Mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya umetajwa kuwa sababu iliyomsukuma Mbunge wa Singida Kaskizini, Lazaro Nyalandu kujivua wadhifa wa ubunge na kuondoka CCM, Fikra Pevu imeelezwa.
Nyalandu ambaye alishiriki katika mchakato huo, lakini hivi karibuni ameonekana kutofautiana na msimamo wa chama chake akitaka katiba ya Warioba ndio ipitishwe huku akiwataka wabunge wenzake kukataa hoja ya kuondoa ukomo wa urais ambayo imekuwa ikitolewa na baadhi ya wananchi.
“Nawashukuru wabunge wenzangu CCM na upinzani wanaounga mkono hoja ya kurejea upya Rasimu ya Katiba Mpya kama ilivyopendekezwa na Tume ya Warioba”, aliandika Nyarandu Oktaba 23 mwaka huu katika ukurasa wake wa Twitter na kuongeza kuwa,
“Wabunge tusikubali hoja zinazolenga kukiuka ukomo wa muda wa uongozi uliowekwa kikatiba wa miaka mitano. Tujikite kupata Katiba Mpya Tanzania”.
Katika kuendeleza hoja yake ya Katiba Mpya, Nyalandu alikaririwa kuanza mchakato wa kufikisha hoja binafsi kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ya kurejea mchakato wa Katiba Mpya aliyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba.
Katiba ya Warioba ilizingatia mapendekezo mengi ya wananchi lakini kutokana na kutishia maslai ya wanasiasa wakiwemo wale wa chama tawala ilipingwa vikali na ikabadilishwa na kuwa na Katiba Pendekezwa au Katiba ya ‘Chenge’.
Kabla hajatimiza hazma ya kufikisha hoja binafsi bungeni, Nyalandu ameamua kujivua nafasi yake ya ubunge na uongozi ndani ya CCM huku akiwa na dhamira ya kuhamia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Licha ya Mbunge huyo kutaja sababu za kujiuzulu nafasi ya Ubunge na kuhama kutoka katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa ni ongezeko la ukiukwaji wa haki za binadamu na vitendo vya udhalimu wanavyofanyiwa baadhi ya watanzania, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaeleza kuwa tofauti za kisiasa ambazo zinaendelea katika chama chake zinaweza kuwa zimechangia uamuzi huo.
Nyalandu amechukua uamuzi wa kujiuzulu leo katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari siku chache baada ya kumaliza ziara ya kutembelea wananchi katika jimbo lake la Singida Kaskazini.
Amesema amechukua uamuzi huo akiwa na hazma ya kutimiza haki yake ya kikatiba na ameamua kukihama Chama Cha Mapinduzi na kujivua nafasi ya Ubunge.
“Nimeamua kujiuzulu nafasi yangu ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na nafasi zote za Uongozi ndani ya Chama kuanzia leo, Oktoba 30, 2017”.
“Asubuhi ya leo nimemwandikia Spika wa Bunge, Mh. Job Ndugai, barua ya kujiuzulu nafasi yangu ya Ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini kupitia tiketi ya CCM, nafasi ambayo nimeitumikia kwa vipindi vinne mfululizo tangu nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2000 hadi Sasa”. – Lazaro Nyalandu.
Fikra Pevu imeelezwa kuwa dalili za Nyalandu kutofautiana na misimamo ya chama chake (CCM) zilianza kujitokeza hivi karibuni katika tukio la kushambuliwa na kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu mapema Septemba mwaka huu, ambapo alishambuliwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma.
Lissu alitibiwa katika hospitali ya Mkoa Dodoma na baadaye alihamishiwa katika Hospitali ya Nairobi iliyopo nchini Kenya ambako anaendelea na matibabu mpaka leo.
Akiwakilisha wabunge wa mkoa wa Singida, Septemba 16 mwaka huu Nyalandu alifunga safari mpaka Nairobi kumjulia hali Tundu Lissu huku akiwataka watanzania kuweka pembeni tofauti zao kisiasa na kidini na waungane kwa pamoja kupinga dhuluma dhidi ya watanzania ambao wanashambuliwa na watu wasiojulikana.
"Nimefika hospitali ya Nairobi mapema leo kumjulia hali Mhe. Tundu Lissu. Naamini kwamba hatua zaidi na haraka zitahitajika kumsadia apate huduma za kitabibu katika ubora na ufanisi uliopo kwa sasa duniani. Ni maombi yangu kwetu sote, tuweke pembeni tofauti zetu za kiitikadi, ama mitazamo, tuungane na kushikamana kama Taifa kwa ajili ya kumwomba Mungu anyooshe mkono wake, na kumponya”, alinukuliwa Nyalandu na vyombo vya habari akiwa Nairobi.
“Aidha, shambulio hilo walilolifanya watu wasiojulikana limedhalilisha taifa, na kudhoofisha taswira ya kukomaa kwa demokrasia inayoruhusu kuvumiliana na kuheshimiana licha ya tofauti zetu za kiitikadi na mitazamo ya kisiasa”, Alinukuliwa Nyalandu akiongelea hali ya Lissu.
Kutokana na hali ya Lissu kuimarika, mikakati mbalimbali ya kumtoa Nairobi kumpeleka katika nchi nyingine kwa ajili ya matibabu zaidi ziliendelea. Hata katika hatua hiyo, Nyalandu alijitokeza tena kutaka kufanya mipango ya kumsafirisha Lissu hadi Marekani kupata matibabu. Lakini mkakati huo ulikwama kwasababu madaktari walishauri kuwa hali ya mgonjwa hairuhusu kusafirishwa.
Nyalandu ambaye kwa ushirikiano wa Shirika la Samaritan’s Purse, mwezi Mei mwaka huu alifanikisha safari ya wanafunzi 3 majeruhi wa ajali ya basi la Shule ya Msingi Lucky Vincent iliyoua watu 35 kuelekea Marekani kwa ajili ya matibabu ambapo walilazwa katika hospitali ya Mercy iliyopo Jiji la Sioux, Iowa. Kwa kutumia ushawishi wa shirika hilo, Nyalandu na familia ya Lissu walianza mikakati ya kumsafirisha Lissu nje ya Kenya kabla ya kupata pingamizi la madaktari wa Nairobi.
Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (katikati) akiteta jambo na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Kushoto) na Godbless Lema, Arusha Mjini (Kulia), Ezekiel Wenje, mwanachama wa CHADEMA na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari (akiwa nyuma ya Nyalandu), hivi karibuni jijini Nairobi, Kenya.
Hata aliporudi nchini akitokea Kenya, Nyalandu aliendelea kutoa matamko ambayo yalikuwa yanapinga vitendo vya kuminya demokrasia na kuvamiwa kwa baadhi ya watanzania ambavyo vimekuwa vikitokea katika maeneo mbalimbali nchini.
Fikra Pevu imeelezwa kwamba kuna tofauti ya mitazamo ndani ya CCM kuhusu kushirikiana na wapinzani katika masuala mbalimbali ya kitaifa, ambapo wengine wanaliona suala hilo kama ni uzalendo lakini baadhi ya viongozi wanaliona kama ni usaliti kwa chama.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya wanachama kuogopa kushirikiana na wanachama wa vyama vingine kwa kuhofia kuchukuliwa hatua ndani ya chama.
Mwaka 2016, alisikika kiongozi mmoja wa ngazi ya juu CCM akisema watu ambao wanaenda kuwaona wabunge wa upinzania ambao wamepata matatizo ya kuumwa au kufungwa jela wanakisaliti chama.
Hatua hiyo ilimlazimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, ambaye pia ni Mbunge wa Igunga, Dkt. Peter Kafumu na Makamu wa Kamati hiyo, Vicky Kamata (Mbunge Viti Maalumu-CCM) kujiuzulu nafasi zao katika kamati hiyo Ili kuonyesha hisia za kutoridhishwa na msimamo huo wa baadhi ya viongozi wa CCM.
Sababu ya kujiuzulu kwao zinatajwa kuwa walikuwa na mipango ya kwenda kumuona Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) ambaye alikuwa anashikiliwa katika gereza la Kisongo mkoani Arusha kwa tuhuma za uchochezi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ameandika katika ukurasa wake wa Facebook akimpongeza Nyalandu kwa uamuzi aliyoufanya, ambapo amesema,
“Lazaro Nyalandu, umeonyesha Uongozi. Kwa namna haki za watu zinavyovunjwa na Uchumi wa Nchi unavyoporomoka. Umefanya maamuzi sahihi, wakati sahihi na kwasababu sahihi. Kila la kheri”.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaeleza kuwa kitendo cha Nyalandu kujiuzulu kinaweza kuwa ni shinikizo ndani ya chama chake kutokana na mwenendo ambao amekuwa akiuonyesha hivi karibuni ambao unatajwa kutofautiana na misamamo ya baadhi ya viongozi wa chama tawala.