AJALI mbaya ya aina yake kuwahusisha wasanii, imesababisha vifo vya wasanii 13 wa kundi la muziki wa taarabu la Five Star’s Modern Taarab na kujeruhi wengine saba.

Miongoni mwa waliofariki wamo wanaume kumi na wanawake watatu na wengine saba kujeruhiwa kati yake mmoja vibaya katika ajali iliyohusisha gari yao aina ya Toyota Coaster yenye namba za usajili T 351 BGE iliyokuwa ikiendeshwa na Juma Hassan aliyesalimika na kutoroka.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro SACP Adolfina Chialo, akiongea na majeruhi wa ajali ya wanamuziki wa Five Star’s Modern Taarab.

Imeelezwa kwamba ajali hiyo imetokea baada ya gari lililobeba wasanii hao wakitokea Mbeya, kuelekea jijini Dar es salaam kuacha njia na kulivaa lori lililokuwa limesimama na kupinduka kabla ya kulikwepa na kukutana uso kwa uso na lori lililokuwa likija mbele yao.

Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Morogoro Ibrahim Mwamakula, aliwaambia waandishi wa habari mjini Morogoro kwamba ajali hiyo ilitokea Jumatatu ya Machi 21, saa 2.30 usiku, ndani ya eneo la hifadhi ya taifa ya Mikumi, kilometa karibu sita kutoka lango kuu la kuingilia hifadhi hiyo kutoka upande wa Dodoma.

Kwa mujibu wa Mwamakula aliyefika eneo la tukio na hospitali kusaidia kuhifadhi miili ya watu hao, chanzo cha ajali hiyo ni Mwendo kasi wa gari hiyo aina ya Costa iliyokuwa imewabeba wasanii na uzembe wa dereva Juma kujaribu kulipita gari jingine bila kuwa na uangalifu.

Ajali hiyo ilitokea baada ya Costa hiyo kujaribu kulipita lori aina ya scania lililokuwa limebeba mbao lililokuwa limesimama barabarani baada ya kuharibika lenye namba za usajili T848 APE na tela namba T 556 BDL mali ya Meshack Rajab Mvamba, na kukutana mbele yake na lori aina ya scania lenye namba T 182 BKB na tela namba T 530 BHY ambalo katika kuikwepa Costa hiyo na lenyewe lilipinduka.

Aidha Costa hiyo ilichuna upande mmoja wa lori la mbao, na lenyewe kuharibika upande huo vibaya na kupinduka.

Raisi wa bendi hiyo Ally Juma (25) maarufu kama “Ally J” ambaye ni miongoni mwa majeruhi walionusurika, alisema gari hiyo ilikuwa na watu 24 wakiwemo wasanii 21, madereva wawili na abiria mmoja, na walikuwa wakitokea Mkoani Mbeya kwenye maonesho ambapo Jumapili walifanya wilayani Kyela mkoani humo na kabla, siku ya Ijumaa walifanya maonesho Makambako, Mikumi siku ya alhamisi na Kilosa Mkoani Morogoro siku ya jumatano.

 

Miongoni mwa waliopoteza maisha yumo mwanamuziki Issa Kijoti na kiongozi wa bendi hiyo Nassoro Madenge ambaye ndugu, jamaa na marafiki zake walijitokeza kwa wingi usiku huo katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya mkoa wa Morogoro wakitokea jijini Dar es salaam,na kukesha hadi majira ya saa 10 alfajiri wakiendelea kusaidia zoezi la kushusha miili iliyokuwa imeharibika vibaya kwa kuchanwa na kukatika baadhi ya viungo.

Wengine waliokufa ni waimbaji wa bendi hiyo Husna Mapande na Hamisa Omary ambaye ni mke wa msanii Mussa Mipango, mpiga solo Shebe Juma, mpiga gitaa la base Omary Hashim, mbeba vyombo Omary maarufu kama Toli, Mfanyakazi wa bendi hiyo Ngereza Hassan, wapiga kinanda Tizzo Mgunda na Hamma Kinyoya, mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Maimuna na mcheza shoo wa kundi la “Kitu Tigo” la Ilala ambaye jina lake halijaweza kujulikana mara moja na hao wote walikufa papo hapo katika eneo la ajali.

Mwingine aliyekufa akipelekwa katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu ni Haji Mzaniwa (32) mkazi wa jijini Dar es salaam ambaye ni mbeba vyombo katika bendi hiyo.
Majeruhi katika ajali hiyo waliolazwa katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro ni pamoja na mwimbaji Mkongwe na mgeni aliyekuwa amefanya onesho moja tu katika bendi hiyo, Mwanahawa Ally (55), Suzana Benedict (32),Zena Mohamed (27), Samila Rajab (22), Ally Juma (25), Rajab Kondo (25), Mwanahawa Hamis (38), Shaban Hamis (41) na Msafiri Mussa (22) wote wasanii na wakazi wa jijini Dar es salaam.

Ajali hiyo ilisababisha msururu mrefu wa magari zaidi ya 100 yakiwa yamekwama katika pande zote za njia na kushindwa kupita upande mmoja kwenda mwingine kutokana na ajali hiyo kuzuia njia, huku jitihada za kuwaokoa maiti waliokuwa wamenasa katika Costa hiyo zikiendelea kufanywa na askari wa hifadhi ya Taifa ya Mikumi, watu waliokuwa ndani ya magari yaliyoshindwa kupita na askari polisi waliofika muda mchache baadaye wakiongozwa na Mwamakula.

By Jamii Africa

JamiiForums' Editorial Website | Tanzania's Online News Portal | Dedicated for Public Interest Journalism

Leave a Reply

Your email address will not be published.