Serikali yaingilia kati sakata la kodi, kupanda bei mafuta ya kula nchini

Jamii Africa

Serikali imesema kinachofanya mafuta ya kula kuadimika katika baadhi ya maeneo nchini, ni kutokuwepo kwa makubaliano ya kodi na wafanyabiashara wanaoagiza mafuta hayo kutoka nje ya nchi.

Kauli ya serikali imekuja siku chache baada ya kuwepo kwa malalamiko ya kupanda kwa bei ya mafuta ya kula, kutokana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuzuia meli ya mafuta kushusha mzigo bandarini mpaka zilipe kodi kulingana na sheria mpya ya kodi iliyopitishwa Februari mwaka huu.

Utaratibu wa kodi uliopo wa kodi ni kwamba mafuta safi yanayoagizwa toka nje yanakatwa kodi ya asilimia 25 na mafuta ghafi (crude oil) hutozwa asilimia 10.

Akitoa ufafanuzi leo bungeni, Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema tatizo lilipo kuhusu kile kinachotajwa kuanza kuadimika kwa mafuta ya kula ni kutoelewana  kwa TRA na wafanyabiashara ambao wanataka watozwe asilimia 10 kwasababu mzigo wanaoingiza nchini ni mafuta ghafi.

Lakini kwa mujibu wa waziri Mwijage, vipimo vya Kamishna wa forodha katika bandari ya Dar es Salaam vilionyesha mafuta hayo yaliyozuiliwa tangu mwezi uliopita kuwa sio ghafi wala safi. Kutokana na msimamo huo wa idara ya forodha wanadai kodi inayotakiwa kulipwa ni asilimia 25 lakini wafanyabiashara walikataa.

“Kinacholeta tatizo ni kutokukubaliana katika viwango vya kodi. Ukileta mafuta kwa sheria tuliyopitisha sisi Tanzania kwa mafuta ghafi tunamtoza asilimia 10. Vipimo vilivyopimwa na kamishna wa customs (forodha) vinamuonyesha kwamba hii sio crude oil (mafuta ghafi) au finished oil (mafuta safi) ambayo inamuonyesha kamishana basi hivi ni mafuta safi anataka kutoza asilimia 25,” amesema Mwijage.

Kutokana na utata unaoendelea baina ya pande mbili, serikali imeingilia kati na inafanya mazungumzo na wahusika na itatoa tamko rasmi kesho.

“Serikali tumelichukua hili na wataalamu wa serikali watatoa majibu kati ya leo na kesho ili kujua hii ni crude au sio crude tuweke asilimia 10 au 25,” amebainisha Mwijage.

Hata hivyo amewatoa hofu wananchi kwamba bado nchi ina hazina ya kutosha ya mafuta ghafi ya kula  ya tani 90,000.

“Kwamba sasa hivi kwenye hifadhi ya matenki kuna takribani tani 40,000. Na meli  zilizoko nje zenye mafuta ghafi ya maweze takribani 50,000. Meli zilizoko nje na zilizoko ndani zina takribani tani 90,000,” amebainisha Mwijage na kuongeza kuwa,

“Lakini kama nilivyowaeleza tunayo hazina ya kutosha, crude oil tani 90,000 na kwahiyo katika mfungo ramadhani tutakwenda kufunga vizuri na kula vizuri vyakula vyetu vyenye mafuta ya kutosha .”

Waziri alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Nchemba, Juma Nkamia ambaye alitaka kujua ni hatua gani ambazo serikali inachukua kukabialiana uhaba wa mafuta ya kula nchini.

Mafuta ya kula hutumika zaidi kuongeza ladha kwenye chakula

Taarifa zilizopo kutoka Shirika la Viwango nchini (TBS) ambazo zilitolewa na Afisa mmoja ambaye alihojiwa na gazeti moja la kila siku, zinaeleza kuwa katika vipimo vyao, mafuta hayo ambayo yamezuiliwa ni ghafi na kwamba viongozi wa juu wajiridhishe kabla hawajafanya maamuzi ni kodi ipi itozwe.

Utafiti uliofanywa na Fikra Pevu  katika baadhi ya maduka ya Dar es Salaam, bei ya mafuta ya kula imepanda ambapo robo lita inauza sh. 1,000 kutoka bei ya awali ya 600 na nusu lita imepanda kutoka 1,000 hadi 1,600. Jijini Dodoma, ndo ya lita 20 inauzwa 70,000 kutoka 56,000. Na kule jijini Arusha, lita moja imepanda kutoka 35,000 hadi 4,000 na ndoo ya lita 10 imepanda kutoka 31,000 ya awali hadi 35,000.

 

Msamaha wa kodi ya Tende

Kwa upande mwingine serikali imesema inaangalia uwezekano wa kusamehe kodi inayotozwa kwenye tende inayotumika wakati wa mfungo wa Ramadhani.

“Suala la tende tuzungumza na waziri wa Fedha na kuna kikao tulikifanya juzi kwa sababu hakikuwepo katika sheria yetu tuliyopitisha baada ya kuona lile tangazo la nchi  jirani ndiyo likawa linazunguka, tutalipeleka ili tumshawishi ili katika kipindi hiki Bunge na nchi tuchume thawabu,” amesema Mwijage.

Mounekano wa tende zinazotumiwa wakati wa mfungo wa Ramadhani

Majibu hayo yalitokana na  mwongozo alioutoa, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) ambaye aliitaka Serikali kuondoa kodi ya tende katika mfungo wa Ramadhani ambao Waislamu kote duniani hufunga.

Akiwa leo bungeni, Bashe amedai: “Naomba kutumia kanuni ya 69 kama utaridhia ili angalau tuweze kuahirisha bunge angalau kwa dakika 30 tuweze kujadili jambo moja tu kwamba mwezi wa Ramadhani unakaribia na kama alivyoanza kusema Mheshimiwa Nkamia (Juma) bei ya mafuta ya kula imepanda, bei ya Sukari imepanda.

“Lakini Nchi zilizotuzunguka zimefuta kodi katika moja ya chakula ambacho huliwa sana mwezi wa Ramadhan na Waislamu na ni Sunna wakati wa kufuturu tende, kama utaridhia tuahirishe angalau kwa nusu saa Bunge lijadili tuweze kufanya azimio la kuitaka Serikali ifute kodi hiyo”.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *