Ripoti ya FikraPevu ‘yapeleka’ mwalimu mwingine kunusuru kufungwa shule Nyasa

Jamii Africa

SAA chache baada ya gazeti tando la FikraPevu kuripoti kuhusu shule yenye wanafunzi 195 kufundishwa na mwalimu mmoja, tayari Serikali imetuma mwalimu mwingine.

Kuwasili kwa Mwalimu Charioni Mpombo kutoka Shule ya Msingi Tingi, katika Kata ya Tingi wilayani Nyasa kutainusuru shule ya Matarawe sifungwe kila wakati mwalimu pekee aliyepo anaposafiri ama kuugua.

Alhamisi, Januari 26, 2017 saa 1:00 asubuhi, FikraPevu iliripoti kwamba Shule ya Msingi Matarawe katika Kijiji cha Marungu, Tarafa ya Mpepo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, ilikuwa imefungwa kwa wiki mbili zaidi tangu kufunguliwa kutokana na mwalimu pekee aliyekuwepo, Gaudence Msuha (48), kuwa mafunzoni mjini Songea.

“Nimeletewa mwalimu mmoja wa kiume,” alisema kwa furaha Mwalimu Msuha ambaye hulazimika kufundisha vipindi takriban kumi kwa siku. "Bado nahitaji walimu, lakini angalau nimepata msaidizi na watoto wanaweza kuendelea na masomo hata ninaposafiri."

FikraPevu inazo taarifa kwamba, mara baada ya taarisha hiyo kuchapishwa, kulikuwa na mawasiliano mfululizo kutoka wizarani na halmashauri ya wilaya ya Nyasa ambapo inaelezwa kwamba Mwalimu Mpombo alipewa taarifa ya ghafla na kulazimika kuondoka wakati huo huo bila hata kujiandaa ili tu akaripoti kabla ya kuanza kazi rasmi.

Katika taarifa yake ya awali, FikraPevu ilieleza kwamba, Mwalimu Msuha anafundisha peke yake idadi hiyo ya wanafunzi ambao wako darasa la awali, la kwanza na la pili na mbali ya kulemewa na mzigo wa masomo, lakini kila anapopata dharura hulazimika kufunga shule.

Tangu Januari 10 hadi 18, 2017, Mwalimu Msuha alikuwa akihudhuria mafunzo ya siku nane mjini Songea ya kujengewa uwezo masomo ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) yaliyotolewa kwa walimu wote wa awali kutoka wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma.

Hali hiyo inaelezwa kukwamisha hata zoezi la uandikishwaji wa watoto wa darasa la awali na la kwanza, kwani mara nyingi wazazi wengi huwapeleka watoto wao mara shule zinapofunguliwa.

“Baada ya kurejea ndiyo wanafunzi wanaendelea kujiandikisha katika darasa la awali na msingi, wazazi walikuja na kukuta shule imefungwa,” anasema na kuongeza kwamba mpaka sasa waliojiandikisha chekechea ni 40, wa darasa la kwanza wapo 60 na walioko darasa la pili ni 95.

Hiyo haikuwa mara ya kwanza kufungwa kwa muda kwa shule hiyo yenye darasa la awali, la kwanza na la pili tangu ilipoanzishwa mwaka 2016.

“Niko peke yangu shule nzima, mimi ndiye mwalimu mkuu, mwalimu wa taaluma, mwalimu wa miradi na kadhalika, sasa inapotokea natakiwa kuhudhuria vikao hata kwa Mratibu Elimu Kata, inanilazimu nifunge,” anasema Mwalimu Msuha (48) wakati alipozungumza na FikraPevu kwa njia ya simu.

Anasema hali hiyo inawanyima fursa watoto kujifunza, lakini haizuiliki kutokana na uhaba wa walimu uliopo hata katika halmashauri ya wilaya hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Mwalimu Msuha akasema amekuwa akifundisha vipindi 10 kwa siku katika madarasa yote matatu, ukiwa ni wastani wa vipindi 50 kwa wiki.

“Masomo makuu ya darasa la kwanza na la pili ni Kusoma, Kuandika na Kuhesabu, lakini kuna masomo mengine matatu ya ziada wakati darasa la awali wana masomo mawili, nashukuru tu kwamba darasa la kwanza na awali wanaingia asubuhi na wale wa la pili wanakuja mchana, vinginevyo hali ni ngumu mno,” anasema.

Mwalimu Msuha ameiambia FikraPevu kwamba, hata shule mama ya Marungu yenye takriban wanafunzi 400 kuanzia darasa la awali hadi la saba, nayo ina walimu wanne tu.

Matarawe ni shule iliyoanzishwa mwaka 2016 ili kupunguza wingi wa wanafunzi katika shule ya Marungu, ambapo imejengwa kwa nguvu za wananchi.

Mpaka sasa, kwa mujibu wa Mwalimu Msuha, kuna vyumba viwili na ofisi vilivyokamilika wakati ujenzi unaendelea katika vyumba vingine viwili.

Mwalimu huyo anasema kwamba, Shule ya Marungu imebaki na walimu wanne badala ya sita kutokana na yeye kwenda kuanzisha shule hiyo ya Matarawe wakati mwalimu mwingine, Salome Moyo amestaafu mwaka 2016.

“Pale sasa wamebaki Mwalimu Mkuu Alex Komba, Bi. Gema Nduguru ambaye ni msaidizi, James Lowini wa taaluma na Zakayo Komba,” anasema Mwalimu Msuha, ambaye yeye ana cheti cha Daraja la IIIA.

Mkoa wa Ruvuma unakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi wa umma ambao wanakadiriwa kufikia 7,747 huku sekta ya elimu ikiongoza kwa upungufu wa walimu 3,456 ikifuatiwa na sekta ya Afya ikiwa na upungufu wa watumishi 2,472.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, Mkoa wa Ruvuma wenye shule za umma 732 na za binafsi 10 (kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2012), una jumla ya walimu 6,103 tu, kati yao wanaume ni 3,344 na wanawake 2,759.

Aidha, Wilaya ya Mbinga, ambayo iligawanywa mwaka 2013 na kuzaliwa Wilaya ya Nyasa, ilikuwa na walimu 2,117 tu, kati yao wanaume 1,185 na wanawake 932.

Hata hivyo, Wilaya ya Nyasa ina walimu 737 tu katika shule 106 za msingi zenye jumla ya wanafunzi 35,381.

Jitihada za kumpata Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Oscar Mbiuzi, ili kuelezea changamoto za elimu, ikiwemo ya shule ya msingi Matarawe, hazikuzaa matunda baada ya simu yake kutokuwa hewani.

Uhaba wa walimu katika shule hiyo na nchini Tanzania kwa ujumla unaonekana kuwa changamoto katika utekelezaji wa Lengo Namba Nne la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDG) linalosisitiza elimu bora.

2 Comments
  • Asanteni sana FikraPevu.

    Sisi wazazi tusio na uwezo wa kuwapeleka ndugu zetu wa huko vijijini kwenye shule za mbali zenye walimu, Matarawe ni msaada kwetu. Hivyo kukosekana kwa walimu ilikuwa changamoto kubwa.

    Pamoja na kwamba bado changamoto haijaisha lakini walau serikali imeanza kuchukua hatua tena kwa haraka

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *