Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwighanji wakiwa wamelala baada ya kudondoka kutokana na mauzauza yaliyoikumba shule hiyo.
HALI ya watoto katika Shule ya Msingi Mwighanji, Tarafa ya Mgori wilayani Singida imekuwa ya taharuki kubwa baada ya kupatwa na ugonjwa wa kuanguka hovyo kwa muda miezi mitano sasa, FikraPevu inaripoti.
Taarifa kutoka shuleni hapo zimeeleza kwamba, hali hiyo ya mauzauza imezua sintofahamu kwa waalimu, wanafunzi na wazazi kwa ujumla.
FikraPevu imeelezwa kwamba, pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwighanji kuitisha vikao kadhaa kuzungumzia kadhia hiyo, bado hali imeendelea kuwa mbaya zaidi.
“Hali ni mbaya, yaani watoto wanaanguka hovyo, wanaweweseka utadhani wamepandisha maruhani, ni jana tu (Januari 24, 2017) baada ya mashekh wa kijijini hapo kwenda shuleni na kusoma dua, wanafunzi wengi waliendelea kuanguka, hali iliyomlazimu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo kuwaruhusu warudi makwao kabla ya muda,” alieleza mwananchi mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Inaelezwa kwamba, kumekuwa na mgawanyiko hata kwa wananchi wenyewe kuhusu suala hilo kutokana na baadhi yao kutupiana lawama za ushirikina.
Mmoja wa wanafunzi akiwalaza vyema wenzake waliodondoka ghafla.
Akiongea kwa huruma na masikitiko, Mwalimu Aloyce wa shule hiyo amesema hali hiyo imeathiri mahudhurio ya wanafunzi kwa kiasi kikubwa.
“Hali hii imetutia hofu hata sisi walimu, hatuna tena hamu ya kuendelea kufundisha katika shule hii kwani vitimbi vimekuwa vya muda mrefu na hakuna ufumbuzi wa haraka,” alisema.
Alisema mpaka sasa idadi ya wanafunzi wanaohudhuria masomo imepungua kutoka 800 hadi 300 kwa siku na kwamba hali bado ni mbaya na isipopatiwa ufumbuzi wa haraka shule inaweza kufungwa.
Mpaka sasa hakuna mbunge wala diwani aliyetembelea shule hiyo kujionea hali ilivyo na taarifa zinasema viongozi wa dini ya Kikristo nao wanajiandaa kwenda kufanya ibada shuleni hapo.