Sababu za wanajeshi wa Tanzania kuendelea kulinda amani nchini Congo DRC

Jamii Africa

Inaelezwa kuwa vikosi vya jeshi la Tanzania kuendelea kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  (Congo DRC) licha ya kupoteza wanajeshi wake 14 katika shambulio dhidi ya waasi, inatajwa kuwa ni hatua ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia ikiwemo shughuli za kibiashara

Wiki iliyopita wanajeshi 14 wa Tanzania na 5 wa Congo DRC  waliuwawa na wengine zaidi ya 44 walijeruliwa  katika shaumbulio linalotajwa kuwa baya tangu mapigano dhidi ya waasi yaanze katika ukanda wa mashariki mwa nchi hiyo hasa eneo la Kivu ambalo kwa sehemu kubwa linazungukwa na makundi ya waasi.

 Kwa mujibu wa Umoja wa Taifa (UN) unasema shambulio hilo lilitokea Desemba 7 mwaka huu katika kambi ya jeshi ya ulinzi wa amani (MONUSCO). Waasi wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) walivamia kambi ndogo iliyopo eneo la daraja la mto Simulike barabara ya kutokea Oicha kwenda Kamanga mpakani mwa Uganda Kaskazini Mashariki ya Wilaya ya Beni, jimbo la Kivu Kaskazini.  

Siku chache baada ya shambulio hilo serikali ya Tanzania kupitia Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali James Mwakibola alisema shambulio hilo limeleta madhara makubwa lakini kikosi chao kilichopo huko kina uwezo wa kutekeleza majukumu kwa uweledi na umahiri stahiki.

Msimamo huo wa serikali unathibitisha wazi kuwa vikosi hivyo vitaendelea kuwepo katika nchi hiyo ili kurejesha amani na kuimarisha uhusiano uliopo ikiwemo kukuza shughuli za kibiashara baina ya nchi hizo mbili.

Mahusiano ya kibiashara ya DRC na Tanzania yanaungwanishwa na Bandari ya Dar es Salaam ambayo hutumika kuingiza mizigo inayotoka nje za nchi kwenda Congo DRC kupitia mtandao wa barabara na reli. Licha ya DRC kuwa na maziwa na mito lakini haina bandari inayounganisha na maeneo mengine ya dunia na kulazimika kutumia bandari ya Dar es Salaam kupitisha mizigo.

Kulingana na taasisi ya TradeMark East Africa inaeleza kuwa mizigo inayosafirishwa kuelekea DRC kupitia bandari ya Dar es Salaam imeongezeka mara kumi zaidi kila mwaka katika miaka 13 iliyopita. DRC ni msafirishaji wa pili wa mizigo inayoingia katika bandari ya Dar es Salaam ambapo ni asilimia 25 ya mizigo yote inayopita katika bandari hiyo.

Takwimu zinaonyesha kuwa usafirishaji wa mizigo ya DRC umeongezeka kwa wastani wa asilimia 24 tangu mwaka 2004 ambapo ilikuwa tani 155,611 na kufikia tani 1,117,249 mwaka 2013. Njia inayotumika zaidi ni mtandao wa barabara ambao unaanzia Dar es Salaam kupitia mikoa ya Nyanda za Juu kusini na kuingia Zambia kisha kuunganisha katika maeneo ya Mashariki mwa Congo.

Rais Joseph Kabila wa Congo DRC akipokelewa na rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli katika moja ya ziara alizofanya hapa nchini mwaka huu.

 

Ili kuimarisha mahusiano ya kibiashara, mwaka 2016 nchi hizo zilikubaliana kutumia reli ya TAZARA  inayounganisha nchi za Tanzania na Zambia na kuongeza wigo kwa kuinganisha reli ya Congo DRC (SNCC) ili kukidhi mahitaji ya kibiashara ya Congo, nchi yenye utajiri mkubwa wa madini.

Kulingana na ripoti ya shirika la reli la  TAZARA ya mwaka 2016 inaeleza imefanya maboresho mbalimbali ya miundombinu na kuifikia reli ya Congo DRC ambapo muda wa kusafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam hadi Lubumbashi  Congo DRC umepungua kutoa siku 40 hadi kufikia siku 10. Na TAZARA pekee inasafirisha mizigo kati ya Dar es Salaam na mji wa New Kapili-Mposhi uliopo Zambia kwa wastani wa siku tano.

Hata hivyo, serikali imeendelea na  mradi mkubwa wa upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam unaojulikana kama ‘Dar es Salaam Marine Gateway Project (DMDP)’ ambao unalenga kuifanya bandari hiyo kuwa na hadhi ya kimataifa na kuwezesha kupokea meli kubwa na kuhifadhi mizigo mingi.

Mradi huo wa DMGP umefadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) ambapo Tanzania imepokea Dola za Kimarekani milioni 345 kukamilisha mradi huo ambapo utaongeza uwezo wa kupokea mizigo kwa tani milioni 25 miaka saba ijayo. Pia utapunguza muda wa kusubiri kutoka saa 80 hadi 30.

Kukamilika kwa mradi huo kutafungua zaidi milango ya kibiashara katika ya Tanzania na DRC. Lakini kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa mizigo unatatizwa na mapigano ya waasi dhidi ya serikali ya Congo, ambapo malori ya mizigo yamekuwa yakishambuliwa na kushindwa kufika kule yanakotakiwa kwenda.

Mwaka jana, malori 12 kutoka Tanzania yalitekwa na waasi wa Maimai katika eneo NamoyoJimbo la Kivu Kusini nchini DRC na n akuyateketeza malori 4 na kuwashikilia mateka madereva kwa siku kadhaa kabla ya kuwatelekeza.

Kutokana na mahusiano ya kibiashara, Tanzania kupitia kikosi cha ulinzi cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO) alipeleka wanajeshi wake   kulinda amani mashariki mwa DRC ili kuwalinda raia ambao wamekuwa wakisumbuliwa na waasi.

Ramani ya Tanzania na Congo DRC

 

Historia ya Mapigano Congo DRC

 Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) nchi ya yenye utajiri wa madini lakini imekuwa kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu tangu kuondoka kwa rais Mobutu Sese Seko. Mpaka sasa inakadiliwa kuwa watu milioni 6 wamekufa kutokana na mzozo wa kisiasa katika nchi hiyo.

Mapigano katika nchi hiyo yanachochewa na sababu za kisiasa na kiuchumi ambapo uwepo wa madini umeibua mivutano ya makundi ya kijeshi kutawala katika maeneo yenye manufaa ya kiuchumi.

Nchi hiyo ambayo ilijipatia uhuru wake 1960 kutoka kwa wakoloni wa Ubeligiji  ambapo mwaka 1965 Mobutu  Sese Seko alichukua madaraka na kuitawala Congo mpaka ilipofika 1997 akaondolewa na waasi waliongozwa Laurent Kabila.

Licha ya Kabila kuingia madarakani hali haikutulia, vita vya ndani viliendelea tangu mwaka 1997 hadi 2003, lakini mwaka 2001 rais Kabila uliuwawa na mlinzi wake wakiwa kwenye ndege. Mtoto wake Joseph Kabila akapewa madaraka mpaka 2006 ulipofanyika uchaguzi wa kidemokrasia ambao ulimbakiza madarakani.

Mwaka 2011 ulifanyika uchaguzi mwingine na Kabila akachaguliwa tena kuwa rais lakini hakufanikiwa kukomesha mapigano ya waasi. Na baada ya kumaliza kipindi chake cha pili cha uongozi inaelezwa anataka kugombea tena lakini anakabiliwa na shinikizo kubwa la wananchi na vyama vya upinzani asigombee tena. Kukosekana kwa utulivu nchini humo kumeifanya Tume ya Uchaguzi kusogeza uchaguzi mkuu wa rais mpaka mwaka 2018.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *