Urembo siku hizi ni mtaji au daraja la kupata mambo mengi maishani. Ukishabikia sana kujenga tabia njema ukasahau kuboresha urembo basi unaweza kupitwa na fursa mbalimbali ikiwemo uchumba na ndoa. Sijawahi kusikia mwanaume akifanya “waxing ya ndevu” aumie kwa ajili ya kuwa soft ili ndevu zisimkwaruze mwanamke…! Amkeni!
Misemo imesheheni siku hizi utasikia “Mwanamke urembo”!
Hivi uzuri au urembo wa mwanamke wa kiafrika siku hizi ni nini? Wahenga walikuwa na usemi “Uzuri wa mwanamke siyo sura au urembo bali ni tabia njema”. Methali hii sina hakika kama bado inabeba maana yoyote kwa sababu kila mwanamke anahangaikia sana urembo na katika mahangaiko hayo huweza kujikuta akisahau kutunza tabia njema. Kwanini hali imekuwa hivyo, ni swali la kujiuliza.
Urembo siku hizi ni mtaji au daraja la kupata mambo mengi maishani. Ukishabikia sana kujenga tabia njema ukasahau kuboresha urembo basi unaweza kupitwa na fursa mbalimbali ikiwemo uchumba na ndoa. Hata hivyo kwa miaka ya siku hizi watu watakuambia uzuri na urembo siyo lazima uzaliwe navyo bali waweza kununua dukani! Hebu tafakari ndugu msomaji na ujiulize nini kimeleta mabadiliko haya kwa kasi ya ajabu? Inatubidi turudi nyuma kidogo tuangalie urembo wa asili na ule wa dukani ili tuweze kujua hizi mbio za kukimbilia kununua urembo zina maana au ni kupoteza pesa na muda tu?
Hakuna mjadala kwamba, tangu zamani za kale, urembo ulitawala kila kitu cha mwanamke kuanzia nywele, shingo, kifua na matiti, kiuno, nyonga na makalio hadi miguu. Hatuwezi kusahau mikono na kucha zake na hata rangi na wororo wa ngozi. Pia tunaweza kusema kwa uhakika kwamba kila kiungo cha mwanamke kina sifa zake kwa vigezo vya urembo wa kiafrika.
Vigezo vya kiafrika vyakinzana na vya kimamboleo?
Nywele – Kwa asili, waafrika wengi wana nywele kipilipili lakini wako pia wenye nywele za kuteleza, zinazoweza kufananishwa na singa, zisiofungamana kwa mafundo. Nywele husukwa mitindo ya aina mbalimbali, hupakwa mafuta na kuzifanya ziwe laini. Kusuka kuna faida kadhaa kwa nywele za kiafrika. Kwanza ni kurefusha nywele na pili ni kumfanya mwanamke aonekane mrembo na mtanashati na mlimbwende. Makabila mengi yalikuwa na utamaduni wa kurembesha nywele kwa mitindo mbalimbali kama “mabutu” au “vitunguu”“twende kilioni” au “utii wa Roda”, “jicho la mke-mwenza”, Kilimanjaro” n.k Ukiacha sifa ya urembo, nywele zilikuwa na nafasi ya pekee katika makabila na mila mbalimbali na ziliweza kuashiria mambo mbalimbali. Mathalani, kunyoa nywele kuliweza kuashiria msiba au tukio baya.
Siku hizi, wanawake wa kiafrika hubadilishwa nywele kwa kusuka nywele za mitindo ya “rasta” “dreadlocks”, “weave-on”n.k. Mitindo hii huchanganya ‘nywele’ za bandia katika nywele za asili na kuzifanya zionekane ndefu na nyororo na huweza kubadilishwa mitindo katika ufungaji. Wanawake huweza kubadilisha kabisa muonekano wa nywele zao za asili kwa kuweka dawa na kuzifanya zilainike na hata kuzibadili rangi. Urembo wa asili polepole unapotea kwa vile kipimo cha uzuri wa nywele kimebadilika na kuakisi umagharibi zaidi. Nywele fupi za kipilipili mara nyingi hazionekani maridadi. Aidha, wanasema kwamba toka waanze kutumia virembesho vya nywele vya namna hii, wanajikuta polepole wakikosa uthubutu wa kukaa na nywele zao za asili, na pale wanapokuwa na nywele asili, hawajiamini mbele za watu! Wanajiona kama wako tofauti sana na watu wengine.
Tukija kwenye kifua na matiti, wanawake wa kiafrika kwa asili walichukulia matiti kama chakula cha mtoto na wasichana walipoanza kubalehe na kuota matiti, hayakufichwa kama tunavyoona siku hizi. Katika makabila mengi ya kiafrika matiti ya mwanamke hayakupewa uzito saaana katika urembo kwa vile umuhimu wake ulielekezwa zaidi kwa watoto watakozaliwa. Kitendo cha kunyonyesha ni ushahidi tosha kuwa matiti hayakuwa kitu cha kumfanya mwanamke aonekane “sexy”. Mwanamke aliweza kuvuta ziwa mbele ya mtu yeyote hata baba yake mzazi na kuanza kunyonyesha tena kwa kujiamini sana na kila mtu aliona ni sawa kabisa. Kama matiti yalikuwa na nafasi katika urembo, basi sifa hiyo ilikuwa ya faragha baina ya wapenzi au wana ndoa na haikuzungumziwa waziwazi.
Siku hizi wanawake wanajikuta wakihangaika sana na matiti yao kwa vile yanahusishwa zaidi na urembo na siyo chakula cha watoto! Wako wanawake wanaokataa kunyonyesha kwa vile ati matiti yao yatachakaa na kuwa kandambili. Uvaaji wa mavazi ya kuacha kifua wazi, na kuvaa sidiria za kunyanyua maziwa kote kunatokana na dhana ya kuhusisha urembo na matiti yaliyosimama na kujaa vizuri. Matiti yaliyolala, kusinyaa au kuanguka hayana nafasi katika mitindo au urembo. Hatuwezi kushangaa pale tunapoona wanawake wakihangaika kutafuta vitu vinavyosadikiwa kurudisha matiti katika hali ile ya “usichana”- matiti yaliyokaa mishale ya saa sita mchana! Kipimo cha uzuri hapa kinawekwa na “wanufaika” ambao siyo watoto wanaohitaji kunyonyeshwa kwa lishe, bali wale wanaofaika kwa kuangalia, kutomasa na hata kunyonya kwa starehe!
Kipindi fulani tulisoma kwenye magazeti na mitandao mbalimbali na hata kuona picha kuhusu mashine ya kichina ya kunyanyua matiti. Mashine hiyo hufanya kazi kwa kutumia umeme na kuvuta kwa vacuum. Zoezi hilo linaloenda kwa gharama ya sh 150,000/= linamtaka mwanamke kuhudhuria huduma hiyo kwa wiki kadhaa ili kupata matokeo yanayotakiwa. Siwezi kujadili zaidi kuhusu chombo hiki ila ninachojua ni kwamba kuvutwa matiti huwa kunauma sana. Sipati picha hawa akina dada wanaohudhuria ‘matibabu’ hayo ya kunyanyua matiti kama wanajali kujua madhara ya kifaa hicho na kama zoezi hilo linafanikiwa kwa kiwango gani ili wapige hesabu kuona kama wanapata faida ya pesa wanayotoa (value for money) maana siku hizi mtu makini hutaka kujua kama kapata thamani ya pesa yake anayotoa.
Kiuno nacho hakina budi kiwe chembamba kilichobeba makalio ya kuweza kumfanya mwanamke akitembea basi ajisikie anaringa kwa kunesanesa. Sina uhakika kama kwa asili makalio makubwa ilikuwa ni ‘ishu’ kwenye urembo kwa maana ya kiafrika, wanawake walijaliwa kuwa na miili iliyojaa hasa kwa mwanamke aliyekwisha kupevuka na hata kuzaa. Mwanamke wa kiafrika “Miss Bantu” kwa sifa ana makalio makubwa na miguu minene kiasi akivaa kitenge au mavazi ya kiafrika basi huweza kuwa na mvuto wa aina yake.
Umbo lililojaa hasa kuanzia nyonga na kushuka ndicho kilikuwa kipimo cha urembo! Wanawake hawakujali sana kuwa wembamba na wembamba haukuwa kipimo cha uzuri au urembo wa kiafrika. Kwa kipimo cha kisasa, urembo wa mwanamke umekuwa kwenye misukosuko kiasi ambacho imekuwa vigumu kujua urembo hasa ni upi. Wengine watakuambia vigezo vya “Miss Tanzania/Miss World” vyenye kulenga wembamba na urefu ndio kipimo cha kisasa cha mwanamke mrembo. Hapo mdada hutafuta kujikondesha kwa mazoezi, kujinyima chakula na hata kujitapisha! Wakiwa wajawazito hata chakula hawali kisa wanaogopa watanenepa. Kiafrika ujauzito na uzazi ni kipindi mwanamke alitunzwa kwa milo minono na kunenepeshwa ili akitoka awe amenenepa sana na kuiletea familia hasa mume heshima na sifa! Sasa siku hizi kujikondesha huku sijui kama ni sifa kwa mume au mzazi loh!
Wanawake wako njia panda kwenye vipimo hivi. Wanawake wanatafuta kuwa na makalio makubwa kwa vile wanasikia wanaume wanapenda makalio yaliyojaa, na sina uhakika kama kipimo hiki ni cha kimataifa! Utasikia “Ona kalio la kichina hilo” wakimaanisha mwanamke mwenye makalio makubwa na inasadikiwa wachina wameleta dawa za kuongeza ukubwa wa makalio. Waganga wa jadi nao hawajarudi nyuma katika kujipatia chochote kutokana na huu mkanganyiko wa urembo. Matangazo katika mabango barabarani na magazetini yanawavuta wanawake waende wakapate huduma ya kuongeza makalio na “hips”. Sijui kama uganga huu ulikuwepo toka zamani za kale kusaidia wanawake kwenye urembo ya asili.
Nijuavyo, vipodozi vya asili kama hina, liwa, msandali havikuwa dawa za kienyeji bali vilitokana na mazao na miti iliyoweza kuchumwa na mrembo mwenyewe bila kuhitaji mganga. Kuna wakati suala hili lililetwa hata kwenye vyombo vya juu kama watunga sera na sheria kujaribu kupiga marufuku lakini sijui iliishia wapi. Marufuku hizi zimewahi kuelekezwa kwa vipodozi vya kufanya ngozi iwe nyeupe al-maarufu kama mkorogo. Wataalamu wamejaribu kuiliongelea suala hili kwa kirefu sana na kuonyesha madhara yake. Aidha sheria zimewekwa kupiga marufuku baadhi ya vipodozi na hata kufanya msako madukani na kuwaadhibu wafanya biashara wanaoagiza mali hizo lakini juhudi hizi hazijazaamatunda hata kidogo.
Urembo wako ni kwa faida yako?
Wazungu wana methali isemayo “beauty is in the eyes of the beholder” wakimaanisha uzuri wa mtu uko kwenye macho ya yule anayeuona. Sasa, huu urembo mwenye kuuona ni nani? Je, ni mwenyewe mhusika kwa maana ya “mrembo mwenyewe” au ni wale wanaomuona? Wenye kumuona ni wengi na kila mtu ana haki kuamua kama anachokiona machoni mwake ni “urembo” au “uzuri” au ni nini. Ninajiuliza, ”Hivi nitajali nini kama wewe unayenitazama utahukumu kuwa mimi siyo mrembo?”. Mpita njia ana haki gani kuniamulia? Wanawake wengi watakuambia, mwanamke unatakiwa uonekane mrembo kwa wenzio na hasa wale wa jinsi tofauti. Hapo kwenye “jinsi” tofauti inabidi tupapigie msatari kwa maana pana kitu kikubwa sana chenye kupelekesha wanawake wahangaike sana kuusaka urembo na uzuri. Katika pita pita yangu nimebahatika kuongea na wanaume kutaka kujua mwanamke mrembo ni yupi na haya yalikuwa ni baadhi ya majibu:
..”Mimi napenda sana mwanamke awe na urembo wa asili – asitumie madawa ya ngozi au nywele”
..”Inategemea… kwangu mimi napenda sana mwanamke mwenye umbo la wastani, asiwe mrefu sana …awe na umbo litakalonifanya nimmudu… (Portable)”
…”sipendi mwanamke mwembamba hata kidogo. Nataka nisikie nyama na siyo mifupa”
“Napenda mwanamke mrefu mwembamba bana…. Huniambii kitu! Minyama uzembe inani put off vibaya sana…”
..”mwanamke mweupe ni ugonjwa wangu”
Hayo ni baadhi ya majibu ya wanaume niliowauliza. Majibu yao yanaashiria mchanganyiko wa tafsiri ya urembo na haya ndio huwachanganya wanawake. Wanawake wako katika mbio za kuwafurahisha wanaume zaidi ya kujifurahisha wao wenyewe. Cha ajabu hapo, hakuna mwanaume aliyezungumzia tabia njema, ikimaanisha tabia njema au mbaya haibadili chochocte kwenye urembo wa mwanamke.
Wakina dada na wakinamama, kwanini hamfanyi vitu kwa kujifurahisha wenyewe? Wanaume wanaposhinda saloon kunyoa na kufanya scrub hawafanyi kwa ajili yenu bali kwa starehe zao. Mijadala kuhusu wanaume na salon inaonyesha kabisa kuwa wanafanya kujifurahisha na kujipendezesha wao. Sijawahi kusikia mwanaume akifanya “waxing ya ndevu” aumie kwa ajili ya kuwa soft ili ndevu zisimkwaruze mwanamke…! Amkeni!
Mamlaka husika sijui kama mna habari kuhusu hizi teknolojia mpya za kichina… Tungependa kujua kama TFDA, TBS, na nyinginezo mmethibitisha viwango na ubora wa vifaa hivi.
Kiukweli mimi niko allergic na mwanamke ambaye anaonekana kiasili zaidi. Hatumii ma-artificial material.
Most mwanawake wanahita kupendeza kwahiyo waache wapendeze kwani bila wao tusinge mpata mrembo wa Africa yani namanisha Miss Africa na pia mwanamke ni kama maua anapaswa kupendeza kila mda kama pambo fulani ndani ya nyumba
Mambo yote hayo ni Pale mtu anapokosa kujiamini anaanza kutafuta vitu ambavyo nivya kubadilisha umbile na rangi yake ya asili aliyopewa na Mungu.
hello