Ngeleja aibomoa kambi ya CHADEMA, Wenyeviti, Makatibu watimkia CCM

Jamii Africa

WAZIRI wa Nishati na Madini, William Mganga Ngeleja ameibomoa ngome ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), baada ya viongozi wa chama hicho Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza kurudisha kadi na kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Miongoni mwa viongozi wa Chadema waliohamia CCM na kutambulishwa jana kwenye mkutano wa hadhara mjini Sengerema mkoani Mwanza ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Sengerema, Ayub Malima, Katibu wa chama hicho wilaya, Kesi Misalaba, Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema Sengerema, Sarah Mathayo na mwenyekiti wa Vijana wilaya Chadema, Stanslaus Pstory.

WAZIRI wa Nishati na Madini, William Mganga Ngeleja (katikati), akimpongeza aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, Ayub Malima, baada ya kiongozi huyo na wenzake saba kutangaza rasmi kuhamia CCM, kwenye mkutano wa hadhara mjini Sengerema. Kushoto ni mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo, Jaji Tasinga Gabanyaga

Viongozi wengine wa Chadema waliohamia CCM ni Katibu wa Vijana wilaya hiyo, Frenk Dotto, Lusia Mussa Mjumbe, pamoja na Sayi Busumabu mjumbe pamoja na mwanachama mmoja wa Chama cha Wananchi (CUF), Peress Essau ambaye mwaka 2005 aligombea ubunge jimbo hilo la Sengerema.

Wakizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Sengerema mjini, ambao uliandaliwa na Waziri Ngeleja na mbunge wa jimbo la Sengerema (CCM), kwa ujumla wao viongozi hao walieleza kuchoshwa na sera za vyama vya upinzani kwa madai kwamba vyama hivyo havina mwelekeo mzuri.

“Nimeamua kuhamia CCM baada ya kugundua kwamba vyama vya upinzani havina shukurani. Kuna mambo mazuri yamefanywa na Serikali ya CCM kama barabara za lami lakini wao bado wanabeza mafanikio hayo.

“Kwa hiyo nimeona ni bora nihamie CCM kwa chama ninachokiona kina mwelekeo na sera nzuri… nawaomba na wanachama wengine wa CHADEMA muondoke huko mje CCM chama kubwa”, alisema aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema wilaya hiyo ya Sengerema, Malima.

Kabla ya Malima kuhamia CCM kutoka Chadema, aliwahi kusimamishwa kwa barua ya Machi 16, 2011 yenya kumbu. Na. CDM/J/SENG/01/2011 iliyotumwa kwa Katibu wa Chadema mkoa wa Mwanza, kwa madai ya kusababisha mgogoro ndani ya chama hicho, lakini baadaye Baraza la Uongozi wa mkoa wa Chadema ulitengua uamzi wa kusimamishwa kasha kumrejesha kazini.

Awali mwenyekiti wa CCM wilaya ya Sengerema, Jaji Tasinga Gabanyaga, aliwapongeza viongozi hao wa upinzani kuhamia CCM, na kwamba hali hiyo inaonesha dhahiri kwamba sera za chama hicho tawala ni nzuri na ndiyo maana Watanzania bado wanakiamini chama hicho.

Kwa mujibu wa Tasinga, waliojiunga wasiwe na wasiwasi  na kwamba CCM haina makundi na kila kitu kinaendeshwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za chama, hivyo chama hicho tawala chini ya uenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kitashirikiana na wanachama hao wapya katika kujenga taifa lenye maendeleo makubwa.

Kwa  upande wake, Waziri wa Nishati na Madini, na mbunge wa jimbo la Sengerema, Ngeleja alisema: “Ujio wa wanachama hawa wapya ni furaha kubwa sana kwetu, na hali hii inaonesha wazi kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne inaleta maendeleo”.

Aidha, Waziri Ngeleja aliwaomba wananchi wote wa wilaya hiyo kujenga ushirikiano mzuri baina ya viongozi wa vyama na Serikali, ili kuwezesha upatikanaji wa maendeleo makubwa ya kisekta na si vinginevyo.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Sengerema

16 Comments
  • Huyo ndiye Ngeleja waziri wa madini na nishati. Ana posho ya Tshs 4,000,000 kwa siku; hakika kwa mwananchi wa kawaida kuiruka ni vigumu. Ninanalowaasa wananchi, fuateni matakwa ya moyo wenu wakati kuafaka utakapofika!

  • Kweni Ngereja aliyebomoa kambi ya CHADEMA ni Ngereja yupi? Mimi namfahamu huyu ambae alimtuma Jailo Kuomba Rushwa yupo mwingine? Kama ni huyu si aanze na kuondoa mgao wa umeme kwanza huko anakoenda siko!! Kama ni mwingine nifahamisheni. Vinginevyo huyu anapokea 4m kwa siku akiwa Dodoma ajisafuishe kwanza.

  • ni heri kuwa na mwerevu mmoja kuliko wasiowerevu 100 waende salama ndiko saizi yao. na kama wapo wengine waende mapema.

  • Watanzania tulio wengi njaa inasumbua hawo walio hama chama na kumfuata ngeleja na chama chao twawa jua kuwa ni nani na wameshindwa kwa kuwa CHADEMA nichama makini hivyo watu watatu au wa tano hawa wezi kukiua chama chenye rasilimali watu ushauli wangu kwa WATANZANIA WOTE TUWE MAKINI SANA NA WATANZANIA WENZETU WASIO NA MSIMAMO KISIASA NA KIJAMII

  • Inaonekana hao waliohama hawajui nini maana ya maendeleo, hivyo waaacheni wakaendeleze chama kilichobadirika na kuwa cha wezi watupu

  • Huyo Ngereja pamoja na serikali yake inabidi itueleze ni vipi anaruhusu madini kuchimbwa na kusafirishwa kusafishwa nje ya nchi?

  • waende zao, sisi chadema hatutaki mafisadi wa elimu, ardhi fedha za umma na ngono,kama ccm walivyokuwa mafisadi wa vitu hivyo hapo juu

  • Hawa Jamaa kujiondoa CDM ni sawa kwani inaonyesha ni Vibaraka vya Ngereja toka muda Mrefu.CDM haifugi Mamluki afadhali wamejingundua mapema maana upepo wa CDM ni mkali ungewashika tuu.
    CDM People power!!

  • sidhani kama wanajua wanachofanya, CCM ina wenyewe na ni chama cha walionacho,walalahoi ni kupiga kura thn wanasahaulika.

    Ngeleja tangu wamemchagua Sengerema ni mara ngapi amerudi kwao kama hii ndo mara yake ya kwanza?

    Sasa jamani ni Mbunge wa sengerema au wa Dar? Tena kama kuna mamluki wengine aende nao CDM haina mpango nao.

  • watanzania wengine sijui ndiyo kukua kifikra kwenyewe ama ni kitu gani? Hivi ngereja ana reputation gani ya kukaa mbele ya adhara na kuufanya watu wamsikilize na kucxhukua uamuzi wa kukimbia CHADEMA? kwa kipi hasa CCM wamefanya hivi karibuni cha kushurutisha watu kufanya uammuzi wa gafla namna hii@ kweli sikio la kufa hailiskii dawa!!!!!!

  • Mi sishangai kwa Watanzania kuhama CHADEMA kwenda CCM, ila ninachoshangaa ni kwa jinsi watanzania wanavyokuwa na kigeu geu. Ngeleja taarifa zake kuhusu sakala la Luhanjo na Jairo tumezipata, leo anakuwa na ujasiri wa kusimama mbele ya watanzania na kuwabembeleza. Mbaya zaidi Watanzania wanajirahisisha kwa hawa jamaa wasiokuwa na hata chembe ya huruma. Gharama za maisha zimepanda, bado tumesikia Tanesco wanapandisha bei za umeme, Rasilimali za nchi wanakula hawa jamaa, ufisadi n.k. Bado leo watanzania wanadanganyika kuhamia CCM!!!! Kwa lipi la maana wanalolifanya zaidi ya kutuharibia Nchi? WATANZANIA ZINDUKENI. TUTAWAACHIA WACHACHE WATUSAIDIE KUFIKIRI HADI LINI? WAJUKUU NA VITUKUU VYETU VITUSIFIE KWA LIPI LA MAANA TULILOLIFANYA? NI NII KUHAMA HAMA VYAMA?

  • Muandishi aliye andika story hiii, walio kimbia, na hata wale wenye Michango yenye Mrengo fulani kiufupi hizo njaaa zitawaua, Ushabiki Mandazi ni Mzigo.

    Muandishi mzima unakwenda kwenye tukio unakosa Angle of the story very Wonderful.

    Amesomea chuo gani. Kweli taaluma inadhalilishwa.!
    Nenda SAUT Ukasome huo ndi Ushauri wangu kwako Mwandishi.

  • wachape lapa na ngeleja ila siku ya kura waachane nayeb wachague CDM maana naona hawa jamaa hali zao ni mbaya sana.

  • CHADEMA wameishiwa, hawana sera zaidi ya VURUGU na MAANDAMANO!wanategemea nguvu ya umma kuliko sera na mwelekeo wa kimaendeleo

  • mwana mpotevu aliondoka kwa baba yake akaenda nchi za mbali akazunguka huko nahuku lakini aliporudi kwa baba baba alimpokea kwa shangwe kubwa miss peres karibu sana ccm we ni mwl wangu katu/seco.safi sana ngereja we ni jembe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *