Ripoti:Vinara wa Rushwa? Watumishi na Wanasiasa

Jamii Africa

Ripoti ya Tathmini ya Rushwa nchini ambayo ilikuwa imecheleweshwa kuwekwa hadharani  kwa miaka miwili na TAKUKURU hadi Rais Kikwete alipoagiza iwekwe hadharani wiki iliyopita inaonesha kuwa wananchi wengi wa Tanzania wanaona kuwa wanasiasa na watendaji mbalimbali nchini ndio vinara wa rushwa.

Akiandika katika utangulizi wa ripoti hiyo Rais Kikwete amekiri kuwa watendaji wa serikali yake wanaonekana na wananchi kuwa ndio vyanzo vya rushwa kutokana na uroho wao. “Rushwa imeenea sana na ni kikwazo kikubwa cha juhudi za maendeleo; chanzo kikuu cha rushwa ni tamaa ya watumishi wa umma na wafanyabiashara” amesema Rais Kikwete.

Hukumu hii ya wananchi dhidi ya serikali na watendaji wake imekuja kuthibitisha kile ambacho tayari ripoti mbalimbali kabla yake zilishakionesha kuwa rushwa ni tatizo ambalo limejikita katika jamii yetu katika ngazi mbalimbali na taasisi mbalimbali nchini. Rais Kikwete akiandika katika utangulizi huo anasema “katika baadhi ya sekta za umma, rushwa imekuwa ni jambo la kawaida”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo tamaa hiyo ya wanasiasa na watendaji mbalimbali imekuwa ni chanzo kikubwa cha rushwa na vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa ni tatizo kubwa sana katika taifa letu. “tamaa ya kujilimbikiza mali kwa njia zisizo halali kunakofanywa na watendaji mafisadi na wanasiasa kunahamisha (kwa rushwa kubwa)  kiwango kikubwa cha raslimali za umma kwenda watu binafsi, na hivyo kupunguza uwezo wa serikali kutoa huduma mbalimbali za msingi na kulipa mishahara mizuri watumishi wa umma” inasema ripoti hiyo.

Kwa muda mrefu uhusiano wa rushwa na maisha ya kawaida haujawahi kuanikwa wazi namna hii kiasi cha kuonesha kuwa huduma mbalimbali za kijamii kama maji, umeme, barabara na hata mishahara ya watumishi imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na vitendo vya rushwa ambavyo vimekithiri nchini. Ripoti hii inathibitisha hoja ambazo zimewahi kutolewa na watu mbalimbali kuwa vitendo vya rushwa vinaathiri maisha na uchumi wan chi kuliko ambavyo imekuwa ikidhaniwa awali kuwa vinaathiri watu tu binafsi.

Hata hivyo ripoti hiyo inaonesha kuwa rushwa ndogondogo nayo inahusiana na umaskini wa watendaji wa ngazi za chini ambao kutokana na umaskini wao hujihusisha na rushwa hizo ili kuongezea mishahara yao. Uhusiano huu wa rushwa na mishahara unaonekana ni wa utata kwani rushwa inapoathiri mishahara ripoti inaonesha kuwa wenye mishahara hiyo midogo nao hujihusisha na rushwa na hivyo kwa namna moja kuchangia wao wenyewe kuendelea kulipwa mishahara midogo.

“Watumishi wa umma wasiolipwa vizuri na ambao wanahiji fedha zaidi ili watimize mahitaji yao ya maisha katika mazingira ambayo gharama za maisha zimependa, mfumuko wa bei na uwezekano wa kupoteza kazi siku yoyote wanaamua kujihusisha na rushwa ndogondogo ili kuongezea mapato yao. Hivyo umaskini wao unafanya rushwa ndogondogo kuendelea katika hali kama hii” ripoti hiyo ambayo iliagizwa kufanyika na kusimamiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini inasema.

Ripoti hii ya hali ya Rushwa nchini ni jumla ya ripoti tatu tofauti ambazo zote zilihusisha utafiti uliofanyika wakati mmoja  ripoti ambayo inahusisha ripoti nyingine tatu ambazo zote ziliangalia rushwa katika mazingira mbalimbali kwenye wananchi, sekta binafsi na watendaji wa umma.

Mikoa yote 21 ya Tanzania bara ilihusishwa katika utafiti huo ambapo watu wapatao 14,394 kwenye kaya mbalimbali na taasisi za umma na binafsi walihusishwa na kuulizwa maswali mbalimbali kuhusiana na hali ya rushwa. Asilimia 94 ya wote walioulizwa walijibu maswali hayo na kutoa picha ya hali ya rushwa nchini ilivyo.

Hata hivyo ripoti hiyo imekiri kuwa hali iliyoangaliwa sana ni rushwa ndogondogo kwani rushwa kubwa kwa maoni yao inahitaji utafiti mwingine ambao ungeweza kuhusisha kiasi kikubwa cha wahusika kuweza kupata picha halisi ya hali ya rushwa nchini. “Ikumbukwe kuwa rushwa kubwa inahusisha makampuni makubwa; hivyo kiwango cha rushwa kubwa kinachoangaliwa kwenye ripoti hizi kitakuwa si kamili kabisa” inasema ripoti hiyo.

Hata hivyo kama majibu ya walioulizwa ni ya kuaminiwa basi rushwa nchini inahusiana moja kwa moja na kwa kiwango kikubwa na watendaji na wanasiasa nchini. Wahusishwa walipoulizwa nani hasa anajihusisha na rushwa asilimia 84.1 walijibu kuwa ni watendaji serikalini huku wakifuatiliwa na wanasiasa ambao asilimia 44.1 ya wananchi waliwataja. Wafanyabiashara wa ndani walitajwa na asilimia 27.5 huku wafanyabiashara wa nje wakitajwa na asilimia 29.8 ya walioulizwa. Raia wa kawaida walitajwa na asilimia 29.8. Kwa kiwango chochote ni mtazamo wa Watanzania wengi kuwa rushwa ni vitendo vinavyohusisha zaidi watendaji serikalini na wanasiasa.

Hata hivyo, udhaifu mmoja ambao unaonekana kwenye ripoti hii ambayo imeandikwa kwa Kiingereza (tafsiri ya Kiswahili bado haijatolewa) ni kuwa uelewa mkubwa wa wananchi kuhusu rushwa ni mdogo na hasa maana ya neno “rushwa” lenyewe ambalo limetafsiriwa zaidi kama “malipo yasiyo halali” ili kupata huduma mbalimbali. Ripoti hii haichambui hasa “ufisadi” (corruption) jinsi ambavyo inaeleweka kiujumla wake na majibu mengi ambayo yanaakisiwa kwenye ripoti hii yanahusiana na kile ambacho kinajulikana kwenye Kiswahili hasa kama “hongo” yaani malipo yasiyo halali ili kusababisha jambo ambalo lingeweza kufanywa pasipo malipo hayo kuharakishwa kwa kupindisha taratibu na hata kuvunja sheria.

Hivyo, udhaifu huu wa maana unaakisiwa katika ripoti nzima na hivyo kushindwa kutoa picha halisi ya tatizo la ufisadi nchini na hasa maeneo yale ambayo yanaonekana kuwasumbua zaidi wananchi kama ufujaji wa mali ya umma, matumizi mabaya ya madaraka na vitendo vingine ambavyo vinaonesha uvunjaji mkubwa wa haki za wananchi kunakofanywa ili kujinufaisha. Hivyo vitu kama undugu, urafiki, kubebana na kutumia nafasi kunufaisha jamaa (hata bila kupata malipo) hakujaangaliwa ipasavyo.

Kama nilivyoandika kwenye gazeti la MwanaHalisi toleo la leo Jumatano ripoti hii inatakiwa isomwe zaidi na wana CCM na viongozi ambao hawaamini au kukubali kina cha tatizo la ufisadi nchini kwani hakuna chochote ambacho kinatajwa kwenye ripoti hii ambacho hakikutajwa kwenye ripoti ya Warioba ya 1996 au zile ripoti kama za Transparency International au za taasisi nyingine ambazo zimewahi kufanya utafiti kama huo.

Tunachoweza kukiona hata katika ripoti hii iliyoagizwa na serikali kwa shinikizo la nchi wahisani (ambao walilipia ufanyike utafiti) ni hukumu kali dhidi ya serikali ya CCM na ucheleweshaji wake unasadikiwa kufanyika makusudi ili  kuzuia kutoathiri mwelekeo wa uchaguzi mwaka jana. Ikumbukwe ripoti hii iliagizwa kufanyika mwaka 2007 na utafiti ulifanyika na kukamilika mwaka 2009. Hata hivyo ilicheleweshwa kutolewa mwishoni mwa mwaka ule au wakati wowote mwaka 2010 ikihofia kuwa vyama vya upinzani na wanaharakati wangeweza kutumia ripoti hii kujijenga kisiasa.

Hata hivyo haijulikani ni kwa kiasi gani hata kutolewa kwake hivi sasa kutaathiri mtazamo wa watu dhidi ya serikali ya CCM ambayo ndio imeunda serikali zote mbili na ambavyo inaonekana imeshindwa kabisa kushughulikia tatizo la rushwa nchini zaidi ya kufanikiwa kutoa ripoti mbalimbali ambazo zinatonesha tu machungu ya watu mbalimbali kuhusu tatizo la rushwa nchini. Kuna  uwezekano hata hivyo kama vyama vya upinzani vikapitia ripoti hizi vizuri basi chuki dhidi ya CCM na serikali yake ikazidi kuongezeka na CCM kulazimika kutumia nguvu kubwa sana kuwashawishi wananchi kuwa wanaweza kukabiliana na changamoto ya rushwa kama Rais Kikwete anavyoahidi katika utangulizi wa ripoti hiyo.

Fikra Pevu itaendelea kukuletea dodoso mbalimbali za ripoti hizi muhimu na zitapatikana kwenye mitandao mbalimbali kwani mara baada ya kutolewa hadharani siku ya Jumatatu kwenye tovuti ya TAKUKURU ripoti hizo ziliondolewa. Tunawapatia wananchi hapa ili wajisomee.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *