Zahanati za Ndundunyikanza na Mtanza zinazopatikana katika kata ya Kipugira wilayani Rufiji hazina huduma za vyoo.
Hali hiyo inawalazimu wajawazito wanaofika kwenye zahanati hizo kwa ajili ya kupima na wengine kuja kujifungua, kwenda nyumba za jirani na zahanati, na wengine hulazimika kwenda kwenye shule ya msingi ya Ndundunyikanza na Mtanza.
Mganga mkuu wa zahanati ya Ndundunyikanza Dollo Victor anasema choo hakitumiki kwa muda wa miezi minne, kutokana na vyoo hivyo kujaa na kuwapa wakati mgumu wajawazito na wagonjwa wengine wanaoenda kupata matibabu katika zahanati hiyo.
Nilishuhudia choo cha zahanati ya Ndundunyikanza kikiwa kimechafuliwa huku kikiwa kimejaa na kutoa harufu kali nainayoleta usumbufu kwa wagonjwa.
Pamoja na mganga wa zahanati kuzungumza kwamba choo hicho hakitumiki inaonekana wapo baadhi ya watu wanaingia na kujisaidia, haijulikani wanaingia muda gani.
Dollo anasema milango iliibiwa kutokana na kukosekana kwa ulinzi katika zahanati hiyo, hali ambayo inawapa mwanya wezi kufika hapo na kuchukua chochote wanachokiona kinafaa.
Hali hiyo ya kukosekana kwa huduma ya choo inaikumba pia, zahanati ya Mtanza katika kata hiyo hiyo ya Kipugira hali ambayo Mkunga muuguzi wa zahanati hiyo Fatma Mpakakwaku anaiita ni “mateso makubwa.”
Anasema huduma hiyo ya choo haipo ka muda wa miezi sita, katika zahanati hiyo na kueleza tatizo kama la Ndundunyikanza ambapo choo cha zahanati hiyo kimejaa na upande mmoja umeanguka hali ambayo inamfanya mtu aliyeko ndani kuonekana na watu walioko nje.
Hiki ndicho choo nilichokikuta Mtanza
Mkuu wa wilaya ya Rufij Nurdin Babu, anasema anaelewa umhimu wa choo katika zahanati ila aliita hali hiyo kwamba ni moja ya changamoto zinazoikabili sekta ya afya nchini.
Wakati mkuu akieleza hayo, sera ya afya ya mwaka 2007 inasema Serikali kwa kushirikiana na wadau na wananchi itaendeleza juhudi zake za kupanua na kukarabati majengo ya kutolea huduma za afya.