Taifa Stars ‘yanyolewa kwa wembe butu’, safari ya Kenya 2018 yachina

Jamii Africa

TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeendelea kudhihirisha kauli ya Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ally Hassan Mwinyi, kwamba ni ‘kichwa cha mwendawazimu’ baada ya ‘kunyolewa kwa wembe butu’ na Rwanda Jumamosi, Julai 22, 2017.

Baadhi ya mashabiki wanajifariji kuwa, Stars haijafungwa na Rwanda katika mechi mbili, lakini ukweli kwamba imetolewa katika kinyang’anyiro cha kusaka tiketi ya kucheza kwa mara ya pili fainali za Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (Kombe la CHAN) unadhihirisha kuwa Tanzania ina safari ndefu ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.

Timu hiyo ililazimisha kwenda suluhu na wenyeji Amavubi kwenye Uwanja wa Stade Regionale Nyamirambo jijini Kigali na kuwapa fursa Rwanda kusonga mbele katika raundi ya tatu kwa faida ya bao la ugenini kufuatia sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza Julai 15, 2017.

Matumaini ya Watanzania mamia kwa maelfu kwenda kuishangilia timu hiyo na kushuhudia fainali za Kombe la CHAN 2018 katika nchi jirani ya Kenya yameota mbawa kwa mara nyingine na inahitajika miujiza kama enzi za kocha Mbrazili Marcio Maximo ambaye aliipeleka kwenye fainali hizo kwa mara ya kwanza mwaka 2009.

Fainali za Kombe la CHAN zitachezwa nchini Kenya kuanzia Januari 11 hadi Februari 2, 2018 katika viwanja vya Nyayo na Moi Kasarani jijini Nairobi, Uwanja wa Manispaa mjini Mombasa na Uwanja wa Kinoru mjini Kisumu.

Timu hiyo sasa inabidi isubiri fainali za mwaka 2020 na kwa sasa inapaswa kujipanga kwa ajili ya kuwania tiketi ya kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2019.

Wakati Stars ikifungashiwa virago, Uganda na Rwanda zimefuzu kwa raundi ya tatu ambapo zitamenyana katika mechi ya kwanza Agosti 11, 2017.

Uganda imefuzu hatua hiyo baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Sudan Kusini katika mechi ya marudiano kwenye Uwanja wa Nakivubo jijini Kampala. Mechi ya kwanza baina yao ilikwisha kwa suluhu.

Burundi, ambayo awali ilikuwa imefurahia kusonga mbele kabla ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) halijaondoa adhabu ya kifungo kwa Sudan, ndoto zake zinaweza kutindikiwa hasa baada ya leo Jumapili Julai 23, 2017 kulazimishwa suluhu na Sudan katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Prince Louis Rwagasore.

Timu hizo zitarudiana Julai 28, 2017 kwenye Uwanja wa Khartoum na mshindi baina yao atamenyana na Ethiopia katika raundi ya tatu.

Ethiopia imesonga mbele kwa jumla ya mabao 8-1 dhidi ya Djibouti. Haikupata shida kwenye raundi hiyo baada ya Djibouti kujitoa hivyo Ethiopia, ambayo ilikuwa imeshinda mechi ya kwanza 5-1, ikapewa ushindi wa chee wa mabao 3-0.

Kuyaaga mashindano hayo, Tanzania ‘imeungwa mkono’ na Lesotho, Msumbiji na Zimbabwe ambazo zimeshindwa kufurukuta mbele ya Comoro, Madagascar na Namibia.

Ndoto za Zimbabwe zimetoweka leo Jumapili, Julai 23, 2017 baada ya kutolewa kwa mikwaju ya penalty 5-4 na Namibia kufuatia matokeo ya jumla kuwa bao 1-1.

Comoro nayo, ingawa imefungwa bao 1-0 na Lesotho, imefanikiwa kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1 kufuatia ushindi wa mabao 2-0 ilioupata nyumbani Julai 15, 2017.

Timu hiyo ya visiwani itapambana na Namibia katika raundi ya tatu.

Msumbiji imeshindwa kutamba nyumbani baada ya kukubali kkipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Madagascar, ambayo imesonga mbele kwa jumla ya mabao 4-2 kwani katika mechi ya kwanza mjini Antananarivo timu hizo zilitoka sare ya 2-2.

Madagascar sasa itacheza na Angola ambayo imeshinda 3-2 dhidi ya Mauritius na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4-3 kufuatia sare ya 1-1 katika mechi ya kwanza.

Afrika Kusini imesonga mbele kwa jumla ya mabao 3-0 dhidi ya Botswana kufuatia ushindi wake wa bao 1-0 Jumamosi na sasa itakumbana na Zambia katika raundi ya tatu.

Zambia imesonga mbele kwa jumla ya mabao 7-0 dhidi ya Swaziland baada ya Jumamosi kushinda 3-0. Katika mechi ya kwanza Zambia ilishinda ugenini mabao 4-0.

Mauritania, licha ya kufungwa bao 1-0 nyumbani leo Jumapili, lakini imeifungashia virago Liberia kwa jumla ya mabao 2-1 kufuatia ushindi wake wa ugenini wa mabao 2-0.

Timu hiyo sasa itacheza na Mali, ambayo jana iliitandika Gambia mabao 4-0 na kusonga mbele kwa jumla ya idadi hiyo, kwani mechi yao ya kwanza ilikuwa tasa.

Senegal, ambayo imepata ushindi wa jumla ya mabao 4-2 dhidi ya Sierra Leone, itakutana na Guinea katika  raundi ya tatu.

Awali iliilazimisha Sierra Leone sare ya bao 1-1 na jana ikashinda mabao 3-1 nyumbani.

Guinea nayo imeifunga Guinea-Bissau mabao 7-0 jana na kusonga mbele ka jjumla ya mabao 10-1 kufuatia ushindi wake wa ugenini wa mabao 3-1 Jjulai 15, 2017.

Togo imefuzu kwa mikwaju ya penalty dhidi ya Benin baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya mabao 2-2. Kwanza zilifungana 1-1 na leo zimefungana 1-1.

Kwa matokeo hayo, Togo sasa itakutana na Nigeria katika raundi ya tatu.

Misri itacheza na Morocco katika raundi ya pili, wakati Sao Tome and Principe itacheza na Cameroon.

Ratiba kamili ni hii ifuatayo:

2017-08-11 Senegal vs Guinea

2017-08-11 Egypt vs Morocco

2017-08-11 Sao Tome and Principe vs Cameroon

2017-08-11 Congo vs DR Congo

2017-08-11 Equatorial Guinea vs Gabon

2017-08-11 Algeria vs Libya

2017-08-11 Rwanda vs Uganda

2017-08-11 Togo vs Nigeria

2017-08-11 Comoro vs Namibia

2017-08-11 Afrika Kusini vs Zambia

2017-08-11 Madagascar vs Angola

2017-08-11 Liberia vs Mali

2017-08-11 Niger vs Ivory Coast

2017-08-11 Burkina Faso vs Ghana

2017-08-11 Ethiopia vs Burundi

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *