Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameitaka jamii kuunga mkono kampeni iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwasaidia wanawake wenye watoto ‘waliotelekezwa’ na waume zao.
Akizunguma leo wakati wa uzinduzi wa Chanzo ya saratani kwa wasichana katika viwanja vya Mbagala Zakhem, jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais amesema wanaume waliowazalisha wanawake hao kwa kupenda au bahati mbaya wanapaswa kutimiza wajibu wao wa kutoa matunzo kwa watoto wao.
Amesema zoezi lililoanzishwa na Mkuu wa Mkoa ni hatua nzuri ya kisheria kuwasaidia wanawake ambao wanakabiliwa na ukatili wa kijinsia ambapo mikoa mingine iige ili kuhakikisha wanawake na watoto wanapata haki zao za msingi ikiwemo matunzo.
“Mkuu wa mkoa nakupongeza, hatua hii itatupa takwimu zitakazotusaidia kufanya tafiti, pengine na mikoa mingine itafanya. Naomba baada ya hatua hii wakina mama hawa waelekezwe njia ya kufanya”, amesema Makamu wa Rais.
Ameongeza kuwa taasisi ya Ustawi wa Jamii inapaswa kushughulikia kesi zote za wanawake waliotelekezwa na amewataka watu wasibeze juhudi za Makonda kwasababu zinalenga kuondoa tatizo la malezi katika jamii.
“Taasisi nyingine zitoe ushirikiano, tukikosoa hatua hizi za awali tutakuwa hatusaidii jamii, maafisa wa maendeleo ya jamii wapo pale wayabebe yatakayokusanywa, watakaokubaliana yaishe wayamalize lakini yale yatakayopelekwa mahakamani yapelekwe”.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akizungumza na wanawake waliotelekezwa jana jijini Dar es Salaam.
Akizungumza awali katika viwanja hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameelezea kampeni hiyo sambamba na kutaja orodha ya wanaume waliozaa na wanawake hao ambapo inajumuisha viongozi wa dini na wabunge.
Kwa mujibu wa Makonda, wanawake 480 wanaodai kutelekezwa, waliofika jana katika ofisi yake kupata msaada wa kisheria, kati yao 47 wamesema wametelekezwa na wabunge na 14 wamedai kutelekezwa na viongozi wa dini.
“Wengine wamewataja wafanyabiashara mashuhuri ambao ukiwatazama huwezi kuamini kama wanafanya ukatili huu”, amesema.
Ameongeza kuwa mwaka 2017 pekee walizaliwa watoto 129,347 ambapo kati ya hao asilimia 60 walitelekezwa ambapo wengine wanalelewa katika vituo vya watoto yatima.
Ikumbukwe kuwa jana wanawake hao wanaodai kutelekezwa wakiwa na watoto wao walifika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kupata msaada ambapo tayari wameandikisha taarifa zao za msingi na kuwaandikia barua wanaume waliozaa nao ili wafike katika ofisi hiyo kwaajili ya hatua inayofuata.
Sheria inasemaje juu matunzo
Mila na desturi za Tanzania zinamtambua mwanaume kama kiongozi wa familia mwenye jukumu la kutoa matunzo kwa mke na watoto wake na kuhakikisha anatoa matumizi kama chakula, mavazi , matibabu, makazi na mahitaji ya msingi kama ada za shule, vifaa vya shule na kila kitu ambacho ni mahitaji ya msingi kwa makuzi na ustawi wa mtoto.
Kwa hiyo mzazi asiyejihusisha kwa namna yoyote na huduma hizi ambazo zinatambulika kisheria huyo ndiye aliyetelekeza familia au watoto.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu kifungu cha 166 kinasema kuwa mtu yeyote ambaye ni mzazi au mlezi au mtu mwingine mwenye uangalizi halali wa mtoto yeyote mwenye umri usiozidi miaka kumi na nne, hali ana uwezo wa kumuhudumia mtoto, kwa kuamua au kinyume cha sheria au bila ya sababu za msingi akakataa kumhudumia na akamtelekeza mtoto bila msaada, atakuwa ametenda kosa.
Mzazi akikataa kumhudumia na akamtelekeza mtoto bila msaada, atakuwa ametenda kosa.
Wadau wanena
Akizungumza na FikraPevu, Violeth Chonya kutoka Kituo Cha Usuluhishi (CRC), Chama Cha Wanawake Wanahabari Tanzania (TAMWA), amesema Makonda anapata nguvu ya kuratibu zoezi hilo kwasababu atalazimika kufanya kazi na wanasheria na watu kutoka ustawi wa jamii kuendesha kesi za utelekezaji watoto ili haki itendeke.
“Yeye anafanya kazi na watu wa Ustawi wa Jamii, dawati la jinsia na wanasheria, wote wanahusika na hizo kesi za child protection (kuwalinda watoto)”, amesema Violeth.
Akifafanua kuhusu umri sahihi wa mtoto kupata matunzo ya baba, amesema ni mtoto yeyote ambaye hajaanza kujitegemea na bado yupo kwenye uangalizi wa wazazi. Ameeleza kuwa wajibu wa kumtunza mtoto ni wa wazazi wote wawili na endapo mzazi mmoja hatawajibika anakuwa amefanya kosa kisheria.
“Mtoto ana haki ya kupata matunzo mpaka pale atakapoanza kujitegemea. Hata kama mtoto ana umri wa miaka 18 lakini hana uwezo kujitegemea wazazi wote wawili wanawajibika kumlea mtoto”, amesema na kuongeza kuwa,
“Hapo kuna Sheria ya Ustawi wa Jamii pamoja na Sheria ya Mtoto ya 2009 inafanya kazi kwasababu ukiangalia pia Sheria ya Ndoa inamwamuru kama baba kutunza familia. Sheria ya mtoto inasema mtoto ana haki ya kupata matunzo ya baba na mama. Sasa pale inapotokea upande mmoja hautekelezi hilo ni kosa kisheria”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJUKI), Janeth Mawinza amesema utelekezaji wa familia ni ukatili wa kijinsia kwasababu una mkosesha mtoto matunzo na haki ya kupata malezi ya wazazi wote wawili.
“Kesi nyingi tunazozipokea ni utelekezaji wa familia hili ndio limechukua nafasi kubwa zaidi lakini pia inafuatia na kesi hizo za ubakaji, vipigo na kesi za kisaikolojia”, amesema Janeth.
Amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutunza familia na kuishi kwa haki na usawa ili kuhakikisha jamii inapata maendeleo endelevu, “Tumefanikiwa kuwapa watu elimu na kuanza kujitambua na kuanza kupambana na ukatili huo wa kunyanyasa watoto”.
Serikali kupitia Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amekemea udhalilishwaji wa watoto ‘waliotelekezwa’ na baba zao ambao tangu jana picha zao zimekuwa zikisambazwa katika mitandao ya kijamii baada ya kufika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakiwa na mama zao.
Amewataka wanawake hao kufuata mifumo ya kisheria kupata msaada kwasababu jambo hilo ni nyeti na linahitaji uangalifu ili kulinda maslahi ya watoto kama Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inavyoelekeza.