Sakata la Mwenyekiti wa TSNP, Abdul Nondo lachukua sura mpya. Afikishwa Mahakamani Iringa, anyimwa dhamana

Jamii Africa
DAR: Viongozi wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania(TSNP) wameitwa kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai(DCI) kwa mahojiano - Hayo yamebainishwa kwenye taarifa iliyotolewa na Afisa Habari wa TSNP, Hellen Sisya ikiwa ni siku moja imepita tokea Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kutoa ripoti yao juu ya Abdul Nondo - Alisema kuwa “Tumepokea taarifa ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inatofautiana kabisa na ile ya Iringa juu ya kuonekana kwa Nondo” - Hellen ameendelea kwa kusema pamoja na mapungufu yote wanaamini Nondo atatendewa haki atakapofikishwa mahakamani

Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania (TSNP), Abdul Nondo aliyedaiwa ‘kujiteka’ amefikishwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa kujibu mashtaka mawili ya kutoa taarifa za uongo mtandaoni na kudanganywa kuwa alitekwa.

Kwa mujibu wa Wakili wa mwanafunzi huyo, Jebra Kambole amesema Nondo alisafirishwa usiku wa kuamkia leo kwenda Iringa na tayari amefikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili lakini hajapata dhamana.

Akisoma mashtaka yanayomkabili Nondo, Wakili wa serikali, Abeid Mwandalamo amesema shitaka la kwanza ni kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa Whatsapp akiwa eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam kwamba yupo hatarini ‘I’M AT HIGH RISK”.

Katika Shitaka la pili Nondo anadaiwa kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma wa Mafinga alipoenda kuripoti kwenye kituo cha Polisi cha Mafinga kuwa alitekwa na watu wasiojulikana Dar es Salaam na kusafirishwa hadi kwenye kiwanda cha Pareto Mafinga. Nondo amekana mashtaka yote wawili.

Abdul Nondo ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amenyimwa dhamana baada ya upande wa Jamhuri kuweka pingamizi la dhamana kwasababu za usalama wake wakieleza kuwa bado maisha yake yapo hatarini.

Akizungumza leo, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, John Mpitanjia amesema anaomba apatiwe muda wa kusoma sheria ili kujiridhisha ikiwa mshtakiwa akipewa dhamana maisha yake yatakuwa hatarini. Shauri hilo limeahirishwa na mtuhumiwa amepelekwa rumande.

 

Taarifa za awali

Mnamo Machi 6, 2018 Abdul Nondo alipotea katika mazingira ya kutatanisha na kupatikana siku iliyofuata Machi 7, 2018 mjini Mafinga, mkoani Iringa ambako alishikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kabla ya kurejeshwa Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi.

Taarifa za Nondo kupotea, zilikuja takribani wiki mbili baada ya mauaji ya Akwilina Akwiline, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa chuo cha usafirishaji cha taifa (NIT).

Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi “iliyorushwa na askari wa jeshi la polisi,” wakati jeshi hilo likidai kukabiliana na wafuasi Chadema, waliokuwa wanaelekea kwa msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kinondoni kushinikiza kupewa hati za viapo kwa mawakala wake kusimamia uchaguzi.

Nondo amekuwa mstari wa mbele kushinikiza baadhi ya viongozi wa Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani, akiwemo waziri wa wizara hiyo Mwigullu Nchemba, kuwajibika kwa mauaji ya mwanafunzi huyo na vitendo vya utekaji, kuteswa na kuuawa kwa raia wasio na hatia.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika vinasema Nondo aliripotiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha na alipatikana akiwa hai eneo la Mafinga mkoani Iringa. Alidai kuwa alijikuta katika eneo hilo baada ya kuzinduka kutoka katika lindi la usingizi na kuwauliza wenyeji wa eneo hilo mahali aliko.

Baadaye alijisalimisha kituo cha polisi Mafinga kabla ya kufikishwa Makao Makuu ya Polisi mkoani humo kwa mahojiano na kusafirishwa hadi jijini Dar es Salaam ambako aliendelea kushikiliwa na Jeshi hilo bila kufunguliwa mashtaka yoyote.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alikiri jeshi lake kumshikilia Nondo.

Mambosasa alisema Nondo hakuwa ametekwa, bali alikuwa akiendelea na shughuli zake za kawaida kwa kumtembelea mpenzi wake. “taarifa kuwa Abdul Nondo aliyedaiwa kupotea katika mazingira ya kutekwa, ulikuwa ni uzushi kwani hakutekwa isipokuwa alikuwa kwa mpenzi wake.”

Maelezo ya Mambosasa yalitofautiana na yale ya jeshi la polisi mkoani Iringa, kuwa “Nondo alifika kituoni hapo akiwa hajitambui”.

Hata hivyo, tangu akamatwe Abdul Nondo hajawahi kuzungumza na wakili wake wala vyombo vya habari jambo ambalo limekuwa likipingwa na watetezi wa haki za binadamu.

 

 Wanasheria wafungua kesi kumtetea

Tayari mawakili wa Nondo kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) wamewasilisha Mahakama Kuu maombi rasmi ya kutaka mwanafunzi huyo afikishwe mahakamani.

Katika kesi hiyo, washitakiwa ni Mkurugenzi wa mashitaka (DPP), Mwanasheria mkuu wa Serikali (AG) na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) walitakiwa kufika leo mahakamani hapo kujibu tuhuma hizo katika kesi ambayo imeanza kusikilizwa leo.

Akizungumza nje ya Mahakama hiyo baada ya kesi hiyo kuahirishwa, Wakili Jebra Kambole amesema, “Kimsingi Mahakama baada ya kusikiliza pande zote mbili katika hoja za awali imetoa amri zifuatazo; kwanza kabisa imetoa amri kwa mwanasheria wa serikali kuleta majibu tarehe 26/3/2018 lakini pia sisi 27/3/2018 tunatakiwa tulete majibu yetu.

Mahakama imesema baada ya hapo itasikiliza pande zote mbili 4/4/2018 kuangalia dhamana, lakini pia kuangalia haki yetu sisi kuweza kumuwakilisha Abdul Nondo lakini pia kutoa amri kwamba alikamatwa kihalali au umeshikiliwa kwa namna gani hapa katikati na kama sheria zilikiukwa kwa mujibu wa katiba ya nchi”.

Wakati kesi hiyo ikitajwa leo Mahakama Kuu, Nondo amerudishwa tena Iringa na kufunguliwa mashtaka mawili ya kutoa taarifa za uongo na kudai kuwa alitekwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *