TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) sasa imenyoosha makucha yake michezoni kwa kuivalia njuga kashfa ya upangaji wa matokeo ya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya Simba na Yanga.
Jaribio hilo la kupanga matokeo lilifanyika siku chache kabla Simba na Yanga hazijakutana katika mechi ya mzunguko wa Kwanza Tanzania Bara iliyofanyika Oktoba 29, 2011 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katika mechi hiyo Yanga ilishinda 1-0.
Habari za uchunguzi zinaeleza kwamba tayari Takukuru imekwishawahoji watu kadhaa akiwemo kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa Simba (jina linahifadhiwa) na wachezaji wa Yanga, wiki iliyopita.
Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani, alithibitisha kuwa suala hilo lilikuwa mezani kwao ingawa hakutaka kuingia kwa undani kuhusiana na uchunguzi wao.
“Suala hilo lipo mikononi mwetu linafanyiwa kazi, upelelezi ukikamilika tutatoa tamko,” alisema.
Vyanzo vya habari vinaeleza kwamba upelelezi unamlenga zaidi kiongozi huyo wa Simba anayedaiwa kumpigia simu mshambuliaji wa Yanga, Pius Kisambale, siku chache kabla ya pambano lao wakati Yanga ikiwa kambini kwenye Hoteli Double Tree iliyoko Masaki, jijini Dar es Salaam.
Taarifa zinasema, wakati Kisambale anapigiwa simu alikuwa na baadhi ya viongozi wa Yanga na kwamba simu hiyo iliwashtua viongozi hao, hivyo kumfanya mchezaji huyo aongeze sauti ili nao wasikie kilichozungumzwa.
Shuhuda wa tukio hilo anaeleza kwamba mshambuliaji huyo alirekodi maneno ya kiongozi huyo mzito wa Simba, kitendo ambacho pia kilifanywa na viongozi waliokuwa wamemzingira.
Katika mazungumzo hayo, inaelezwa kwamba kiongozi huyo wa Simba alimtaka Kisambale acheze chini ya kiwango ikiwa atapangwa na kuahidi kumpatia ‘mzigo’ huku akimwomba awaeleze na wenzake juu ya mpango huo.
Hali hiyo inaelezwa kuwakasirisha viongozi wa Yanga walioamua kulipeleka suala hilo Takukuru ili mhusika achukuliwe hatua za kisheria.
Taarifa zaidi zinasema wiki iliyopita Takukuru ilimhoji Kisambale na wachezaji kadhaa wa Yanga katika ofisi yao iliyoko Upanga jijini dare s Salaam.
Mbali ya Kisambale, kiongozi huyo wa Simba pia amehojiwa na Takukuru kuhusu kashfa hiyo inayoonyesha kukubuhu kwa vitendo vya rushwa michezoni kiasi cha kuporomosha kandanda nchini.
“Rushwa imetawala michezoni na watu wanalichukulia kama shamba la bibi bila kujali namna kiwango cha michezo kinavyoporomoka. Sasa watu wamechoka,” kilisema chanzo hicho.
Kisambale aligoma kuzungumzia suala hilo na kusema hafamu chochote, huku Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwa akiruka kimanga na kusema hawezi kulizungumzia.
“Siwezi kuzungumzia,nendeni mkamuulize huyo kiongozi wa Simba mwenyewe, mambo haya yako kwenye vyombo vya sheria,” alisema.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa upelelezi umehusisha mawasiliano mbalimbali ya simu kati ya wachezaji wa Yanga na kigogo huyo wa Simba huku taarifa nyingine zikiongeza kwamba hata mawasiliano baina ya kiongozi huyo na baadhi ya waandishi wa habari za michezo nayo yanachunguzwa.
Mbali ya suala hilo, Takukuru pia inadaiwa kuchunguza kashfa inayomhusisha mshambuliaji wa Simba Ulimboka Mwakingwe aliyetaka kumhonga kipa wa zamani wa Mtibwa, Shabaan Kado katika msimu wa 2010/2011.
Ulimboka alikamatwa na walinzi wa kiwanda cha sukari Mtibwa akiwa na fedha zinazodaiwa zilikuwa rushwa kwenda kwa Kado ili aachie mabao katika mechi yao ya Ligi Kuu.
Vyanzo vya habari vinasema tayari Kado anayeidakia Yanga kwa sasa, amekwishahojiwa na Takukuru, ingawa mwenyewe amegoma kuzungumzia kilichoendelea kwenye mahojiano hayo.
Matokeo ya uchunguzi huo yanaweza
kubadili sura ya soka la Tanzania ambalo kwa miaka kadhaa limekumbwa na kashfa nyingi za rushwa, upangaji wa matokeo na uamuzi mbovu, hasa likizihusisha timu za Simba na Yanga.
Yeyote atakayepatikana na hatia anaweza kuadhibiwa kwa mujibu wa Kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), la Afrika (CAF) na la Dunia (FIFA).
Kanuni za FIFA katika vifungu (a), (b) na (c) zinabainisha kwamba mtuhimiwa akikutwa na hatia anaweza kufungiwa maisha, faini ya Sh17 milioni, au kutoruhusiwa kabisa kuingia katika uwanja wowote wa soka.
Taarifa za uchunguzi wa Takukuru zimekuja wiki chache tangu kocha wa Miembeni, Salum Bausi, ajiuzulu kwa madai kwamba mmiliki wake Ibrahim Makungu aliwashinikiza wachezaji waiachie Simba ishinde ili kuleta msisimko wa Kombe la Mapinduzi. Simba ilishinda kimizengwe mabao 4-3.
Viongozi wa Yanga – Julius Rutainurwa na Issa Makongoro – walifungiwa maisha ya CAF mwaka 1984 baada ya kutaka kuwahonga waamuzi kutoka Ethiopia waliokuja kuchezesha mechi ya raundi ya kwanza kati ya Yanga na Gor Mahia ya Kenya kwenye Klabu Bingwa Afrika.
Mnamo mwaka 2008, TFF iliwafungia maisha waamuzi Othmani Kazi, Omari Miyala na Omari Mfaume baada ya kubainika kupokea rushwa ya TSh. 200,000 ili kuibeba Majimaji katika mechi yake na Mtibwa.
Matukio ya rushwa kwenye soka:
1964: Kashfa kubwa ya uchezaji kamari kwenye soka iliibuliwa. Mtandao wa wachezaji kamari ulioongozwa na Jimmy Gauld uliwahusisha pia wachezaji kadhaa wa Ligi, wakiwemo wachezaji watatu wa Sheffield Wednesday, wakiwemo wawili wa timu ya taifa ya England, ambapo walifungiwa maisha baada ya kupanga matokeo katika mechi waliyoshinda dhidi ya Ipswich Town. Kashfa kama hiyo iliwahi kutokea mwaka 1915.
1994: Klabu ya Olympique Marseille ilikumbwa na kashfa ya upangaji matokeo kwa Olympique de Marseille inadaiwa kuwahonga wachezaji wa Valenciennes, Jacques Glassmann, Jorge Burruchaga na Christophe Robert ili wacheze chini ya kiwango katika msimu wa 1992-1993.
Marseille ilivuliwa ubingwa wa Ulaya, ubingwa wa Ufaransa ikanyimwa nafasi ya kushiriki Klabu Bingwa Ulaya, Kombe la Super na Klabu Bingwa ya Dunia pamoja na kushushwa daraja. Rais wake Bernard Tapie alikutwa na hatia na kufungwa jela miaka miwili.
Februari 1999: Mtandao wa wacheza kamari wa Malaysia ulinaswa ukijaribu kufunga kifaa chenye kutumia remote ili kuharibu na kuzima taa katika Uwanja wa klabu ya Charlton Athletic iliyokuwa Ligi Kuu baada ya kumhonga ofisa mmoja wa usalama wa uwanja huo.
Kama mechi ingevunjika wakati wa mapumziko, basi matokeo ya mchezo pamoja nay ale waliyoweka wacheza kamari yangesimama sawia.
Genge hilo ndilo lililohusika katika tukio la kuzima kwa taa kwenye Uwanja wa West Ham mwaka 1997, na baadaye katika Uwanja wa Crystal Palace wakati wa mechi na Wimbledon.