Safari bado ni ndefu kuelekea uhuru wa kweli kwa vyombo vya Habari Tanzania

Jamii Africa

Tanzania inaungana na nchi zingine duniani kusherekea Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani huku kukiwa sintofahamu ya uhai wa vyombo hivyo kutokana na baadhi ya matukio yanayoendelea nchini,

Licha ya ahadi nyingi za viongozi wa serikali kulinda na kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari,  hali ni tofauti ikizingatiwa kuwa kauli za viongozi na sheria zilizopo zimeendelea kuminya uhuru wa wanahabari pale wanapoibua mambo yanagusa maslahi ya taifa.

Katika kipindi cha miaka miwili ya serikali ya awamu ya tano, yametokea baadhi ya matukio ikiwemo vitisho, kupigwa faini, kufungiwa vyombo vya habari na kuteswa na kutekwa kwa wanahabari. Matuki hayo ni tishio kwa mstakabali wa uhuru wa kujieleza nchini.

 

Kuvamiwa na kupigwa faini kwa runinga na redio

Machi 17, 2017 Ofisi za Clouds Media zilivamiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akiongozana na watu wapatao 4 wenye silaha ambapo aliwalazimisha waandaji wa kipindi cha SHILAWADU kurusha kipande cha video hewani kinyume na taratibu za habari. Uvamizi huo ulizua tafrani ikizingatiwa kuwa Mkuu huyo wa mkoa hakufuata taratibu za kuingia kwenye ofisi za Clouds zilizopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.

                Wanahabari wanahitaji uhuru zaidi kutekeleza majukumu yao

Januari 1, 2018, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilivitoza faini sh. Milioni 60 vituo vya runinga vya Star TV, Azam, Channel  Ten, EATV na ITV baada ya kutangaza habari ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kuhusu tamko la tathmini ya uchaguzi mdogo wa marudio wa kuchagua madiwani uliofanyika katika kata 43 kwenye mikoa 19 ya Tanzania  Novemba 24 mwaka jana.

Tathmini hiyo iliibua mambo mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya nguvu ya vyombo vya dola, matukio ya watu kutekwa na watu wasiojulikana, watu kupigwa, kujeruhiwa  kwa lengo la kuharibu na kuvuruga uchaguzi  na vilevile kuwatia hofu wapiga kura.

Lakini TCRA ilidai kuwa habari hiyo ilikuwa ya ‘kichochezi’, haikuwa na mizania wala kuzingatia maadili ya uandishi wa habari.

Baadhi ya redio ikiwemo Magic FM, Redio 5, Times FM, Clouds FM kwa nyakati tofauti zimekuwa zikionywa na kupewa adhabu kwa kile kinachotajwa kutangaza maudhui yasiyozingatia weledi na taaluma ya habari.

 

Vitisho na Kupotea kwa Wanahabari

Novemba 2017, Mwandishi wa habari kutoka Kampuni ya Mwananchi, Azory Gwanda, aliripotiwa kutekwa na watu wasiojulikana Mkoa wa Pwani na mpaka sasa hajulikani alipo. Inadhaniwa kuwa tukio la kutekwa kwake linahusiano na kuripoti kwa matukio ya mauaji ya raia katika eneo la Kibiti-Wilaya ya Mkurunga.

Disemba 21, 2016, mwandishi wa runinga ya ITV, Khalfan Liundi alikamatwa na kuwekwa mahabusu kwa amri ya aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti kwa kile kilichodaiwa ni kuripoti mgogoro wa maji katika Wilaya hiyo na kudai kuwa taarifa hiyo ilikuwa na harufu ya ‘uchochezi’.

Aprili 12, 2018, Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai aliiagiza Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge, kumuhoji mwanahabari Paschal Mayallah na wahariri wa gazeti la kila wiki, la Raia Mwema kwa madai ya kuchapisha habari iliyodaiwa kuchafua hadhi ya bunge, iliyotoka Aprili 9 mwaka huu.

Pascal aliandika habari yenye kichwa ‘Bunge linajipendekeza kwa serikali?’ ikiwa ni maoni yake juu ya nguvu ya bunge kuiwajibisha serikali pale inapokosea.

 

Kufungia magazeti

Mwaka 2017, Jumla ya magazeti 4 (Tanzania Daima, Raia Tanzania, Mawio na MwanaHalisi ) yalifungiwa na kulipishwa faini kwa sababu tofauti, ikiwemo chini ya sheria kandamizi ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, ambayo ina vifungu vyenye utata vinavyoweza kutumiwa vibaya.

Licha ya kufungiwa, baadhi ya magazeti yamekuwa yakipewa maonyo na vitisho pale yanapoandika habari nyeti zinazogusa maslahi ya ‘vigogo’ waliopo katika taasisi mbalimbali nchini.

Matukio yote haya dhidi ya vyombo vya habari yamekuwa yakienda sambamba na utekelezaji wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015, Sheria ya Upatikanaji wa Habari ya mwaka 2016 ambazo zote zimekuwa zikilalamikiwa kwa kuminya uhuru wa kujieleza nchini.

Sheria ya Upatikanaji wa Habari ya mwaka 2016 yalalamikiwa kuminya haki ya kupata taarifa

 

Sheria na kanuni za Maudhui Mtandaoni

Baada ya kupitisha Sheria ya Makosa ya Mtandao (The CyberCrime 2015), mwanzoni mwaka huu serikali  imekuja na Kanuni  za kusimamia Maudhui ya Mitandao ya Kijamii na Utangazaji wa vituo vya redio na runinga (TV)  ambapo kanuni hizi zinatajwa kama mkakati wa kuminya uhuru wa watu kujieleza na kupata taarifa.

Kanuni hizi zinawataka wamiliki wa runinga na redio za mtandaoni, blogu, majukwaa na tovuti za habari kupata kibali na leseni toka serikalini kabla ya kuendesha shughuli zao mtandaoni.

Kuna tetesi kuwa utungaji wa kanuni nyingine ya kulinda faragha na usalama wa  watumiaji iko mbioni kupitishwa.

Ikiwa hali iliyopo sasa haitabadilika wanahabari na vyombo vya habari nchini  hawana sababu ya kusheherekea Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani wakati bado hawafurahii uhuru wa kujieleza ambao unatambulika na Katiba ya mwaka 1977 na Sheria za Kimataifa.

              Watumiaji wa Mitandao ya kijamii Tanzania bado wako kitanzini

 

Maoni ya wadau

Akizungumza hivi karibuni katika uzinduzi wa Ripoti ya Haki za Binadamu-2017, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo Bisimba alishauri serikali kuzifanyia marekebisha sheria zote zinazokandamiza uhuru wa wanahabari ili wafanye kazi zao kwa uhuru bila kuingiliwa na mamlaka.

“Wizara ya Katiba na Sheria kuanzisha mchakato wa kupitia upya sheria zinazohusu uhuru wa kujieleza, hasa Sheria ya Huduma za Habari na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni na kupeleka muswada bungeni ambao utapeleka vifungu vyenye utata na vinavyokiuka haki za msingi virekebishwe au kuondolewa kabisa,” alisema Dk. Hellen.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, akitoa tamko la Umoja wa Mataifa (UN) amezitaka serikali duniani kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari ili vihabarishe ukweli uliopo katika jamii.

“Katika Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari 2018,  nazitaka serikali kuimarisha uhuruwa vyombo vya habari, na kuwalinda wanahabari. Kuhimiza vyombo huru vya habari ni kusimamia haki yetu ya kupata ukweli”, amesema.

Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari hufanyika Mei 3 ya kila mwaka ambapo wadau na wanahabari huitumia siku hiyo kutathmini mchango wa vyombo hivyo katika maendeleo ya nchi zao.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kuweka usawa wa madaraka: Vyombo vya Habari, Haki na Utawala wa Sheria”. Na kimataifa maaadhimisho hayo yanafanyika Accra, Ghana.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *