Tanzania na Ushirikishwaji wa Wananchi katika Maendeleo ya Jamii

Innocent Urio

Katika maendeleo yoyote yale ili yawe endelevu na yenye manufaa kama kusudio lake lilivyopangwa, kuna vitu muhimu lazima kuzingataiwa likiwemo hili la ushirikishwaji (participation of community).

Ushirikishwaji katika maendeleo ya jamii ni kitendo ambacho wale waliokusudia kuanzisha mradi wa maendeleo katika eneo fulani huwashirikisha wananchi husika (hasa wale ambao ule mradi umewalenga) ili kujaribu kupunguza vikwazo katika ufanikishaji wa mradi huo. Ushirikishwaji huo utakuwa katika nyanja kama; upangaji mikakati (strategic planning), huduma zitatolewaje, pamoja na mambo mengine yanayofanana na hayo ili mradi tu yawe yanaendeleza mradi.

Nia kubwa ya kuamua kulizungumzia hili suala ni kujaribu kufikisha ujumbe kwa wahusika ikiwemo serikali (decision makers) ili kujaribu kuangalia upya swala la ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo. Watendaji katika Serikali yetu ya Tanzania wamekuwa wavivu sana katika kuwashirikisha wananchi katika miradi mbalimabali ya maendeleo hivyo kuifanya miradi hiyo isifanikiwe kama kengo lake lilivyopangwa. Hii inawafanya wananchi kutokuwa na mipango mkakati ya kuitumia miradi inayotekelezwa katika maeneo yao ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa wakati wa utekelezwaji wa hiyo miradi. Mradi kama ‘Machinga Complex’ ni picha halisi ya jambo ninalozungumzia.

Kwahiyo, swala la ushirikiswaji linaweza kuwa chachu ya maendeleo hata kama liwe kwa muda mfupi kwa mfano jinsi TCRA walivyojaribu kuwashirikisha wananchi katika dakika za mwisho za uzimaji wa mitambo ya analojia hapa Tanzania mwishoni mwa mwaka jana (2012). Walijaribu kutoa miongozo na maelezo kwa njia tofautitofauti vikiwemo vyombo vya habari kupitia matangazo, vipindi maalum, midahalo, makala, pamoja na nyimbo kitu ambacho kiliamsha hisia za watanzania walio wengi na kuamua kuhamia digitali japokuwa kuna changamoto nyingi.

Lakini, kwa upande mwingine wananchi nao wako nyuma sana kwani hawataki kujihusisha na mambo muhimu ambayo serikali yao inawaletea mitaani kwao; wengi husingizia kuwa na majukumu mengi sana hadi kushindwa kushiriki kikamilifu katika miradi na hata kushindwa kuishinikiza serikali iwashirikishe au iitekeleze miradi kwa mujibu wa mipango mkakati.

 JE, USHIRIKISHWAJI UNA FAIDA GANI?

Faida za ushiriklishwaji ziko nyingi sana na ni muhimu kama tunataka kweli kuleta maendeleo endelevu hapa nchini kwetu Tanzania. Faida hizo zinamuelekea mwananchi moja kwa moja pamoja na serikali au wenye miradi kama ifuatavyo;

Ø  Unapunguza vikwazo kutoka kwa wananchi husika wa eneo lile kutokana na wao kuwa na uelewa na kinachoendelea na nini hatima yao mwishoni mwa mradi

Ø  Ushirikishwaji pia unaleta ile hali ya ulinzi (sense of security) pale ambapo kila mmoja anakuwa katika hali ya kuulinda ule mradi kwa sababu anajua nini hasa lengo la kile kanachotendeka pale.

Ø  Umiliki wa ule mradi unakuwa wa Jamii, kitu ambacho kitasaidia ule mradi kuwa salama na endelevu kwa kua kila mwananchi atakuwa ameutunza kama wake kutokana na ile hali ya ushirikishwaji kabla ya kuanza kwa mradi.

Ø  Ushirikishwaji pia utasaidia kufikiwa kwa lengo ambalo waandaaji wa ule mradi waliukusudia

Ø  Itasaidia pia kuzingatia swala la utamaduni wa wazawa ili kuzuia uvunzaji wa miiko ya jamii husika.

TAFAKARI: KUNA UMUHIMU MKUBWA SANA WA KUSHIRIKISHWA KULIKO HASARA JAPO KUA HAKUNA KISICHOKUWA NA FAIDA NA HASARA.

KUNA HASARA PIA KUWASHIRIKISHA

 Nazo ni

  • Kupoteza muda mwingi
  • Vipingamizi vitakuwa vingi
  • Kuna watu wengine watapuuzia

JE, NANI WAKULAUMIWA?

Kutokana na hali ilivyo sasa hasa Tanzania na nchi nyingi za kiafrika, tukimtafuta mchawi ni nani tutakamatana wenyewe na kulaumiana lakini chanzo cha tatizo haliko kwetu tu ila ni kwa dunia nzima. Ukijaribu kupitia vitabu mbalimbali vya sayansi ya jamii utabaini kuwa kuna kitu ambacho kinatutenganisha sisi na serikali yetu pamoja na wananchi wengine. Mwanasayansi ya jamii mmoja anayefahaamika kwa jina la Karl Marx alisema kuwa kupotea kwa nguvu kazi ya pamoja kumeteketezwa na mfumo wa kibepari ambao umetawala dunia kwa sasa. Naam, ubepari kimekuwa chanzo kikuu cha utengano!

Katika ubepari huwa kuna kauli moja wanaitumia ambayo inasema ‘EVERY THING IS FOR YOUR SELF BUT GOD ONLY IS FOR US ALL’ kitu ambacho kinatutenganisha sisi wote hadi hata miradi inavyoletwa  kwenye maeneo yetu tunashindwa kushirikishwa kutokana na kila mtu anakuwa akifuatilia maisha yake mwenyewe kwasababu hakuna atayemsaidia zaidi ya kumcheka na kumsengenya pale atakapokuwa amekosea.  KWA MAANA HIYO TUNAGUNDUA KUA UPEPARI UNAOIMARISHWA NA UTANDAWAZI NDIO CHANZO KIKUU CHA TATIZO HILI KATIKA NCHI YETU AMBAYO NI CHANGA BADO KIUCHUMI LAKINI IKIWA NI MOJA KATI YA NCHI KONGWE KATIKA BARA LA AFRICKA.

NINI KIFANYIKE?

Hapa watanzania na waafrika kwa ujumla inabidi tuziamshe akili zetu na tujaribu kuangalia nyuma tulikosea wapi ili tupange mikakati ambayo itaweza kutukwamua hapa tulipo.

Nikijaribu kuiangalia Tanzania kisayansi ya Jamii, kidogo nagundua kuwa mfumo wa maendeleo ambao tunautumia ni kama ule WW Rostow aliutoa katika nadharia (theory) moja ianyoitwa ‘modernization’ ambayo inatutaka ‘Ili tufikie walipofikia wenzetu wa Marekani na wa Ulaya, lazima tupitie hatua ambazo wao walizipitia ikiwa ni kutoka low stage ambayo wanaiita traditional stage, alafu tufuate hatua ya pili ambayo ni pre-condition stage, alafu tuendelee na take off stage ambayo kidogo mafanikio yanaanza kuonekana kwenye hatua hii alafu hatua ya nne ni drive to mature stage ambayo watu waanza kuwekeza katika viwanda vikubwa na hatua ya mwisho ni high mass consumption ambayo watu wanawekeza nje ya nchi zao na wanakuwa na vipato vikubwa’.

Sasa kwa sisi watanzania kweli tunafuata hizo hatua (stages) lakini tunakosea kitu kimoja ambacho kinatufanya sisi tuwe nyuma kimaendeleo. Kitu hicho ni kuwa tunafuata hatua kweli lakini mambo ambayo tunayafanya yanakuwa yamevuka ile hatua tulio nayo. Ni sawa na mtoto wa miaka mitano anaanza kuchumbia mwanamke ili kuoa.

Tumeamua kujiingiza kwenye masuala ambayo tusingetakiwa kuyaruhusu kwa wakati huu hadi pale ambapo tungekua angalau tumefikia kwenye take off ya ukweli. Hii ni kwa sababu wenzetu walifanya hivyo wakafanikiwa na kwakua hata wewe ukiendelea hutaki mwenzako akupite basi unaamua kumdanganya ili ajiingize katika mambo ambayo yatakua mzigo kwake baadaye ili uendelee kutamba; hivyo ndivyo wanavyotufanyia wazungu ili tuzidi kushindwa zaidi. Kikubwa kilicho tufanya hadi tukafikia hatua hiyo ya kujiingiza kweye mambo yasio ya uwezo wetu ni swala zima la utandawazi tulio upokea kwa kwa mikono miwili enzi za serekali ya awamu ya tatu. Wanasayansi walisha sema wazi kuwa ili utandawazi uifanikishe nchi na wananchi wake ni lazima nchi hiyo iwe na uchumi mzuri na wa ushindani zaidi ya hapo utandawazio huo unakua ni hatari.  Utandawazi huo ndio umekua chombo au silaha ya ubepari kututeganisha sisi kwa sisi na serikali yetundio maana hata ushirikiswaji wetu kwenye shughuli za maendeleo ya jamii yetu unakua haupo na kama ukiwepo unakua si wa moja kwa moja.

MAPENDEKEZO

Inabidi watanzania tuamke na tujaribu kufikiria njia sahihi ambazo tunaweza kuzitumia hasa katika mfumo huu huu wa kibepari ili kuleta maendeleo yetu wenyewe. Tunatakiwa kuishinikiza serikali kutengeneza msingi imara wa uchumi (strong economic base) ambao utatokana na rasilimali zetu tulizo nazo kama hizi za gesi na madini. tatafanikiwa hili  kwa kutowekeza muwekezaji yeyote yule isipokuwa serikali ndo iwe mmiliki na muuzaji wa hizi rasilimali ili ziwe uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu ambapo mwisho wa siku serikali hiyohiyo itakuwa imepata kipato kikubwa cha kutuendeleza sisi kuliko serikali kutegemea kodi kama chanzo cha mapato.

Ukweli unabaki kwamba bila kushirikishwa kikamilifu katika shughuli nzima za maendeleo yetu wenyewe  tutazidi kuwa masikini na ongezeko kubwa la watu wanaoishi katika mazingira magumu na matatizo mengine ya kijamii hivyo serikali inabidi ichukue hatua mahususi ili kujaribu kufanya jambo ambalo linahitajika na watanzania walio wengi hasa wa hali ya chini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *