MPANGO wa kuboresha elimu bora kwa watanzania unaonekana kukabiliwa na changamoto nyingi katika baadhi ya maeneo yenye mazingira magumu kama hali ilivyo katika shule ya msingi Darpori iliyopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.
Mwenyekiti wa kijiji cha Darpori Andason Haule anasema kijiji hicho chenye utajiri wa madini ya dhahabu kina watu karibu 10,000 kilianza rasmi mwaka 2004, kina karibu makabila yote 120 yaliopo nchini pamoja raia kutoka nchi jirani za Malawi na Msumbiji.
Kijiji cha Darpori kilichopo katika kata ya Tingi kinaundwa na vitongoji vinne ambavyo ni Songeapori,Lunyere,Tanzania One na Njarambe,kijiji kina shule moja ya msingi ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazochangia kushusha elimu kwa wanafunzi.
Andrew Kayuni ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Darpori anazitaja changamoto ambazo zinaikabili shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2002 ikiwa na jumla ya wanafunzi 143 kati yao wavulana 72 na wasichana71 kuwa ni pamoja na shule kuwa na vyumba vinne tu vya madarasa kati ya saba vinavyohitajika hali ambayo inasababisha darasa la tatu na nne pamoja na darasa la sita na la saba kusoma katika chumba kimoja.
“Mwalimu wa darasa la tatu akiingia wanafunzi wa darasa la nne wanabaki darasani kimya wakimsubiri mwalimu wao pia katika chumba cha darasa la saba mwalimu mmoja anapoingia anafundisha darasa linalohusika na wale ambao hawahusiki ingawa wapo darasani wanakuwa kimya hali hii inavuruga ratiba ya masomo na kuleta usumbufu mkubwa kwa wanafunzi na walimu katika ufundishaji’’,anasisitiza mwalimu Kayuni.
Picha inaonesha wanafunzi wa shule ya msingi Darpori wilayani Mbinga mkoani Ruvuma ambao wanakabiliwa na changamoto ya kutumia kitabu kimoja katika somo la Kiswahili kusoma darasa zima
Shule ya Darpori ina walimu watano tu kati ya mahitaji ya walimu wanane,walimu hawana choo pamoja na upungufu mkubwa wa samani za shule yakiwemo madawati hali ambayo inasababisha dawati moja kukalia watoto watano hadi sita badala ya dawati hilo kukaliwa na watoto wawili hadi watatu.
Changamoto nyingine ambayo inawadharirisha walimu katika shule hiyo ni familia mbili za walimu wenye familia ya watu 10 hadi 16 kuishi katika nyumba moja ya shule yenye vyumba viwili hali ambayo imesababisha walimu kuishi katika mazingira magumu ya kazi.
“Shule yetu ina nyumba mbili tu za walimu, nyumba hizi zina vyumba viwili pamoja na sebule,hapa shuleni kuna walimu watano,katika nyumba hizi mbili kila nyumba moja zinaishi familia mbili za watu kati ya 16 hadi 18,mwalimu mmoja hana nyumba amepanga katika nyumba za wachimba madini ambazo analipa pango kubwa tunaomba serikali isaidie kuleta fedha za ujenzi wa nyumba za walimu’’,alisema.
Ameiomba serikali kuwatazama kwa macho ya huruma walimu wote nchini ambao wanafanyakazi katika mazingira magumu kama ilivyo katika kijiji cha Darpori ambako mazingira na maisha ya walimu ni magumu hali ambayo inasababisha mishahara wanayopata kuishia kulipa nauli na kulala katika nyumba za wageni wakati wanafuatilia mishahara yao .
Anusiata Mbunda amefundisha katika shule ya msingi Darpori kwa miaka minne sasa, anasema kutokana na mazingira magumu ya kufundishia miaka miwili iliyopita alitamani kuacha kazi lakini anaendelea kuvumilia ili kuwasaidia watoto wa kijiji hicho ambao anasema wanahitaji elimu kama ilivyo kwa watoto wengine wanaoishi katika mazingira bora ya kujifunzia.
“Ndugu mwandishi umefanya vema kuja kututembelea na kuona matatizo yetu hebu fikiria kuna baadhi ya masomo hapa kitabu kimoja wanasoma darasa zima badala kusoma wanafunzi wawili, dawati moja wanakaa wanafunzi sita,chumba kimoja cha darasa yanasomea madarasa mawili kwa wakati mmoja katika mazingira kama haya kweli elimu bora itatolewa?’’,alihoji.
Shule ya msingi Darpori ina vitabu vichache vya kufundishia na kujifunzia kutokana na idadi ndogo ya wanafunzi wanaosoma wasiozidi 140 hali ambayo inasababisha kupata shilingi 7000 tu zinazotolewa na idara ya elimu katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga katika mpango wa kuboresha elimu yaani MEM kwa ajili ya ununuzi wa vitabu.
Godfrid Nchimbi ni mwalimu wa shule ya msingi Darpori anasisitiza kuwa maisha na mazingira ya kufundishia katika shule hiyo ni magumu kwa mfano wakati wa kwenda kuchukua mshahara wanatumia magari ya machimbo ya dhahabu ambapo wakati wa masika kutokana na ubovu wa barabara inawalazimu kuomba ruhusa ya wiki moja na kulipa nauli ni shilingi 80,000 umbali wa kilimeta 82.
Bidhaa na vyakula katika kijiji hiki cha machimbo ya dhahabu bei juu kwa mfano vocha ya simu ni shilingi 1500 badala ya 1000,soda shilingi 1500 hadi 2000,bei ya petroli ni kati ya shilingi 5000 hadi 8000 kwa lita moja walimu wenye pikipiki tunaingia gharama kubwa ya mafuta’’,alisema.
Pamoja na changamoto hizi mkuu huyo wa shule hiyo anasema kitaaluma shule inajitahidi kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya Taifa ya darasa la saba ambapo mwaka 2008 wanafunzi watano walifaulu kati yao wavulana watatu na wasichana wawili ,mwaka 2009 jumla ya wanafunzi saba walifaulu kati yao wavulana watatu na wasichana wanne na mwaka 2010 wanafunzi 12 walifaulu kati yao wavulana watano na wasichana saba.
Mwenyekiti wa kijiji cha Darpori Andason Haule amekiri kuwa mazingira ya shule hiyo hayaridhishi na kwamba baadhi ya changamoto zimeanza kutafutiwa ufumbuzi ikiwemo ufyatuaji wa matofali kwa ajili ya kuongeza vyumba vya madarasa,nyumba za walimu pamoja na kujenga choo cha walimu ambapo amesisitiza hadi kufikia mwezi Novemba mwaka huu wanatarajia vyumba vya madarasa vitakuwa vimekamilika.
Utafiti uliofanywa na UWAZI-TWAWEZA iliyopo HIVOS Tanzania Oktoba 2010 unaonesha kuwa Kadri shule inavyokuwa pembezoni zaidi kutoka makao makuu ya Halmashauri za vijijini ndiyo inavyokuwa na walimu wachache zaidi na vifaa vyenye ubora duni.