WILAYA ya Bahi iliyopo mkoani Dodoma, inakabiliwa na tatizo kubwa la ndoa za utotoni zinazosababisha watoto wa kike kukatishwa masomo yao.
Uchunguzi wa JamboTanzania umebaini kwamba hali hiyo inatokana na tamaa ya baadhi ya wazazi ambao huamua kuwaoza watoto wao kwa uroho au tamaa ya kupata mahali.
Mkuu wa wilaya ya Bahi Betty Mkwasa amesema kuwa baadhi ya wazazi wilayani humo, hudanganyika na tamaa ya kupata mahali bila kujali madhara watakayopata watoto wao hapo baadae.
DC Mkwasa amesema kuwa asilimia kubwa ya watoto wanaozwa kwa wafugaji ambao inadaiwa wana uwezo mkubwa wa kiuchumi kutokana na kumiliki idadi kubwa mifugo.
Amefafanua kuwa jambo la kusikitisha ni kuona kwamba watoto wanaoolewa wengine wana umri mdogo sana kuanzia miaka kumi na moja na wengine hawajamaliza darasa la saba.
Kutokana na tatizo hilo, mkuu huyo wa wilaya ameeleza kuwa tayari ameendesha Oparesheni kabambe kwa kushirikiana na jeshi la polisi kuwasaka wote wanaohusika na vitendo,hivyo ambapo tayari zaidi ya watu watano wamekamatwa na kufikishwa katika mkono wa sheria.
Mkwasa ameongeza kuwa changamoto iliyopo pale washitakiwa wanapofikishwa mahakamani,ni kwamba mashahidi hawafiki kutoa ushahidi kutokana na sababu za kulindana hali ambayo hupelekea kesi hizo kufa.
Amewaonya wakazi wa wilaya hiyo kuacha mara moja kuozesha watoto wao wa kike badala yake,waamke na kuwapatia elimu ili iwasaidie kwa siku za baadae.
Amesema kuwa bado Serikali inaendelea na Oparesheni ya kuwasaka watoto wa kike walioachishwa masomo na wazazi wao kwaajili ya kuwaoza ,ili warudishwe shuleni waweze kuendelea na masomo.
Pia Serikali wilayani Bahi,inaendelea kufanya uchunguzi kuwatafuta watu wote wanaoendeleza vitendo hivyo,pamoja na wale waliotoroka,baada ya kujihusisha kuoa watoto wa shule za msingi.
Kwa upande wake afisa elimu wa wilaya ya Bahi,bibi Maria Methew,anasema kuwa katika kipindi cha mwaka 2013 hadi mwaka 2014 jumla ya watoto wa kike 17 waliokuwa wanasoma katika shule mbalimbali za msingi wilayani Bahi, waliachishwa masomo kutokana na ndoa za utotoni zilizosababisha wapate ujauzito.
Afisa elimu huyo anasema kuwa vitendo hivyo vinahusisha zaidi wanaume wanaotoka makundi ya wafugaji,ambao hutumia fedha zao kuwarubuni wazazi hali ambayo inasababisha watoto wa kike kukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Aidha amefafanua kuwa katika kukabiliana na tatizo hilo kwa sasa kila shule ina mwalimu wa maadili ambaye mara kwa mara anakutana na watoto wa kike na kuzungumza nao mambo mengi ikiwemo kuwaonya wasitumbukie katika tatizo hilo.
Amesema kuwa wamewataka watoto wa kike wanaosoma shule za msingi wilayani humo kutoa taarifa kwa walimu wao wakuu pale wanapoona wazazi wao wanataka kuwaoza ili Serikali iweze kuwachukulia hatua.
Jambo jingine ameeleza kuwa kila shule imeunda klabu kwaajili ya kuwa na midahalo ya wanafunzi kwa lengo la kuzungumzia,upigaji vita ndoa za utotoni pamoja na utoro.
Mfugaji maarufu wilayani Bahi Nkwabi Mabula wa kijiji cha Bahi Makulu amekiri kuwa wapo baadhi ya wafugaji wenzake kutokana na kutokuwa na elimu pamoja na kuendekeza mila potofu wanaoa watoto wadogo.
Amesema kwa mfano baadhi ya wafugaji wa kabila lake la kisukuma,hupenda wanawake weupe ,kwahiyo hata wakiona watoto wadogo wa kike weupe wanaingia tamaa ya kutaka kuoa.
Mabula anasisitiza ipo haja kwa Serikali na asasi binafsi kuyatembelea makundi ya wafugaji katika maeneo mbalimbali ili wawapatie elimu itakayowasaidia waondokane tabia ya kuoa watoto wadogo.
Naye mmoja wa wazazi ambaye alihusika kumuozesha binti yake mwenye umri wa miaka kumi na moja bibi Joyce Mazengo,amekiri kwamba walichukua uamuzi huo kutokana na shinikizo la mume wake ambaye mara baada ya kupokea mahali alitoroka ili kukwepa mkono wa sheria.
Mkazi mwingine wa wilaya hiyo,Athanasi Amani ameongeza kwamba makundi ya wafugaji na jamii za vijijini wilayani humo ni lazima zielimishwe umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike kwani anaamini kwa kufanya hivyo ndoa za utotoni zitakiwisha.