TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imeamua kukunjua makucha yake na kuyaelekeza kwenye sekta ya michezo nchini Tanzania ambapo tayari inawashtaki watu watano kwa tuhuma mbalimbali za rushwa, ufisadi na utakatishaji wa fedha.
Jamal Emil Malinzi (57), Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Katibu Mkuu wake Celestine Joas Mwesigwa (46) na Mweka Hazina wa shirikisho hilo Nsiande Isawafo Mwanga (27) walifikishwa mahakamani Juni 29, 2017 mbele ya Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri wa Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka 28 yakiwemo ya utakatishaji wa Dola za Marekani 375,418.
Jamal Malinzi akienda kupanda karandinga baada ya kesi yake na wenzake kuahirishwa.
Licha ya vigogo hao wa TFF, Takukuru pia iliwakamata na kuwafikisha mahakamani Rais wa klabu ya soka ya Simba, Evans Aveva na makamu wake Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ kwa makosa ya kughushi na utakatishaji wa Dola 300,000 za Marekani.
Vigogo wote hao wa michezo nchini wanaendelea kubaki rumande kwa kunyimwa dhamana kwa kuwa kisheria makosa ya utakatishaji wa fedha hayana dhamana ambapo kesi Namba 213/2017 ya akina Malinzi itatajwa tena Julai 17, 2017.
Lakini pigo jingine likawapata akina Malinzi baada ya wakili wa kujitegemea, Jerome Msemwa, kujitoa kuwatetea kwa maelezo kwamba hakupata maelekezo sahihi kutoka kwa wateja wake hao.
Katika kesi hiyo, Malinzi anakabiliwa na mashtaka 28 huku wenzake wakikabiliwa na makosa yasiyozidi manne.
Kukamatwa kwa vigogo hao wa soka kwa makosa waliyoyatenda wakiwa kwenye nyadhifa zao kumeleta taswira kwamba, kwa sasa hakuna ambaye anaweza kusalimika kwenye michezo ikiwa anajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi.
Sekta ya michezo, ambayo kwa miaka mingi ilikuwa ‘imesahauliwa’ na mamlaka za umma ikiwemo ulipaji wa kodi na ukaguzi wa hesabu, inaelezwa kwamba imegubikwa na vitendo vingi vya rushwa na ufisadi ambavyo sasa vinaweza kuibuliwa na Takukuru na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria, wakiwemo wachezaji na mashabiki.
Kupanga matokeo, kuhujumu wachezaji na timu ni mambo ambayo kwa miaka mingi yamekuwa yakilalamikiwa michezoni, hasa kandanda, hali ambayo ilielezwa kwamba ilikuwa ikidumaza michezo.
Tuhuma za akina Malinzi
Kwa muda mrefu kumekuwepo na tuhuma mbalimbali dhidi yao kuhusu matumizi mabaya ya fedha za TFF ambayo ni taasisi ya kitaifa na inasemekana Takukuru wamekuwa kwenye uchunguzi dhidi yao kwa muda sasa mpaka Juni 28, 2017 walipoamua kuwatiwa nguvuni.
Hivi karibuni gazeti la Nipashe liliandika mfululizo wa makala zilizokuwa zikielezea tuhuma za ufisadi zilielekezwa kwa Malinzi na viongozi wenzake wa TFF.
Katika Ripoti ya Ukaguzi wa fedha za udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa Taifa Stars iliyotolewa Oktoba 2, 2014, inaelezwa kuwa, mbali na mambo mengine, TBL iliamua kufanya ukaguzi huo ili kujiridhisha kama shirikisho hilo linazingatia makubaliano yaliyomo kwenye mkataba.
Ukaguzi huo ulifanywa na Mkaguzi Mkuu wa ndani wa TBL, Richard Magongo, kuwa kati ya Novemba 13, 2013 (siku 11 tangu uongozi wa sasa wa TFF uingie madarakani) na Februari 15, 2014, Dola za Marekani 315,577 (Sh. milioni 688.368) zilitumika bila ya nyaraka za kuthibitisha matumizi yake kinyume cha makubaliano ya mkataba wa pande hizo mbili.
Kati ya Novemba 11, 2013 na Machi 11, 2014, Dola za Marekani 381,248 (Sh. milioni 831.616) pia zilichotwa kwenye akaunti hiyo na kutumika kwa shughuli ambazo hazijaanishwa katika mkataba wa TBL na TFF, ripoti inabainisha.
Mchanganuo wa ripoti hiyo unaonesha kuwa, miongoni mwa waliotajwa kwenye ripoti hiyo kutumia fedha hiyo ni pamoja na Rais wa TFF, Jamal Malinzi, ambaye Desemba 24, 2013 alilipwa Dola za Marekani 159 kupitia vocha yenye namba 1075 zikiwa ni gharama za malazi hotelini (Hotel accommodation).
Ripoti inaonesha kuwa, siku hiyo hiyo (Desemba 24, 2013), Malinzi alilipwa na TFF Dola 10,000 kupitia vocha namba 1077 (Repayment to Jamal Malinzi/Marejesho ya fedha za Jamal Malinzi), kisha Februari 6, 2014 akalipwa Dola 15,934 (Loan Repayment to Jamal Malinzi/Marejesho ya mkopo kutoka kwa Jamal Malinzi) na baadaye kulipwa Dola 69,471 kupitia vocha namba 1098 na Dola 63,735 kupitia vocha namba 1401.
Wengine waliopewa fedha hiyo ya udhamini wa TBL kwa Taifa Stars ni aliyekuwa msaidizi wa Malinzi, Juma Matandika, Ali Ruvu na mwingine aliyetajwa kwa jina la S. Madadi ambao kwa pamoja walilipwa Dola 1,084 kupitia vocha namba 828 Februari 6, 2014.
Ripoti pia inabainisha malipo ya Dola 3,500 Januari 16, 2014 kwa ajili ya ziara ya Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF jijini Nairobi.
Pia zimo Dola 4,630 zilizochotwa Desemba 24, 2013 kugharamia mtihani wa utimamu wa mwili kwa waamuzi (Cooper test for referees), Dola 4,120 zilizotolewa siku hiyo hiyo kwa ajili ya Ally Mayay na Ayubu Nyenzi kufanya ziara Uganda na Dola 1,638 ambazo zilitolewa siku hiyo hiyo zikiwa fidia ya malipo ya deni la TFF kulipia ziara ya uongozi wa shirikisho mkoani Mwanza.
Dola 4,023 zilitolewa Desemba 24, 2013 kwa ajili ya posho ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa wafanyakazi wa TFF na Dola 30,000 zilitumika kwa semina elekezi kwa makocha iliyofanyika Lushoto (coach retreat at Lushoto), ripoti inasema.
Aidha, Dola 2,829 zilitumika kutoa rambirambi na misaada, Dola 3,298 zikakopeshwa kwa Chama cha Soka Mbeya huku Dola 989 zikitolewa kwa Chama cha Soka Mkoa wa Mtwara zikiwa ni msaada.
Katika ripoti hiyo, inaelezwa kuwa, Dola 90,000 zilitumika kulipia fidia ya kuvunjwa kwa mkataba wa aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen na Dola 34,177 zikatumika kununua magari mawili aina ya Toyota Hiace.
Ripoti inaeleza kuwa, kulikuwa na mawasiliano rasmi kati ya maofisa wa TFF na TBL kabla ya kufanya malipo kwa Poulsen na ununuzi wa magari hayo.
Mashtaka yanayowakabili
Juni 29, 2017 Malinzi na wenzake walisomewa mashtaka 28 huku yakiwemo ya kughushi na utakatishaji wa Dola za Marekani 375,418.
Kati ya mashtaka hayo, Malinzi pekee anakabiliwa na mashitaka 22 ya kughushi risiti mbalimbali zinazoonesha kuwa aliikopesha TFF fedha kwa nyakati tofauti, mashtaka mengine yanawahusu Celestine na Nsinde huku shtaka moja likiwahusu wote.
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nassoro Katuga kwa kusaidiana na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Leornad Swai akisoma hati ya mashtaka, aliieleza mahakama kuwa, kwa nyakati tofauti washtakiwa hao walitenda makosa hayo ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
* Shtaka la 1: Washtakiwa Jamal na Mwesigwa Juni 5, 2016 Dar es Salaam kwa nia ya kudanganya walighushi nyaraka zinazoitwa “Executive Committee Resolution” za Juni 5, 2016 wakionesha Kamati Tendaji ya TFF imebadili mtia saini wa akaunti ya benki ya TFF kutoka kwa Edgar Leonard Masoud kwenda kwa Nsiande Isawafo Mwanga wakati wakijua si kweli.
* Shtaka la 2: Septemba Mosi, 2016 katika Benki ya Stanbic tawi la Kinondoni, Mwesigwa aliwasilisha nyaraka ya kughushi.
* Shtaka la 3: Desemba 17, 2013 huko TFF, Jamal Malinzi alighushi risiti namba 308 ya Novemba 6, 2013 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 9,300 (Shs. 19 milioni) wakati akijua si kweli.
* Shtaka la 4: Malinzi anadaiwa kuwa Desemba 17, 2013 katika ofisi hiyo ya TFF, alighushi risiti namba 322 ya Desemba 17, 2013 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 10,000 (Shs. 20 milioni) wakati si kweli.
* Shtaka la 5: Malinzi anadaiwa kuwa Desemba 17, 2013 katika ofisi ya TFF alighushi risiti namba 323 ya Desemba 17, 2013 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 18,000 (Shs. 37 milioni).
* Shtaka la 6: Desemba 17, 2013, Malinzi kwenye ofisi hiyo ya TFF alighushi risiti namba 324 ya Desemba 17, 2013 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 5,000 (Shs. 10 milioni).
* Shtaka la 7: Malinzi anadaiwa kuwa Desemba 17, 2013 katika ofisi ya TFF alighushi risiti namba 325 ya Desemba 17, 2013 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 1,032(Shs. 2 milioni) wakati akijua si kweli.
* Shtaka la 8: Machi 26, 2014 katika ofisi ya TFF, Malinzi alighushi risiti namba 1956 ya Machi 26, 2014 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 40,000 (Shs. 84 milioni) wakati akijua si kweli.
* Shtaka la 9: Machi 13, 2014 katika ofisi ya TFF, Malinzi alighushi risiti namba 1957 ya Machi 13, 2014 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 5,000 (Shs. 10 milioni).
* Shtaka la 10: Mei 13, 2014 katika ofisi ya TFF, Malinzi alighushi risiti namba 1624 ya Mei 13, 2014 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 40,000 (Shs. 84 milioni).
* Shtaka la 11: Mei 16, 2014 katika ofisi ya TFF, Malinzi alighushi risiti namba 1634 ya Mei 16, 2014 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 10,000 (Shs. 20 milioni).
* Shtaka la 12: Malinzi anadaiwa kuwa Julai 11, 2014 katika ofisi hiyo ya TFF alighushi risiti namba 1860 ya Julai 11, 2014 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 15,000 (Shs. 30 milioni).
* Shtaka la 13: Malinzi anadaiwa kuwa Julai 11, 2014 katika ofisi hiyo ya TFF alighushi risiti namba 1861 ya Julai 11, 2014 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 3,000 (Shs. 6 milioni).
* Shtaka la 14: Julai 15, 2014 katika ofisi hiyo ya TFF, Malinzi alighushi risiti namba 1863 ya Julai 15, 2014 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 14,000 (Shs. 28 milioni).
* Shtaka la 15: Julai 15, 2014, Malinzi katika ofisi ya TFF alighushi risiti namba 1866 ya Julai 15, 2014 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 4,000 (Shs. 8 milioni).
* Shtaka la 16: Malinzi anadaiwa kuwa Julai 25, 2014 kwenye ofisi ya TFF alighushi risiti namba 1876 ya Julai 25, 2014 akionesha TFF imeikopesha TFF Dola za Marekani 1,000(Shs. 2 milioni).
* Shtaka la 17: Agosti 19, 2014 huko TFF, Malinzi alighushi risiti namba 1890 ya Agosti 19, 2014 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 5,000 (Shs. 10 milioni).
* Shtaka la 18: Oktoba 11, 2014 kwenye ofisi hizo za TFF, Malinzi alighushi risiti namba 1568 ya Oktoba 11, 2014 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 1,200 (Shs. 2.4 milioni) wakati akijua si kweli.
* Shtaka la 19: Malinzi anadaiwa kuwa Agosti 17, 2015 kwenye ofisi hiyo ya TFF alikula njama ya kughushi risiti namba 1511 ya Agosti 17, 2015 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 5,000 (Shs. 10 milioni).
* Shtaka la 20: Julai 22, 2015 kwenye ofisi za TFF, Malinzi alighushi risiti namba 2981 ya Julai 22, 2015 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 2,000 (Shs. 4 milioni).
* Shtaka la 21: Mei 9, 2016 kwenye ofisi ya TFF, Malinzi alighushi risiti namba 832 ya Mei 9, 2016 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 7,000 (Shs. 14 milioni) wakati akijua si kweli.
* Shtaka la 22: Juni 16, 2016 katika ofisi ya TFF iliyopo Ilala Dar es Salaam, Malinzi alighushi risiti namba 931 ya Juni 16, 2016 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 10,000 (Shs. 20 milioni).
* Shtaka la 23: Malinzi Agosti 2, 2016 katika ofisi ya TFF alighushi risiti namb 947 ya Agosti 2, 2016 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 1,000 (Shs. 2 milioni).
* Shtaka la 24: Septemba 19, 2016 katika ofisi ya TFF, Malinzi alighushi risiti namba 1029 ya Septemba 19, 2016 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 1,000 (Shs. 2 milioni).
* Shtaka la 25: Septemba 22, 2016 katika ofisi ya TFF, Malinzi alikula njama ya kughushi risiti namba 1071 ya Septemba 22, 2016 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 15,000 (Shs. 30 milioni).
* Shtaka la 26: Kati ya Septemba Mosi na Oktoba 19, 2016 washtakiwa Malinzi, Mwesigwa na Nsiande kwa pamoja na kwa kushirikiana walitakatisha fedha kiasi cha Dola za Marekani 375,418 huku wakijua fedha hizo ni zao la kughushi.
* Shtaka la 27: Malinzi na Mwesigwa wanadaiwa kuwa katika kipindi hicho cha Septemba Mosi na Oktoba 19, 2016 katika Benki ya Stanbic Tawi la Kati la Kinondoni walijipatia Dola za Marekani 375,418 wakati wakijua fedha hizo zimetokana na kughushi.
* Shtaka la 28: Nsiande Mwanga anadaiwa kuwa kati ya Septemba Mosi na Oktoba 19, 2016 katika ofisi ya TFF alimsaidia Malinzi na Mwesigwa kujipatia Dola za Marekani 375,418 kutoka Benki ya Stanbic huku akijua upatikanaji wake umetokana na kughushi.
Rais wa Simba na makamu wake
Rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva, na makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’ nao wako rumande hadi Julai 13, 2017 kesi yao ya utakatishaji wa Dola za Marekani 300,000 (Shs. 620 milioni) itakapotajwa tena.
Viongozi hao walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 29, 2017 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa, wa Mahakama ya Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matano yakiwemo kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha Dola za Marekani 300,000 (Sh620 milioni).
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Christopher Msigwa, aliwasomea hati ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa.
* Shtaka la 1: Machi 15, 2016 Dar es Salaam washtakiwa hao walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha wakionesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa Dola za Marekani 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.
* Shtaka la 2: Machi 15, 2016 katika Benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala Aveva akijua alitoa nyaraka za uongo ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha.
* Shtaka la 3: Aveva na Kaburu wanadaiwa kuwa kati ya Machi 15 na Juni 29, 2016 jijini Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata Dola za Marekani 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.
* Shtaka la 4: Aveva anadaiwa kuwa Machi 15, 2016 katika Benki ya Barclays Mikocheni, alijipatia Dola za Marekani 300,000 akijua zimetokana na kughushi.
* Shtaka la 5: Mshtakiwa Kaburu anadaiwa kuwa Machi 15, 2016 katika Benki ya Barclays tawi la Mikocheni alimsaidia Aveva kujipatia Dola za Marekani 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.
Hawa si wa kwanza
Hii siyo mara ya kwanza kwa Takukuru kuwafikisha mahakamani wanamichezo kwa vitendo vya rushwa, kwani aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT – sasa TFF), Ismail Aden Rage, aliwahi kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa mwaka 2005 kwa kosa la kuiba mipira 50 na Shs. 3 milioni mali ya chama hicho.
Hata hivyo, Rage alitolewa katika Gereza la Segerea kwa msamaha wa Rais (mstaafu) Benjamin Mkapa mwishoni mwa mwaka huo akiwa tayari ameshatumikia kifungo kwa miezi mitatu.
Lakini Rage alikuwa ameshakata rufaa kupinga hukumu iliyomtupa jela na baada ya kupata msamaha wa rais aliamua kuendeleza kesi hiyo kwa lengo la kujisafisha ambapo Machi 27, 2008 Mahakama ya Rufaa ikamfutia hukumu.
Majaji wa Mahakama ya Rufaa, Damian Lubuva, John Mrosso na Salim Mbarouk walibaini kuwa hakukuwa na ushahidi ulioonyesha kuwa Rage aliiba mipira 50 kati ya 600 ambayo alituhumiwa kuwa aliipokea Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam.
Rage alikuwa anadaiwa kufanya kosa hilo kati ya Februari na Machi 1999. Kesi hiyo ilifunguliwa baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kuunda tume ya kuchunguza tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Shs. 600 milioni za FAT.
Tume hiyo ilibaini baadaye kuwa ni kiasi cha Sh milioni 160 ndizo zilizokuwa zinaonekana kufujwa na kuwasilisha ripoti kwa mkurugenzi wa taasisi ya kuchunguza makosa ya jinai, DCI, ambayo ilibaini kuwa kiasi cha Sh milioni 40, ikiwa ni fedha na mali za FAT, ndizo zilizoibwa na kuiagiza polisi kufungua mashtaka.
Mbali na Rage, washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo walikuwa mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Muhidin Ndolanga, mhasibu Yonaza Seleki na mfanyabiashara, Specioza Lugazia.
Takukuru pia iliwahi kumfikisha mahakamani mchezaji wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe, mwaka 2011 kwa madai kwamba alitaka kumhonga kipa wa Mtibwa Sugar, Shaaban Kado, ili timu ya Simba ishinde mechi baina yao ambayo ilichezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Huu ni mwanzo wa utungu, na kwa kadiri hali ilivyo, ni vyema Takukuru ikaongeza kasi kuchunguza vitendo vya rushwa na ufisadi kwenye michezo ambavyo vinaifanya Tanzania ishindwe kufanya vyema kimataifa.