Ni wakati sahihi kwa wakulima kutumia teknolojia ya uhandisi jeni, mbegu za GMO?

Jamii Africa

Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yameathiri shughuli za kilimo ambazo zinategemea mvua msimu.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya wasomi nchini wanapendekeza  matumizi ya teknolojia ya uhandisi jeni ambayo inatumika kutengeneza mbegu za GMO (Generically Modified Organisms) ambazo zinatajwa kuhimili ukame na wadudu waharibifu. Pia zinazaliana sana kuliko mbegu za asili na kuongeza uzalishaji kwa wakulima

Lakini baadhi ya wataalamu wa mazingira na afya ya binadamu wamezikataa mbegu hizo na kudai kuwa zinaathiri afya ya binadamu, ukuaji wa akili ya watoto ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira.

Kutokana na mkanganyiko uliopo juu ya Mbegu za GMO katika jamii, serikali haijaridhia matumizi ya teknolojia ya uhandisi jeni kwa wakulima na kulichukulia suala hilo kwa tahadhari kubwa kabla ya kuruhusu kuingia nchini.

Majaribio ya mbegu za GMO yaliingia Tanzania mwaka 2008 chini ya mradi wa Water efficient Maize for Africa (WEMA) uliofadhiliwa na taasisi ya Bill&Merinda Gates ya nchini Marekani lakini ulianza mwaka 2016 kwasababu ya vikwazo vya sheria zinazosimamia  usalama wa mali asili.

Kulingana na sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 kifungu cha 69-(1) – (3) iliweka kanuni ambazo zinazouia uingizaji wa vifaa vya kutengeneza mbegu hizo kwa ajili ya utafiti ambapo mtu yeyote atakayeingiza mbegu za GMO atawajibika kwa madhara yatakayotokea kwa afya za watu na mazingira.

Licha ya sheria kuzuia uingizaji wa mbegu za GMO, bado inatoa mamlaka kwa Waziri husika kutoa kibali maalum cha kuagiza mbegu hizo ikiwa zitatumika kwa ajili ya utafiti na majaribio ya kisayansi.

Kituo cha utafiti wa kilimo cha Makutupora kwa kushirikiana na mradi wa WEMA baada ya kupata ridhaa ya serikali wameanza kufanya utafiti juu ya mbegu hizo kubaini kama wakulima wa Tanzania wako tayari kutumia teknolojia ya uhandisi jeni au waendelee kutumia mbegu za kienyeji katika kilimo ambacho kinakabiliwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Akiwasilisha mada katika mkutano wa Kavazi la kwanza la Mwalimu Nyerere (2018) kuhusu utafiti wa awali wa GMO, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaamu, Richard Mbunda amesema bado kuna taarifa ambazo zinapishana katika kiwango ambacho mbegu za GMO zinazostahimili ukame ambazo zimefanyiwa majaribio kwenye Kituo cha utafiti wa kilimo  cha Makutupora kilichopo Dodoma katika uwezo wake wa kupunguza hasara kwa mkulima.

Mbunda amesema mashaka  wanayoyaona baadhi ya watu ni kuhusu usalama wa vyakula vinavyotokana na mbegu za GMO kwa afya na mazingira, mambo ambayo ni lazima watafiti wayaangalie na kujiridhisha kabla ya kuzipeleka mbegu hizo kwenye mamlaka za serikali zinazopitisha mbegu zote nchini.

Wasiwasi mwingine ni namna mkulima mdogo atakavyoweza kunufaika na teknolojia hiyo ikiwemo upatikanaji wa mbegu hizo kwa bei nafuu.  

 Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mkutano huo Dkt. Ng’wanza Kamata ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, amesema, “Wananchi wote wakielewa vizuri jambo hili litasaidia kuondoa mashaka juu ya usalama wa teknolojia ambao umekuwa ukitolewa na watu mbalimbali na mashaka hayo yakiondoka ndipo sasa kila mtu anaweza kuwa huru kuchagua kuitumia teknolojia hiyo au la kwa manufaa yake na manufaa ya taifa kwa ujumla”.

 

Umuhimu wa Mbegu za GMO

 Mtafiti mstaaafu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ((COSTECH), Dkt. Nicholous Nyange  amesema ni wakati mwafaka kwa wakulima wa Tanzania kutumia mbegu za GMO ili kuongeza uzalishaji na kupata soko la uhakika ndani na nje ya nchi. 

 “Inakadiriwa kuwa Tanzania kwa sasa ina watu wapatao milioni 55 na idadi hii inaongezeka kila siku na kama sayansi haitatumika kusaidia kuzalisha chakula cha kutosha basi huenda taifa likasumbuliwa na njaa kila mwaka kwenye maeneo mengi”, amesema Dkt. Nyange.

Amebainisha kuwa pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na wakulima kulima lakini bado hawajaweza kuzalisha chakula cha kutosha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wadudu, magonjwa na ukame unaosababishwa na  mabadiliko ya tabia nchi.

Takwimu za kilimo zinaonesha kuwa Tanzania kwenye uzalishaji wa mahindi unakadiriwa kufikia tani 1.5 hadi tani 2 pale ambapo hali ya hewa na mtawanyiko wa mvua utakuwa mzuri lakini kwa nchi zilizoendelea kama vile Marekani wanazalisha tani 8 hadi 9 kwa ekari moja kutokana na kutumia teknolojia za kisasa.

Mtaalamu huyo wa masuala ya kilimo anaeleza zaidi kuwa ikiwa wakulima watatumia teknolojia ya kisasa ikiwemo ya uhandisi jeni, sekta hiyo itaweza kuchangia vyema kwenye pato la taifa na kuwanufaisha wakulima.   

“Eneo linalofaa kwa kilimo na makazi likigawanywa kwa idadi ya watu waliopo nchini katika kipindi kifupi kijacho halitatosha kupata maeneo ya kutosha kwaajili ya kilimo, makazi na shughuli zingine za kibinadamu hivyo njia pekee ni kuwawezesha wakulima kutumia mbinu za kisasa (GMO) kuzalisha kwa wingi kwenye maeneo madogo ili kuendana na ongezeko la idadi ya watu na eneo la nchi lililopo”, ameshauri Dkt. Nyange.

Naye aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Goodluck Ole Medeye amesema kuwa hakuna namna ambayo Tanzania itakwepa kutumia mbegu hizo au bidhaa za GMO kwa kuwa Tanzania sio kisiwa kwasababu nchi nyingine duniani zinafanya tafiti juu ya mbegu hizo.

 “Tanzania itajikuta wananchi wake wanatumia mbegu hizo kwani kwa sasa nguo nyingi tunazovaa zinatoka nchi zinazozalisha pamba ya GMO na baadhi ya vyakula  tunavyokula kutoka nje vinatokana na mbegu za GMO”, amesema Dkt. Ole Medeye.

            Mtaalamu wa maabala akifanya majaribio ya mbegu

 

Angalizo…

Mtafiti wa zao la mahindi, Dkt. Aloyce Kulaya  amesema kuwa suala la GMO linaangaliwa tu kwenye vyakula lakini teknolojia hiyo inatumika zaidi kwenye kutengeneza dawa za kutibu magonjwa mbalimbali na sio mbegu za mazao.

Ametoa angalizo kuwa teknolojia ya uhandisi jeni sio njia pekee ya kupata ufumbuzi wa matatizo ya wakulima lakini pale mbinu za kawaida zinaposhindwa, teknolojia hiyo  hutumika  kupata ufumbuzi wa haraka na sahihi wa changamoto za magonjwa,ukame na wadudu ambazo zinawasumbua wakulima.

Naye mwakilishi wa Bodi ya Nyama Tanzania, Alfred Mmbaga amewataka watafiti wa GMO kuweka wazi athari za kiafya zinazotokana na mbegu hizo ili wakulima wafanye maamuzi sahihi, kwasababu kumekuwa na malalamiko ya watu kupata maradhi mbalimbali wanapotumia bidhaa zinazotokana na mazo ya GMO. Ameongeza kuwa ni muhimu pia kutafakari suala la ladha ambalo pia ni changamoto kwenye bidhaa hizo.

Akichangia katika mada hiyo, Mtaalamu wa kujitegemea wa Mazingira na Uvuvi, Dkt. Modesta Medard amesema mjadala wa teknolojia ya uhandisi jeni haina umuhimu kwa taifa kwasababu sio rafiki kwa mazingira na viumbe hai.

Amebainisha kuwa nchi nyingi zilizoendelea zimeachana na teknolojia hiyo kutokana na athari zilizogundulika kwenye mazingira na afya ya binadamu. Amewataka watafiti kuvumbua njia mbadala za kuwasaidia wakulima kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kuliko kuwaletea teknolojia ambayo tayari imeonyesha matokeo hasi duniani.

Hata hivyo, wakati Afrika Kusini imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika kupokea na kutumia mbegu za GMO, nchi zilizoendelea  duniani tayari zimezuia matumizi ya aina hii ya mbegu ikiwemo Canada, Argentina, Australia, India na Mexico na msimamo wa EU Ukiwa "Zuia GMO".

                                  Baadhi ya waandamanaji wakiwa wamebeba mabango kupinga GMO isiruhusiwe Afrika

 

GMO ni nini?

 GMO ni aina ya mbegu na mimea ambayo imebadilishwa vinasaba (genes) katika maabara ili kuboresha aina fulani ya tabia inayohitajika, kwa mfano kuongeza virutubisho, na kuongeza uwezo wa kujikinga na madawa. Pia inazalisha mimea inayostahimili ukame.

 Athari zake ni pamoja na kuharibu mfumo wa ikolojia, kuharibu ama kubadilisha kabisa virutubisho katika mimea, kansa, kuharibu rutuba ya ardhi na kusababisha wakulima kua tegemezi wa madawa ya kilimo, kujitokeza kwa magugu ambayo yanajikinga na madawa ya kuua magugu, na hasara kwa wakulima kutokana na ununuzi wa kiasi kikubwa cha madawa.

Marekani ndio inaongoza kwa utengenezaji wa aina hii ya mbegu zikizambazwa na makampuni kama Monsanto, Syngenta AG, na DOW Chemicals ambazo nyingi tumekua tukiziona hapa nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *