Serikali yafanikiwa kudhibiti utoroshaji wa Dhahabu

David Azaria

SERIKALI imesema imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti utoroshaji wa madini katika migodi mikubwa iliyopo hapa nchini baada ya kuweka mfumo madhubuti wa ukaguzi kwenye migodi hiyo.

Hata hivyo imekiri kwamba imekuwa na kazi ngumu kudhibiti utoroshaji wa madini yanayozalishwa na wachimbaji wadogo kutokana na kutokuwepo kwa mfumo mahsusi wa kudhibiti wafanyabiashara wasio waaminfu wanaonunua madini hayo na kuyatorosha kwenda nje ya nchi.

Hayo yamebainishwa Mkoani Geita na Kamishina Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa, Salim Salim wakati wa warsha iliyoandaliwa maalum kwa ajili ya maofisa usalama wa uwanja wa ndege wa Mwanza.

Warsha hiyo iliandaliwa na Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) maalum kwa ajili ya kutoa elimu kwa maofisa hao wa usalama ili waweze kuwa na uwezo wa kudhibiti utoroshaji wa madini kupitia viwanja vya ndege na katika mipaka ya nchi.

Salim alisema kwamba kwa kiasi kikubwa serikali kupitia TMAA imejitahidi kuweka mfumo ambao ni vigumu kwa migodi kutorosha madini kwa lengo la kukwepa kulipa mrabaha na kodi mbalimbali.

Alitoa mfano kwamba katika migodi yote serikali imeweka maofisa wakaguzi ambao wanakuwepo muda wote kushuhudia mchakato mzima wa uzalishaji wa madini hadi usafirishaji wake.

“Kwa jinsi ambavyo serikali imejipanga ni vigumu kwa migodi mikubwa kutorosha madini kwani kuna maofisa wanaokuwepo muda wote tangu uzalishaji hadi wakati wa kusafirisha kwenda nje ya nchi”alisema.

Aliongeza kwamba maofisa hao wa ukaguzi wa madini wamekuwa wakibadilishwa kila baada ya muda mfupi ili kuhakikisha hakuna hujuma zozote zinazoweza kufanywa dhidi ya serikali.

Hata hivyo Kamishina huyo Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa alisema kwamba serikali imekuwa na wakati mgumu kudhibiti utoroshaji wa madini yanayozalishwa na wachimbaji wadogo.

Kwa mujibu wa Salim, katika Kanda ya Ziwa pekee serikali imeweza kutoa jumla ya leseni 1600 kwa wachimbaji wadogo lakini wengi wao wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara kuuza madini kwa njia ya magendo na hivyo kuikosesha serikali mapato.

Kwa upande wake Bruno Mteta ambaye alikuwa amemwalikisha Ofisa Mtendaji Mkuu wa TMAA alisema kwamba kwa ujumla wachimbaji wadogo wamekuwa wakizalishaji tani 20 za dhahabu kwa mwaka lakini ni tani mbili tu ambazo zimekuwa zikilipiwa kodi na ushuru mbalimbali.

Awali akiwasilisha mada kuhusu Sheria ya Madini ya mwaka 2010, Meneja Mipango na Utafiti wa TMAA Julius Mosha alisema kwamba mtu binafsi atakayepatikana na kosa la kutorosha madini atatozwa faini ya shilingi milioni 10 papo hapo au kifungo cha miaka mitatu au adhabu zote kwa pamoja.

Aidha alisema kwamba kwa upande wa kampuni ambayo itabainika kutorosha madini nje ya nchi itatozwa faini ya shilingi milioni 50, na kwamba Kamishina wa Madini amepewa mamlaka ya kutaifisha madini hayo bila kujali thamani yake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *