilimali nyingi ambazo zikitumika kwa ufasaha, taifa hili wananchi wake kwa asilimia kubwa wanaweza kuondokana na umasikini na hata kero za hapa na pale hivyo viongozi wetu ambao ndio wamepewa jukumu la kusimamia hilo wanaonekana kutozingatia taratibu husika, na kusababisha kelele na hata maandamano yasiyokuwa ya lazima ambayo yanafanywa na wananchi wa eneo fulani ambako kero husika inatokea, yakilenga kudai haki zao.

Nionavyo kukalia kimya malalamiko ya wananchi ndipo ulipo msingi wa matatizo mengi ya nchi hii, kila mtu anapenda na kutaka kusifiwa lakini hakuna anayetaka kupokea lawama au hata wajibu wa kuwajibika wengine wakifanya mabaya kwa niaba yao.

Hii leo sio Tanzania ile ya wanyonge ambao wanataka ukombozi wa kweli katika mambo yanayohusu maisha yao na hawana muda wa kusikiliza hadithi za kulindana na kupuuza malalamiko ya wananchi kama vile tunavyoona sasa ulegevu katika kuchukua hatua dhidi ya wanaohusika na malalamiko haya ya makaa ya mawe. 

Kuendelea kwa matukio ya wananchi  kulalamika kudai haki zao za msingi, kunaonesha serikali yetu kutochukua hatua za haraka pale jamii inapowasilisha matatizo yao ya msingi, hivyo yatupasa sasa tubadilike tutekeleze mambo kwa vitendo na uhalisia uonekane sio kupiga porojo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *