Pamba: Dhahabu nyeupe iliyotelekezwa kwa kukosa pembejeo, huduma za ugani na masoko

Jamii Africa

“TUMEJIPANGA kurejesha heshima ya Kwimba katika kilimo na uzalishaji wa zao la pamba. Tumeanzisha kampeni ya kila familia kulima japo ekari moja ya zao la pamba.” Hiyo ni kauli ya Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mtemi Msafiri.

Mkuu huyo wa Wilaya alikuwa akijibu baadhi ya hoja na changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo cha pamba zilizoibuliwa na wakulima wilayani humo.

Kabla na miaka kadhaa baada ya Uhuru, Tanzania (wakati huo Tanganyika), ilikuwa miongoni mwa mataifa yaliyovuma kwa kilimo na uzalishaji wa mazao ya biashara.

Kwa wakati huo, usemi wa “Mkonge-Tanga” na “Pamba-Kwimba” ulitambulika kwa wengi, hasa wanafunzi kuanzia elimu ya msingi na sekondari kupitia masomo ya kilimo na wakati mwingine sehemu kidogo ya mada za somo la Jiografia.

Maeneo hayo mawili siyo tu yalivuma, bali pia yaliongoza kwa kilimo na uzalishaji wa mazao ya mkonge na pamba.

Hali ilianza kubadilika mwishoni mwa miaka ya 1970 baada ya Taifa kukumbwa na mtikisiko wa kiuchumi uliotokana pamoja na mambo mengine na vita vya kumng’oa Nduli Iddi Amin Dada wa Uganda maarufu kama Vita vya Kagera.

Katika mahojiano maalum yaliyofanyika ofisini kwake katika mji mdogo wa Ngudu yaliko Makao Makuu ya wilaya hiyo, Msafiri anaahidi kurejesha heshima ya Kwimba katika kilimo na uzalishaji wa pamba ndani ya kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, eneo linalofaa kwa ajili ya kilimo cha pamba ni jumla ya hekta 125, 332 ambazo zikilimwa kwa tija zinaweza kuzalisha zaidi ya tani 100, 000 za pamba kwa mwaka kulinganisha na tani 2, 016 zilizozalishwa msimu uliopita wa 2015/2016.

Awali, baadhi ya wakulima wa pamba kutoka Kata ya Ndugu walitaja sababu kadhaa zinazochangia wengi wao kuacha kulima zao hilo na kugeukia mazao mengine kama choroko, dengu, alizeti na mpunga.

 

Pembejeo, huduma ya ugani na elimu

Mkulima Mwezeshaji (Field Officer), katika Kijiji cha Kiliaboya, Kata ya Ngudu, Ngulimi John, anasema kilimo cha pamba kimeshuka kutokana na kukosa usimamizi ambao siyo tu umesabaisha wakulima kukosa elimu na pembejeo, bali hata viuatilifu vinavyosambazwa havina ubora unaostahili.

“Licha ya kutopatikana kwa bei rafiki kwa wakulima, baadhi ya viuatilifu/viuadudu vinavyosambazwa kwa wakulima havina uwezo wa kuuwa wadudu,” anasema Ngulimi na kuongeza:

“Hii ni kutokana na kukosekana kwa usimamizi makini kutoka kwa wataalam na viongozi wenye dhamana ya kulinda maslahi ya wakulima.”

Anasema changamoto ya mbegu yenye manyoya aina ya UK 91 (Ukiriguru 91), inayouzwa kwa Shs. 700 kwa kilo ni tija ndogo kutokana na kutoota licha ya kutumika nyingi (karibia kilo 10) kwa ekari moja ya shamba la pamba.

“Mbegu isiyo na manyoya aina ya UK M08 (Ukiriguru M08) inayouzwa kwa Sh2, 500 kwa kilo moja, yenyewe ina tija lakini upatikanaji wake ni wa shida kiasi kwamba wakulima hawaipati kulingana na mahitaji hata kama wanazo fedha za kununua,” anasema mkulima huyo.

Mkaguzi wa Pamba Wilaya ya Kwimba kutoka Bodi ya Pamba nchini (TCB), Penina Range, anasema kutokana ubora wa mbegu ya UK M08, TCB pamoja na wadau wengine wanafanya kila jitihada kuhakikisha mbegu hiyo inapatikana kwa ubora na kiwango halisi kinachohitajika.

Wakati mkulima atahitaji kilo 10 za mbegu yenye manyoya aina ya UK 91 kupanda ekari moja ya pamba, eneo hilo hilo hupandwa kwa kilo sita pekee za mbegu aina ya UK M08 isiyo na nyoya.

 

Maofisa Ugani:

Mkulima mwingine, Robert Cosmas, pia kutoka Kijiji cha Kaliaboya anasema kwa muda wa zaidi ya miaka 10 aliyoshiriki kilimo cha pamba, hajawahi kutembelewa wala kupata huduma ya maofisa ugani.

“Hawafiki kijijini kutembelea wakulima. Kutokana na kukosa elimu na ushauri wa kitaalam, baadhi ya wakulima hutumia dawa ya kundi moja katika minyunyizo ya hatua tatu za kupuliza dawa shambani,” anasema Cosmas.

Anasema hali hiyo inatokana na wakulima kubabaishwa na lugha, majina ya kibiashara na kitaalam ya madawa.

Kitaalam, pamba hunyunyuziwa dawa kuanzia hatua ya kutoa vibahasha, wakati wa kufunga vitumba na hatua ya vitumba kupasuka.

Katika vipindi hivyo, mkulima anapaswa kunyunyiza dawa kulingana na aina ya wadudu na magonjwa yanayoshambulia pamba.

Kuna aina nyingine ya dawa inayotakiwa kupulizwa wakati wowote wadudu wanapoonekana shambani.

Kutokana na kukosa elimu stahiki, baadhi ya wakulima hujikuta wakipuliza dawa bila kuzingatia mahitaji, aina sahihi na muda. Hali ambayo siyo tu hupunguza tija, bali pia huwatia hasara na kuwakatisha tamaa kuendelea na kilimo.

 

Uzalishaji kushuka hadi kilo 300 kwa ekari

Kutokana na changamoto kadhaa, kuanzia maandalizi ya shamba, ubora wa mbegu na viuadudu, wakulima kukosa elimu na huduma kutoka kwa Maofisa Ugani, uzalishaji wa pamba umeshuka kutoka wastani wa kilo 800 hadi 1, 200 kwa ekari moja hadi kufikia kati ya kilo 300 hadi 600.

“Hii inakatisha tamaa wakulima ukizingatia pia na changamoto ya bei inayoshuka na kupanda kulingana na soko duni linalotegemea kuimarika au kuyumba kwa thamani ya shilingi,” anasema Mkulima Mwezeshaji Ngulimi.

“Shamba lililolimwa kwa muda muafaka, likapandwa mbegu sahihi na kunyunyiziwa dawa kulingana na mahitaji linaweza kuzalisha kati ya kilo 800 hadi 1, 2000 kwa ekari moja,” anasema Ofisa Ugani wa Kata ya Malya, Hamisi H. Mzee.

Kiwango hicho kitamhakikishia mkulima pato la kati ya Shs. 800, 000 hadi Shs. 1.2 milioni kwa ekari tofauti na kipato cha sasa cha kati ya Shs. 300, 000 hadi Shs. 600, 000, kwa bei ya Shs. 1, 000 kwa kilo ya pamba.

Makala haya yataendelea……

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *