Daniel Samson
Sekta ya maji inagusa maisha ya kila siku ya mwanadamu. Uhai wa binadamu kwa kiasi kikubwa unategemea uwepo wa maji lakini vitendo vya rushwa huathiri utolewaji wa huduma hiyo katika jamii.
Ripoti ya utafiti wa Shirika la Twaweza (2017) juu ya sauti za wananchi inaonyesha rushwa imepungua katika sekta ya maji ikilinganishwa na sekta zingine ikiwemo za polisi, mahakama, na ajira ambazo ziko katika nafasi ya juu.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa wananchi waliohojiwa wanasema rushwa katika sekta ya maji imepungua hadi kufikia asilimia 26 mwaka huu kutoka asilimia 10 miaka 3 iliyopita. Hii inaweza kuashiria kuwa idadi kubwa ya watu wametambua umuhimu wa maji kama huduma ya msingi kwa wananchi na sio hisani.
Rushwa ni dhana mtambuka inayohusisha pande mbili za mtoaji na mpokeaji ili mtu apate upendeleo wa kupata huduma fulani katika jamii. Kati ya wananchi 1, 705 waliohojiwa ni wananchi 308 ndio walisema walipokea na kutoa rushwa katika sekta ya maji. Waliopokea ni asilimia 6 na waliotoa ni asilimia 5 tu.
Kwa mwaka 2014 waliotoa na kupokea rushwa katika sekta ya maji walikuwa ni asilimia 20 lakini idadi hiyo imeshuka kwa asilimia 14 hadi kufikia 6% mwaka huu. Inaelezwa kuwa dhamira ya dhati ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kupambana kivitendo na rushwa imeachangia kwa sehemu kupunguza vitendo vya rushwa.
Hali hiyo imerudisha nidhamu na uwajibikaji kwa watoa huduma za maji hasa wale waliopo katika ofisi za umma. Pia uzoefu wa wananchi kukutana na matukio ya rushwa umepungua ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita.
“Sambamba na mtazamo wao kuhusu rushwa, uzoefu wa waananchi kuhusu rushwa pia umeshuka tangu mwaka 2014 kwa polisi, Ardhi, huduma ya afya, mashirika yasiyo ya kiserikali, maji na kodi, idadi ya wananchi wanaosema kuwa waliombwa rushwa imepungua katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita”, inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Licha ya ripoti hiyo kubainisha wazi kupungua kwa rushwa katika sekta ya maji lakini sekta hiyo inakabiliwa na ongezeko kubwa la mahitaji ya maji yanayotumiwa viwandani na wakazi wa miji mikubwa. Hali hiyo inaelezwa kuathiri kilimo ambacho kinatumia maji mengi katika shughuli zake.
Kulingana na Benki ya Dunia (WB) katika ripoti yake ya Mapitio ya Uchumi ya mwaka 2017, inaitaja Tanzania kutumia asilimia 80 ya maji yake yote katika shughuli za kilimo. Matumizi hayo ni makubwa ikilinganishwa na matumizi ya dunia ambayo yanafikia 70% katika kilimo. Lakini ukuaji wa miji na viwanda unatishia kupungua kwa maji yanayotumika katika sekta ya kilimo.
Ili kuthibiti ongezeko kubwa la mahitaji ya maji, serikali na wananchi wanashauriwa kutunza vyanzo vya maji na kutumia teknolojia ya kisasa kuvuna maji ambayo yanaweza kutumika kipindi ambacho nchi haina maji ya kutosha.
Teknolojia ya kuhifadhi maji imeonyesha mafanikio makubwa katika nchi zilizoendelea ikiwemo Marekani ambayo inawekeza nguvu kubwa katika uvunaji wa maji na kuachana na matumizi ya maji ya visima ambayo yanaathiriwa na maendeleo ya viwanda.