Polisi kuwakamata wabunge wa CDM waliokatwa mapanga

Jamii Africa

JESHI la Polisi Mkoani Mwanza, limeanza kuonekana kutaka ‘kuwageuzia kibao’ wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoani Mwanza, waliovamiwa na kukatwa mapanga na watu wanaodaiwa ni wafuasi wa CCM, kwani polisi wanatarajia kuwakamata wabunge hao kuhusiana na tukio la kukatwa kwao mapanga usiku wa kuamkia Jumapili ya Aprili mosi, 2012.

Wabunge waliojeruhiwa, Kiwia na Machemli

Siku hiyo, ilikua ni siku ya upigaji kura katika kata ya Kirumba mkoani Mwanza, ambako wabunge hao Highness Kiwia wa jimbo la Ilemela na Salvatori Machemli ambaye ni mbunge wa jimbo la Ukerewe walikuwa miongoni mwa viongozi waandamizi walioshiriki kampeni na mikakati ya chama hicho katika uchaguzi wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wao, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.

Mgombea wa Chadema Dany Kahungu ameibuka na ushindi katika uchaguzi huo wa Udiwanai kata ya Kirumba.

Polisi imesema, inaweza kuwakamata wabunge hao, wakiwa bado wamelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ya jijini Dar es Salaam wanakopatiwa matibabu, au inaweza kuwasubiri watoke hospitalini kisha iwakamate, huku wabunge hao wakiwashutumu polisi kuhusika na uvamizi huo kutokana na kushindwa kuchukua hatua kwa wahusika wanofahamika.

Mbunge Kiwia akiwa amejeruhiwa mgongonio

Mkuu wa Upelelezi wa  Jinai (CID) wa Jeshi la polisi Mkoani Mwanza (RCO), Deusdedith Nsimeki, amesema, inabidi  wabunge hao wahojiwe kwani ndiyo wanaweza kuwa chanzo na watuhumiwa wa kwanza katika ghasia hizo zilizotokea usiku wa kuamkia Aprili Mosi mwaka huu katika eneo la Ibanda Kabuholo, Kirumba jijini Mwanza.

“Hawa wabunge lazima tuwakamate watueleze vizuri kuhusiana na tukio la kukatwa kwao mapanga usiku. Watueleze kwa nini walienda huko Kabuholo gizani usiku tena bila kutoa taarifa polisi?.

“Kukatwa kwao mapanga isiwe sababu ya kutokamatwa na polisi, lazima tuwakamate tuwahoji. Inawezekana wabunge hawa ndiyo chanzo kikubwa katika kesi hii.

“Tunaweza kuwakamata wakiwa wamelazwa hospitalini huko huko, au tukaamua kuwasubiri watoke hospitalini halafu tuwakamate!. Sheria zinaturuhusu sisi kumsomea mashtaka mtu yeyote hata kama kalala kitandani”, alisema RCO Nsimeki ambapo alitania kwa kusema: “Unajua mtu anaweza kukutwa na mke wa mtu akakatwa mapanga na kichwa kikaning’inia, sasa utasema huyo mtu si chanzo?”.

Hata hivyo, mwandishi wa habari hizi alipomuuliza RCO Nsimeki iwapo kuna watu wamekamatwa na polisi kuhusiana na tukio hilo la wabunge kukatwa mapanga na kuumizwa sehemu mbali mbali za miili yao alisema, hakuna mtu hata mmoja aliyekamatwa hadi kufikia jana jioni.

“Hatujakamata mtu yeyote kuhusiana na tukio hili. Lakini tulishaanza kazi yetu ya upelelezi na tutawakamata tu hilo halina tatizo”, alisema Mkuu huyo wa Kitengo cha Upelelezi Makosa ya Jinai Mkoani Mwanza.

Kitendo cha jeshi la polisi mkoani Mwanza kushindwa kuwakamata watuhumiwa wa tukio hilo, inaweza kuwashangaza watu wengi, ikizingatiwa na uzito wa tukio lenyewe.

Majeraha zaidi katika kichwa cha Mbunge Kiwia

Aprili Mosi mwaka huu, usiku wa kuamkia upigaji wa kura katika uchaguzi mdogo wa Kata ya Kirumba, wabunge hao walitekwa na kundi la watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM, wakati wabunge hao na makada wengine wa Chadema wakidaiwa walikuwa wakiwasambaza mawakala wa chama chao kurudi majumbani kwa ajili ya kujiandaa kwenda kusimamia kura za mgombea wa Chadema Kata ya Kirumba, Dany Kahungu katika uchaguzi huo mdogo.

Katika tukio hilo, Mbunge wa Ilemela, Kiwia ndiye aliyeumizwa zaidi kutokana na kupata majeraha makubwa sehemu mbali mbali za mwili wake ikiwemo sehemu ya kichwani na mgongoni, ambapo alilazimika kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC), ya jijini Mwanza kwa matibabu zaidi, huku Machemli akikimbizwa Sekou Toure.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow (RPC), aliwathibitishia waandishi wa habari juzi na kusema kwamba: “Ni kweli wabunge hao wamevamiwa na kujeruhiwa kwa mapanga usiku, na sisi tulipokea taarifa kuwa wafuasi wa CCM wamewateka na kuwaweka chini ya ulinzi wabunge watatu wa Chadema, Kiwia, Wenje na Machemli”.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo, muda mfupi polisi walifanikiwa kufika eneo la tukio na kuwakuta wabunge hao ambao wakiwa wamewekwa chini ya ulinzi na wafuasi hao wa CCM, ambapo polisi walipambana na kufanikiwa kuwaokoa.

Kamanda Barlow aliwataja majeruhi wengine watatu waliokimbizwa katika hospitali ya mkoa ya Sekou Toure na kulazwa kuwa ni pamoja na Haji Mkwenda (21), ambaye amevunjika mguu wa kulia, Judith Madaru (26), ambaye amechomwa kisu sehemu ya ziwa upande wa kushoto na Ivori Festo Machimba (26), ambaye amejeruhiwa kichwani na mdomoni.

Alitaja namba za magari yaliyokutwa kwenye eneo la tukio kuwa ni pamoja na T 377 ARF linalomilikiwa na mbunge Kiwia, T 729 DAD linalomilikiwa na Mohamed Juma pamoja na T 397 ANU aina ya Land Cruiser ambalo mmiliki wake hakupatikana.

Wabunge hao wamehamishiwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi, ambako hali zao zinaelezwa kuendelea vyema, huku wote wawili wakishangazwa na kitendo cha polisi kushindwa kuwakamata watuhumiwa.

Katika maelezo yake mtandaoni, Zitto Kabwe alisema mmoja wa majeruhi ni kiongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ambaye upo uwezekano wa kuwa alipigwa na wenzake katika vurugu hizo, na aliwaomba polisi kutomruhusu kutoka hospitalini.
“Kuna mmoja wa majeruhi ambaye yupo hapa mwanzoni alisema yeye ni mtu wetu na ameumizwa pia. Imegundulika ni mtu wa UVCCM, Ahmed Mkilindi ambaye ndiye alikuwa anaongoza kikosi kilichowavamia kina Kiwia. Amepata jeraha mkononi (friendly fire?). Mwenyekiti wa CCM mkoa yupo hapa kaja kumwona. Nimewaambia Polisi mtu huyu asitolewe hospitali kinyemela bali atoe maelezo polisi kwanza. Huyu ni mtuhumiwa wa kwanza kabisa. Hali ya Kiwia sio nzuri sana. Anatakiwa kufanyiwa ct scan kuona athari aliyopata (maana kapigwa na shoka na mapanga kichwani). Bahati mbaya hapa Bugando kifaa hicho hakifanyi kazi,” alisema Zitto kabla ya wabunge hao kuhamishiwa Dar es Salaam.

Zitto aliendelea kwa kusema, “Siasa za Tanzania zinazidi kujidhihirisha kuwa hazina tofauti na nchi nyingine za Kiafrika. Chama cha siasa kuwa na makundi ya wahuni na kupiga watu ni hatari na chama hicho kinakosa ‘moral’ authority ya kutawala. Tusubiri uchunguzi zaidi wa Polisi. I am so depressed.”

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza na waandishi wa FikraPevu Dar es Salaam

7 Comments
  • ni kweli ni habari ya kusikitisha na ni doa kwa wapenda amani popote, niungane na wapenda amani nikishauri tutumie kila aina ya fursa alizotupa mwenyezi mungu kuwa na subbra yanapojitokeza maswala kama haya nina amini tutapunguza madhara kwa wajamii nzima ukizingatia kuwa kila mmoja anaupeo wake wa kutafsiri tukio lenyewe. tuvipe nafasi vyombo husika vifanye kazi, tuviamini, na vyenyewe vijiamini kwamba vinadhamana,uwezo na mamlaka ya kufanya yaliyomatarajio ya wananchi, hakuna sababu ya kutafuta majibu yetu wenyewe tena ya harakaharaka. mwisho niwape pole wale wote waliopatwa na mkasa huo, inshallah mwenyezi mungu awajalie kupona haraka. mpenda amani ya kweli.

  • ni kweli ni habari ya kusikitisha na ni doa kwa wapenda amani popote, niungane na wapenda amani nikishauri tutumie kila aina ya fursa alizotupa mwenyezi mungu kuwa na subbra yanapojitokeza maswala kama haya nina amini tutapunguza madhara kwa wajamii nzima ukizingatia kuwa kila mmoja anaupeo wake wa kutafsiri tukio lenyewe. tuvipe nafasi vyombo husika vifanye kazi, tuviamini, na vyenyewe vijiamini kwamba vinadhamana,uwezo na mamlaka ya kufanya yaliyomatarajio ya wananchi, hakuna sababu ya kutafuta majibu yetu wenyewe tena. mwisho niwape pole wale wote waliopatwa na mkasa huo, inshallah mwenyezi Mungu awajalie kupona haraka. Mpenda amani ya kweli…Yaupanga Kataya

  • ni kweli ni habari ya kusikitisha na ni doa kwa wapenda amani popote, niungane na wapenda amani nikishauri tutumie kila aina ya fursa alizotupa mwenyezi mungu kuwa na subbra yanapojitokeza maswala kama haya nina amini tutapunguza madhara kwa wajamii nzima ukizingatia kuwa kila mmoja anaupeo wake wa kutafsiri tukio lenyewe. tuvipe nafasi vyombo husika vifanye kazi, tuviamini, na vyenyewe vijiamini kwamba vinadhamana,uwezo na mamlaka ya kufanya yaliyomatarajio ya wananchi, hakuna sababu ya kutafuta majibu yetu wenyewe. mwisho niwape pole wale wote waliopatwa na mkasa huo, inshallah mwenyezi Mungu awajalie kupona haraka. Mpenda amani ya kweli…Yaupanga Kataya

  • jamani Mungu tusaidie waja wako Tunatafuta Amani lakini weingine wanaipoteza kwanini lakini Amani iko wapi Tanzania
    Mungu atawalipa watu waliofanya kitendo hicho cha unyama namna hii Malipo ni hapa hapa na siku ya kihama sijui watajibu nin

  • suara la wabunge wa chadema kukatwa mapanga inadhihilisha kwamba siasa za Tanzania zinakosa mwelekeo na inaonyesha hakuna demokrasia ya kweli na hazina malengo mazuri juu ya maendeleo ya nchi yetu. Kiongozi mwenye nia na maendeleo anaposhindwa katika uchaguzi inabidi atambue ya kuwa bado wananchi hawakubaliani na sera zake au hawana imani nae suara nla kujihusisha na vikundi vya wahuni kwa ajili ya kulipiza visasi inaonyesha hakuwa na lengo la kuongoza bali alikuwa akitafuta uongozi kwa manufaa binafsi.

  • Aisee poleni sana Wabunge wa CHADEMA aisee inaonekana mlishughulikiwa sana. Police wakamateni wahusika jamani tunashindwa kuamimi huu uhuni

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *