Tiketi ya Taifa Stars kwenda fainali Kenya 2018 iko Rwanda

Jamii Africa

KUFUZU ama kutokufuzu kwa Taifa Stars kwa fainali za Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (Kombe la CHAN) kutajulikana leo wakati timu hiyo itakapomenyana na Rwanda katika mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza.

Ingawa bado kuna raundi moja kabla ya kufuzu kwa michuano hiyo itakayofanyika nchini Kenya 2018, lakini tiketi halisi ya Taifa Stars iko mikononi mwa Amavubi ambapo inatakiwa kushinda mechi hiyo kwenye Uwanja wa Nyamirambo jijini Kigali.

Kenya imepata uenyeji wa fainali hizo kwa mara ya kwanza baada ya maombi ya muda mrefu, ambapo uamuzi ulitolewa Juni 27, 2017 na fainali hizo zitachezwa kuanzia Januari 11 hadi Februari 2, 2018.

Hii ni mara ya saba kwa Tanzania kukutana na Rwanda ambapo imeshinda mechi moja tu, kutoka sare mbili na kufungwa mechi nne.

Mechi ya leo ni ngumu kwa Tanzania ambayo haitegemei miujiza bali uhalisia wa ushindi, kwani wenyeji wao Rwanda wana faida ya bao la ugenini walilolipata katika mechi ya kwanza iliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza Julai 15, 2017.

Rwanda wenyewe wanahitaji sare ya aina yoyote ile ili kusonga mbele katika raundi ya pili.

Mshindi wa jumla baina ya Stars na Amavubi atapambana na Uganda au Sudan Kusini, ambazo zinacheza leo kwenye Uwanja wa Nakivubo jijini Kampala huku kila moja ikisaka ushindi.

Ingawa Kocha Mkuu wa Stars, Salum Mayanga, amehidi ushindi katika mchezo huo, lakini jitihada zinapaswa kuimarishwa kwa kikosi chake dhidi ya Rwanda ambayo imepania siyo tu kufuzu, bali hata kulinyakua taji hilo maridhawa.

Kwa upande mwingine, Uganda iko katika wakati mgumu wa kusonga mbele na inahitaji ushindi dhidi ya Sudan Kusini katika mechi ya marudiano itakayofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Nakivubo jijini Kampala baada ya timu hizo kutoka suluhu mchezo wa kwanza.

Uganda Cranes ambayo inanolewa na Milutin Sredojevic ‘Micho’, Mserbia ambaye amekuwa ‘Mswahili’ kwa kuzamia kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa miaka mingi, inatakiwa kujipanga vyema ili iweze kusonga mbele.

Lakini timu ya Sudan Kusini, maarufu kama Bright Stars, inayonolewa na Felix Komoyangi imejipanga vyema licha ya kushindwa kupata ushindi wa nyumbani.

Zambia inapalilia ushindi wake wa mabao 4-0 dhidi ya Swaziland ilioupata ugenini Jumamosi iliyopita, ambapo inahitaji sare tu ili iweze kusonga mbele.

Kocha wa Zambia, Wedson Nyirenda, amesema pamoja na ushindi walioupata, lakini hawatafanya makosa katika mechi ya marudiano kwa kuwa Waswazi hawatabiriki.

Kocha wa Isihlangu Semnikati kama timu ya taifa ya Swaziland inavyoitwa, Pieter De Jongh, ana wakati mgumu wa kuhakikisha vijana wake wanafanya vyema mjini Lusaka.

Matokeo ya mechi zilizopita ni kama yafuatayo:

Julai 15,2017: Sierra Leone 1 – 1 Senegal; Gambia 0 – 0 Mali; Guinea-Bissau 1 – 3 Guinea; Botswana 0 – 2 Afrika Kusini; Tanzania 1 – 1 Rwanda; Comoros 2 – 0 Lesotho; na Djibouti 1 – 5 Ethiopia.

Julai 16, 2017: Liberia 0 – 2 Mauritania; Togo 1 – 1 Benin; Namibia 1 – 0 Zimbabwe; Swaziland 0 – 4 Zambia; Madagascar 2 – 2 Msumbiji; Mauritius 0 – 1 Angola.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *