Shinyanga: Mgodi wafungwa kwa Uharibifu wa Mazingira

David Azaria

Mkuu wa mkoa wa shinyanga Bwana Ally Rufunga ameufunga mgodi wa dhahabu wa KIMEG CO LTD uliopo katika kijiji cha mwakitolyo wilayani shinyanga kwa uharibifu wa mazingira hali inayodaiwa kuhatarisha afya za watu na viumbe wengine.

Mgodi huo umekuwa ukijihusisha na uchenjuaji wa madini ya dhahabu kwa kutumia sumu aina ya Cyanide,bila kufuata kanuni,taratibu na sheria za madini nchini pamoja na sheria ya matumizi ya sumu hiyo.

Mkuu huyo wa mkoa ametoa agizo hilo baada ya kutembelea mgodi huo na kujionea shughuli za uchenjuaji wa dhahabu kupitia sumu hiyo,katika mabaki ya udongo kutoka kwa wachimbaji wadogo.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, Mgodi huo umeshindwa kudhibiti maji yenye sumu ambayo yanaelekea katika mashamba ya watu pamoja na malisho ya mifugo,na kwamba mgodi huo utatakiwa kufanya tathimini ya mazingira tena kupitia ofisi yake.

Mkuu huyo wa mkoa alisema mgodi huo umefungwa kwa miezi miwili kuanzia wiki iliyopita kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa uhalali wa uwekezaji katika kijiji hicho na pia kufanya tathimini ya athari za mazingira katika eneo hilo.

IMG_5853

PICHA: Sehemu ya mchanga uliopo katika moja ya migodi ya uchenjuaji wa dhahabu inayotumia sumu ya Cyanide

Aliagiza uongozi wa Mazingira katika wilaya hiyo kufanya upembuzi yakinifu,ili kubaini kiwango cha uharibifu pamoja na idadi ya watu waliokumbwa na uharibifu huo,na kwamba endapo itabainika mgodi utapaswa kulipa fidia.

“Sheria za madini ziko wazi ,ambazo zilipaswa kufuatwa kabala ya uwekezaji huu,idara ya Mazingira na Madini ndio wahusika katika hili,nataka mshirikiane katika kuhakikisha kwamba jambo hili linafanyika kwa haraka sana….’’ Alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Hata hivyo msimamizi wa mgodi huo Bwana Theogene Zacharia alisema kuwa maji yenye sumu yanadhibitiwa kwenda katika mashamba ya wakazi wa eneo hilo, huku akikanusha kuwepo kwa uharibifu wa mazingira katika eneo hilo.

“Tumefuata taratibu zote zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria,lakini sisi hatuwezi kupingana na amri ya serikali,tunakubali wacha waje wafanye uchunguzi wao sisi tunasubiri majibu…’’ alisema Zacharia.

Kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga una madini ya dhahabu ambapo wachimbaji wadogo na wakati wanafanya shughuli za uchimbaji wa madini pia sio mbali na ziwa Victoria, hivyo kuwepo na tuhuma za uvujaji wa sumu hiyo kali, kunaweza kuhatarisha pia usalama wa wakazi wa ukanda wa Ziwa victoria.

Ukiacha Tanzania Ziwa Victoria pia inatumiwa na Nchi za Uganda na Kenya.

Kumekuwepo na matumizi makubwa ya Sumu aina ya Cyanide katika Mikoa ya kanda ya Ziwa na hasa katika Mkoa wa Geita,ambao unaonekana kuwa na migodi mingi ya uchimbaji wa dhahabu pamoja na uchenjuaji.

Kanda ya Ziwa Victoria ina jumla ya miradi ya uchenjuaji (Vat Leaching Plants) 37 ambapo Mkoa wa Geita unaongoza kwa kuwa na migodi 21,Mwanza 9, Mara 7).

“Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Kanuni zake imebainisha taratibu za kuzingatia,kwa mfanokanuni no. 8 ya  The Mining ( Environmental Protection for Small Scale Mining) inazuia mchimbaji mdogo kutumia kemikali ya sayanaidi kuchenjua madini pasipo kuruhusiwa na Mkaguzi Mkuu wa Migodi (CIM).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *