Rushwa: TAKUKURU wanangoja nini kukamata aliyetaka kumhonga Rais?

Jamii Africa

ALHAMISI, Mei 25, 2017 Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, aliibuka na kusema kwamba wapo wahujumu uchumi waliotaka kumhonga Rais John Magufuli kiasi cha Shs. 300 bilioni ili kusitisha zoezi la uchunguzi wa mchanga wa dhahabu (makanikia).

Polepole alitoa kauli hiyo wakati akitoa wito kwa wananchi, kumuunga mkono Rais Magufuli katika kipindi hiki kigumu kwani nchi iko katika vita mbaya ya uchumi ambayo wahujumu uchumi wamelenga kupigana na maisha ya Watanzania na kurudisha nyuma maendeleo ya Taifa.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphery Polepole

Kauli ya Polepole ilikuja siku moja tu baada ya Rais Magufuli kupokea Ripoti ya Kamati Maalum ya kwanza ya Rais iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma, ambayo ilikuwa inachunguza viwango vya dhahabu na madini mengine katika makontena 277 ya makanikia yaliyozuiliwa bandarini ambayo yalikuwa yasafirishwe kupelekwa China na Japan.

“Kuna watu walitaka kumhonga rais bilioni 300 ili kusitisha uchunguzi. Walitaka kuhonga bilioni 300 kwa ajili ya kusitisha uchunguzi huo, hivi wao wanapata fedha kiasi gani? Lakini rais akawatolea nje, akasema subirini uchunguzi ukamilike. Tusimame naye na hakika tutashinda na historia itaandikwa kwamba tulisimama katika kulinda urithi wetu,” alisema.

Akasema kwamba, kuna vita za aina nyingi, lakini kwa sasa vita za uchumi ndizo mbaya zaidi kwa kuwa zinalenga kurudisha nyuma maendeleo.

“Vita ziko za aina nyingi, ziko zile tunazopigana kwa silaha mtu na mtu, na nchi na nchi, lakini sasa ziko vita za kiuchumi, ni mbaya zaidi zinalenga kuturudisha nyuma.Wahujumu uchumi hawapigani na rais, bali wanapigana na maisha ya wananchi wa Tanzania, tukiwa wamoja tutashinda vita hii, wako watu wanaipinga vita hii yenye dhamira njema, huu si wakati wa kutofautiana ni wakati wa kusimama kumshinda adui,” alisema Polepole.

Polisi, TAKUKURU wako wapi?

Polepole ni kiongozi wa CCM, chama tawala, na alichokisema wengi tulitegemea kitamkwe na ama Jeshi la Polisi lenye kusimamia utii wa sheria na usalama wa raia au Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ambayo ndiyo yenye dhamana.

Kwa hapa tusingetegemea kusikia kauli tu, bali tungepaswa kuona huyo aliyetaka kumhonga Rais akifikishwa kwenye mikono ya sheria na kushughulikiwa kwa sababu tunaamini ‘Rushwa ni adui wa haki’.

Rais Magufuli akiangalia makontena yenye mchanga wa dhahabu bandarini Dar es Salaam.

Kutolewa kwa kauli hiyo nzito, ambayo ni kashfa kubwa, na kiongozi wa chama kunazua maswali mengi yasiyo na majibu.

Je, ina maana CCM ndiyo yenye taarifa za kuhongwa kwa Rais na vyombo husika havikupata? Kama viliipata, vimefanya jitihada gani katika jambo hilo?

Kwa kauli ya Polepole, kwamba Rais aliwatolea nje kwa kuwataka wasubiri uchunguzi ukamilike, ina maana hawa watu wanajulikana na wanafahamika. Sasa kwa nini wasikamatwe?

Kimsingi, kauli ya Polepole ni nzito mno ambayo haiwezi kuachwa ikapita hivi hivi, hasa kwa kuzingatia kwamba Urais ni taasisi nyeti na hivyo kuhusishwa na rushwa ni kashfa kubwa inayohitaji kuchukuliwa hatua stahiki.

Kuna ukweli?

Jambo hili ni zito sana hata katika uso wa kimataifa na sitaki kuamini kama Polepole amelifanya kwa kusukumwa na mtazamo wa ‘kisiasa’ zaidi kuliko uhalisia.

Ikiwa kuna ukweli ni vyema hatua zikachukuliwa, lakini kama limefanywa kisiasa, tuelewe kwamba tutakuwa tumemharibia na kumpotezea heshima ya kimataifa rais wetu pamoja na taifa kwa ujumla.

Tumeshuhudia kashfa nyingi za rushwa zikiwahusisha watawala, na kwa kiasi kikubwa baadhi ya watawala wameng’oka madarakani kwa sababu ya kashfa hizo.

Tumeshuhudia pia namna baadhi ya watawala walivyojilimbikizia mali kwa vitendo vya rushwa na kuziacha nchi zao zikiwa katika umaskini pamoja na madeni makubwa.

Kitendo cha kusikia kwamba Rais wetu alitaka kuhongwa halafu akakataa rushwa, kwanza, kinatia matumaini kwamba tunaye rais mzalendo anayechukia rushwa kwa vitendo na anayeziangatia na kupigania maslahi ya umma.

Lakini pili, Watanzania wanaona kwamba suala la rushwa kubwa kubwa kwa viongozi wa umma bado linaitafuna nchi na kitendo kilichotaka kufanywa kwa rais inaonyesha kwamba wapo watumishi wengi wa umma ambao wamekuwa wakipokea rushwa ili kupindisha mambo na kuuharibu uchumi.

Rais Magufuli alipokagua bandarini na kuzuia usafirishaji wa makondena yenye mchanga wa dhahabu.

Kwa mazingira ya Tanzania, kama zilivyo nchi nyingi zinazoendelea hasa zenye rasilimali za madini, wengi tulitegemea kwamba katika mchakato wa uchunguzi wa makanikia lazima rushwa kubwa kubwa ilikuwa inatembea.

Hii ilijidhihirisha pia mara tu baada ya Rais Magufuli kupiga marufuku usafirishaji wa makanikia, ambapo kupitia mitandao ya kijamii, wapo watu waliotokwa na mapovu kupinga uamuzi huo na kutetea usafirishaji huo.

Kwamba, michezo hiyo michafu ilimfikia mpaka hatua ya kutaka kumhonga Rais kwa kweli ni jambo ambalo linaonekana kuvuka mipaka na dharau kubwa kwa Taasisi ya Urais.

Pengine ndiyo maana wakati akkipokea ripoti hiyo, Rais Magufuli alisema kwamba wapo watu waliokuwa wanataka kukwamisha uchunguzi huo.

Rais Magufuli akipokea ripoti kutoka kwa Profesa Abdulkarim Mrutu.

“Vifaa vyote katika ulinzi vilitumika japokuwa wapo waliojitokeza kutaka kuingilia uchunguzi huo na majina yote ya waliotaka kuvuruga uchunguzi tunayo. Wapo wengine mnawajua wenyewe wakibwatuka, wengine kwenye mitandao, wamepewa fedha.

“Ndugu zangu, tuko kwenye vita na vita ya uchumi ni mbaya sana, mabilioni ya fedha haya ambayo nchi yetu imepoteza, dhahabu tani 7.8 hadi 13.16 kwa kontena 277. Tani 15.5 ni malori mawili na Land Rover moja. Malori mawili ya tani 7 yanaleta tani 14, labda na pick-up zote umezipaki pale na hio ni kwa makontena 277,” alisema Rais Magufuli.

Akaongeza: “Kuna kamati inayotaka kujua makontena yanasafirishwa mangapi, haraka haraka ni makontena 250 na 300 kwa mwezi, kwa mwaka zaidi ya makontena 3,600.

“Ni kitu cha kuumiza mno na kwa hili Watanzania wote tushikamane, hospitali watu wanakosa madawa, mashuka, shule watu wanakosa madawati, fedha za treni mpaka tukope kumbe kuna fedha zinamwagika hapa.

Nilimfukuza Katibu Mkuu wa Nishati na Madini alipoulizwa na Kamati ya Wabunge kiasi cha dhahabu kilichopo, ni aibu kwa mtu aliyesomeshwa na Watanzania such a stupid comment (kutoka kauli ya kipuuzi kama ile).

“(Shilingi) Bilioni 676 hadi trilioni 1.5 tunazipoteza Watanzania, madini mengine hawakujali hata kuyarekodi (Nipe ile document). Tunaweza tukaona kwa miaka 17, tulipaswa kuwa donor country (nchi hisani) kwa vitu tulivyopewa na Mungu,” alisisitiza.

Uwajibikaji muhimu

Suala hili linahitaji uwajibikaji, na TAKUKURU wanapaswa kuwajibika ama kwa kuwakamata wale wote waliotaka kukwamisha uchunguzi kwa hila, ikiwemo kutaka kumhonga Rais, au kwa wao wenyewe kujiuzulu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Haiwezekani TAKUKURU wapo halafu watu wengine wanakaa na kuamua kupanga kumhonga rais kisha wanaangaliwa. Kama hali hiyo ikiachiwa, basi taifa litakuwa limefika pabaya zaidi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *