Polisi Maziwa Makuu kudhibiti ujambazi wa silaha za kivita

Jamii Africa

MAKAMANDA wa Jeshi la Polisi katika Mikoa minane ya Maziwa Makuu, wamekubaliana kwa pamoja kuhakikisha kila mmoja wao anapambana kikamilifu na tatizo la uhalifu wa kutumia silaha za moto katika eneo lake la utawala, na kutoa onyo kali la kuhakikisha kwamba majambazi watakaoingia kwenye mikoa hiyo hawatoki.

Aidha, wamethibitisha kwamba, maeneo ya Maziwa Makuu yamekuwa kichochoro cha kuingiza na kusafirisha silaha za kivita kutoka nchi jirani, pamojana dawa za kulevya, ambapo zaidi ya silaha 60 aina ya Sub Machine Gun (SMG), RPG, AK47, Rifle na mabomu ya kutupa kwa mkono zilikamatwa maeneo mbali mbali ya mikoa hiyo ya Maziwa Makuu.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Saidi Mwema

Makubaliano hayo ya pamoja, yametolewa leo Jijini Mwanza na Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi ( ACP), Liberatus Barlow, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi, kuhusiana na mkutano wa kupanga mikakati ya kupambana na uhalifu wa kutumia silaha, uliowashirikisha Makamanda wa polisi wa mikoa hiyo ya Maziwa Makuu.

Alisema mkutano huo wamejipanga kupeana taarifa zitakazzosaidia kubadilishana uzoefu na taarifa za Kiitelejensia, ili kuona ukubwa wa kazi na kuweka mikakati ya kupambana na uhalifu katika mikoa hiyo ya Maziwa Makuu ambayo ni Mwanza, Kagera, Kigoma, Mara, Tabora, Shinyanga, Rukwa na Tarime Rorya.

“Tumekubaliana kwa pamoja kuhakikisha wananchi wa maeneo yetu wanakuwa salama. Jambazi atakayeingia hatatoka!. Lazima tuweke mikakati kabambe kama hii maana tumebaini ukanda huu wa Maziwa Makuu umekuwa kama njia ya kuingizia na kusafirishia silaha na dawa mbaya za kulevya”, alisema RPC Barlow.

Alisema makubaliano hayo yakitekelezwa vema katika kupambana na kuzuia uhalifu, maeneo mengine ya nchi yatakuwa salama zaidi kwani uingizwaji wa silaha na dawa za kulevya nchini umekuwa ukitishia amani na usalama wa Watanzania.

Kamanda Barlow alisema, Ziwa Victoria kwa upande wa Mwanza ambalo lina visiwa 75 vidogo vidogo ukiondoa Ukerewe, lina eneo kubwa ambalo linaweza kutumika kusafirisha silaha, utekaji wa wavuvi na uvuvi haramu, ambapo upande wa mkoa wa Mara kuna visiwa nane, hivyo kufanya kazi katika mazingira hayo ni vigumu bila kuwa na mikakati ya pamoja na madhubuti.

Akikazia hilo RPC Barlow alisema: “Tanzania kwa Maziwa Makuu inapakana na nchi za Rwanda, Burundi, DRC Congo, Uganda na Kenya, lakini pia Somalia ambao wako jirani. Kwa maana hiyo nchi hizi zinatishia hali ya usalama wa wananchi wetu, kutokana na kukumbwa na migogoro na machafuko ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

“Lazima tukae pamoja ili kila mtu atoe taarifa zitakazosaidia kuweka na kupanga mikakati ya kupambana na kutokomeza kabisa kama si kupunguza wimbi hatari la uhalifu!. Lazima tuwe na vissio (malengo), ya kuboresha usalama wa wananchi wetu wanaotutegemea”.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Selewi, alisema silaha nyingi zinatoka maeneo ya Maziwa ukiondoa ziwa Nyasa ambalo halimo kwenye mkakakati huo.

Alisema pamoja na kuwepo kwa mafanikio katika amaeneo ya Maziwa Makuu, lakini bado kuna changamoto ya uhalifu wa unyang’anyi wa kutumia silaha, kwa sababu ya kupakana na kuzungukwa na watu ambao maeneo yao si salama.

Habari hii imeandaliwa na Sitta Tumma – Mwanza

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *