TEHAMA: Tanzania bado tuna safari ndefu

Gabriel Shewio
wanafunzi wa wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari ya Makumbusho jijini Dar es Salaam

MAENDELEO ya dunia ya sasa yanakimbia haraka. Yanabadilika kila dakika na hakika, hayasubiri anayejongea. Mabadiliko haya makubwa ya dunia, yanatokana na kukua kwa teknolojia na mapinduzi ya kompyuta.

Teknolojia inayoiweka dunia kwenye mabadiliko makubwa ipo katika kilimo, elimu, afya, usafiri na sekta zingine muhimu kwa maendeleo.

Hivi sasa sekta nyingi zinatumia teknolojia ya kompyuta ili kurahisisha kazi na kuwa na matokeo mazuri na yenye uhakika. Katika kutambua na kuendana na kasi hiyo ya maendeleo, Tanzania imejizatiti kuhakikisha haiachwi nyuma.

Ndiyo maana serikali kwa kuona umuhimu huo, ililazimika kuandaa mtaala rasmi utakaohakikisha nchi inapata wasomi watakaoweza kutumia teknolojia kurahisisha kazi.

Waziri wa Mawasiliano, Sayansi Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa anasema Tanzania haitabaki nyuma kuwekeza kwenye teknolojia.

“Serikali inatambua umuhimu wa teknolojia na matumizi ya kompyuta ili kuyafikia maendeleo ya haraka, na kwa kweli bila teknolojia, nchi inaweza kuwa nyuma mno katika maendeleo ya sasa,” anasema Profesa Mbarawa akizungumza na FikraPevu.

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa Tehama (Teknolojia Habari na Mawasiliano), Dar es Salaam, Profesa Mbarawa alisema wataamu wa sasa lazima watumie teknolojia ili wapate matokeo makubwa na mazuri kwa wakati mfupi.

Profesa Mbarawa alisema Serikali inaendelea kuwekeza katika Tehama ili kuhakikisha nchi inafikia maendeleo makubwa ya haraka.

Naye Waziri wa Elimu na Mfunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, anasema kuwa kwa kutambua umuhimu wa sayansi na teknolojia, Tanzania iliamua kuanzisha masomo ya eneo hilo kuanzia mwaka 2000.

Anasema mafunzo kwa masomo hayo kunahakikisha wanafunzi kupata muda wa kufanya mazoezi ya nadharia pamoja na vitendo pia kupewa mitihani.

Hata hivyo, tangu kuanzishwa kwa mpango huu mpaka sasa, zaidi ya miaka 15 imepita,  mwitikio wa shule nyingi kufundisha masomo ya teknolojia na kompyuta, umekuwa mdogo.

wanafunzi-wa-sekondari-ya-mpunyule-wilayani-kilwa-wakijifunza-somo-la-tehama

Wanafunzi wa sekondari ya Mpunyule iliyopo wilayani Kilwa wakijifunza somo la TEHAMA

Mpaka sasa idadi ya shule za sekondari zinazofundisha masomo hayo na kufanya mitihani yake ni 148 sawa na asilimia 3% ya shule zote. Tanzania ina zaidi ya shule za sekondari 4460.

Pamoja na shule chache kuitikia mwito wa kufundisha masomo yaho, bado mazingira na miundombinu wezeshi, kuwafanya wanafunzi kuelewa na kufurahia masomo hayo, ni duni kwa baadhi ya shule.

Zipo baadhi ya shule ambazo zimetilia mkazo mkubwa wa masomo haya ya Tehama. Zikiwa na maabara za kompyuta zenye vifaa vya kutosha kwa mafunzo hayo.

Shule hizo zimetilia mkazo pia kwa kuajiri walimu wenye sifa za kufundisha masomo hayo, hivyo kufanya wanafunzi kupenda na kufurahia masomo.

Miongoni mwa shule za sekondari zinasofundisha Tehama ni pamoja na Wiza. Shule hii iliyoko Mji wa Vwawa, Mbozi, mkoani Mbeya, imekuwa miongoni mwa shule zinazofanya vizuri kwa kuwa ina walimu wa kutosha na sifa za kufundisha  masomo hayo.

Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Padre Francis Magala anasema kuwa shule yake kwa kuzingatia umuhimu wa masomo ya Tehama, iliamua kuwekeza katika masomo hayo ili kuwa na wahitimu wenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya Tanzania.

Taarifa zinaonesha kuwa shule nyingi zinazotangaza kufundisha masomo ya Tehama, hazina walimu wa kutosha na kama wapo, basi hawana ujuzi unaotakiwa.

Wanafunzi wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari ya Makumbusho jijini Dar es Salaam

Wanafunzi wa Kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari ya Makumbusho jijini Dar es Salaam wakijifunza somo la TEHAMA

Aidha, imebainika shule kadhaa zikiwa na kompyuta moja, lakini zikiaminisha umma kuwa zina maabara na walimu wa Tehama.

Je, wanafunzi wanawezaje kuelewa masomo ya Tehama, ikiwa shule ina kompyuta moja? Au kuwa na walimu wasiokuwa na ujuzi zaidi ya kuwasha na kuzima kompyuta?

Tangu mwaka 2011, kumekuwepo kilio cha wanafunzi waishio vijijini kutengwa katika utolewaji wa mafunzo ya Tehama. Changamoto nyingi zilizoainishwa wakati huo bado zinaendelea kuwepo hadi leo, miaka mitano baadaye.

Aidha, mwaka 2012 wadau waliitaka Serikali kuweka mipango madhubuti ili Tanzania iweze kuingia katika ushindani na mataifa mengine kuliko hali iliyokuwepo wakati huo ambapo wanafunzi walikuwa wakijfunza kwa nadharia tu.

Bado kuna safari ndefu kwa Tanzania kuwa na wajuzi wa Tehama, watakaotoa mchango unaokwenda sanjari na mabadiliko makubwa ya maendeleo “yanayoendeshwa” kwa teknolojia.

Ni vyema sasa, serikali ikahakikisha kuwa inawekeza katika vifaa, walimu na miundombinu inayorahisisha mafunzo ya Tehama kwa wanafunzi wote.

Pia ni vyema kwa serikali kuhakikisha; ama inapunguza kodi au kuiondoa kabisa kwa vifaa vyote vinavyoendana na mafunzo ya Tehama; iwe katika shule, vyuo ama watu binafsi ili kuzidisha chachu ya kuwepo kwa wajuzi wa masomo hayo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *