Tahadhari ya Maafa kutokana na mvua za Masika (Machi-Mei 2012)

Jamii Africa

Serikali inawakumbusha wananchi wanaoishi mabondeni kuhama mara moja kutoka kwenye maeneo hayo hatarishi na kwenda kwenye maeneo salama ili kujikinga na maafa yanayoweza kusababishwa na mafuriko au maporomoko ya udongo. Tahadhari hii ya Serikali inasisitiza Taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) iliyotolewa hivi karibuni kuhusu mwelekeo wa mvua za masika zilizoanza mwezi huu wa Machi 2012.

KUMBUKUMBU ya mafuriko ya Disemba 2011, jijini Dar es Salaam

 Ili kuzuia au kupunguza athari za maafa yanayoweza kusababishwa na mvua hizo zitakazoendelea hadi mwezi Mei, 2012, mambo yafuatayo yazingatiwe:-

     i.        Mamlaka za Miji zihakikishe kuwa mifumo ya maji taka inasafishwa ili kuepusha kutuama kwa maji na hatimaye  kusababisha mafuriko.

ii.        Watoto wazuiwe kucheza katika mitaro ya maji ili kuwaepusha kusombwa na maji na vile vile kupata magonjwa. Ni muhimu wananchi kusikiliza, kufuatilia na kutekeleza ushauri wa kitaalamu unaotolewa mara kwa mara na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kupitia vyombo vya habari.

iii.        Kamati za Menejimenti za Maafa katika ngazi  za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji zihakikishe kuwa zinachukua hatua za kujiandaa na maafa yanayoweza kusababishwa na mafuriko, upepo mkali, maporomoko ya udongo au magonjwa ya milipuko.  Aidha, ziandae mipango mbadala ya kukabili maafa hayo.

iv.        Mamlaka za Majiji, Manispaa, Miji, Mikoa na Wilaya zitenge maeneo maalumu ya kuhifadhia watu endapo watakumbwa na maafa yatakayowasababishia kukosa makazi.

v.        Hospitali na zahanati zijiandae kukabiliana na magonjwa ya milipuko kama vile; kipindupindu, malaria, homa ya matumbo.  Aidha, wataalamu wa mifugo nao wajiandaae kukabiliana na magonjwa ya milipuko ya mifugo yanayoweza kutokea.

vi.        Tahadhari zichukuliwe katika maeneo ya migodi hasa ile ya wachimbaji wadogo wadogo, kuhakikisha kuwa maji hayaingii kwenye migodi hiyo.

Wafugaji wanashauriwa kuvuna na kuhifadhi malisho kwa matumizi ya wakati wa kiangazi. Aidha, wanashauriwa kuzingatia na kutekeleza ushauri unaotolewa na Maafisa Mifugo katika maeneo.

Wakulima wanashauriwa kuendelea kufuata na kupata ushauri wa Maafisa Ugani katika maeneo yao kwani mvua hizi zikitumika vizuri zinaweza kuleta faida kwa jamii na taifa kwa ujumla. Aidha, wachukue tahadhari kuhifadhi na kutumia chakula kwa uangalifu.

 

Peniel Lyimo

KATIBU MKUU

OFISI YA WAZIRI MKUU

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *