“Scanning” Nyaraka za Uchaguzi kwachelewesha matokeo rasmi Igunga

Jamii Africa

Japo matokeo yote ambayo tumeyafuatilia yanaonesha kuwa Chama cha Mapinduzi kimeshinda uchaguzi wa Igunga hata hivyo Msimamizi wa Uchaguzi kwenye Jimbo hilo ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga bado hajatangaza matokeo hayo. Kutokana na taarifa kutoka Igunga ambazo FikraPevu imeweza kufuatilia na kuthibitisha kucheleweshwa kwa matokeo hayo kunatokana sana na utaratibu wa ujumlishaji wa matokeo hayo kutoka vituo mbalimbali.

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika toka Igunga kwenye kituo cha kukusanyia matokeo hayo ambapo ni makao makuu ya Halmashauri tatizo kubwa linalosababisha kuchelewesha matokeo ni utaratibu wa kunakili kwa mfumo wa kompyuta karatasi zote za matokeo, na kisha kuzijumlisha rasmi. Hadi hivi sasa haijulikani ni “scanners” ngapi zinatumika kwa ajili ya zoezi hilo. “Zoezi la ‘kuscan’ limeanza tangu jana jioni na limeendelea hadi hivi sasa na kwa mwendo ambao tunauona laweza kuendelea hadi kama hadi saa sita hivi ndipo matokeo rasmi yatakuwa yamejulikana rasmi” amesema mmoja wa wahusika wa zoezi hilo ambaye alikataa kutaja jina lake.

Kutokana na tume kuwahakikishia wananchi kabla ya uchaguzi kuwa matokeo yangetangazwa siku hiyo hiyo ya uchaguzi na hasa hisia kwamba labda kama kuchelewa ingekuwa hadi saa sita usiku kucheleweshwa huku kumezua hali ya wasiwasi na hisia ya “uchakachuaji”. Baadhi ya watu hata hivyo ambao wamefuatilia upigaji kura na ukusanyaji wa matokeo wametilia shaka baadhi ya taratibu zilizotumika kiasi kwamba mmoja wa waliozungumza nasi wamedokeza kuwa safari hii “uchakachuaji umeenda high tech” akimaanisha kwamba mbinu za kuchakachua upigaji kura zimetumia teknolojia ya kisasa.

Hata hivyo, mmoja wa maofisa wanaosimamia zoezi hilo amekanusha vikali suala hilo akidai kwamba “mchuano ni kweli ulikuwa mkali na chama chochote kingeweza kushinda na tofauti ndogo kati ya chama kilichoshinda na kinachofuatia ni dalili ya kazi ngumu ambayo vyama vilikuwa navyo”.Maneno hayo hata hivyo hayajatuliza watu ambao wameonekana kukatishwa tamaa na mfumo wa uchaguzi ambao unashindwa kutangaza mshindi kwenye jimbo moja lenye kata 26 tu na hivyo kutilia shaka uwezo wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa kuweza kuendesha uchaguzi wowote nchini kwa misingi ya haki na uhuru.

 

Na. M. M. Mwanakijiji

3 Comments
  • hata kama ccm wameshinda kwa tofauti hiyo y kura 4000 inadhihirisha wazi ushindani toka chadema na hii ni dalili njema kuwa tuendako mambo yatajuwa shwari. nimefuatilia kidogo kwa mjini chadema imepiga bao. hii inamanisha kuwa kila penye waelewa basi lazima chadema inashinda. kila penye jamii yenye kupata mwanga wa elimu utagundua chadema inapeta. nawapongeza hawa wapambanaji dhidi ya maovu na dhidi ya nguvu kubwa ya pesa waliyo nayo ccm. siku yaja watang’oka tu. tusikate tamaa ushindi unakaribia

  • Unajua kama uwezo wetu wa kutumia teknolojia ni mdogo basi watuajiri sisi tuwasaidie kujumlisha hzo kura..Kama tatizo sio hilo basi wanachakachua hapo hzi kura.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *