Teknolojia mpya kuthibiti wizi wa fedha mtandaoni

Jamii Africa

Ukuaji wa teknolojia na kuvumbuliwa kwa njia za kisasa katika sekta ya habari na mawasiliano, kumerahisisha upatikanaji wa huduma za fedha kwa njia ya simu ambapo watu hawalazimiki tena kutunza fedha zao benki.

Hali hiyo inachagizwa na ongezeko la watu wanaotumia simu za mkononi na kuletwa kwa teknolojia ya simu ambayo inawawezesha watumiaji kutunza na kufanya miamala ya fedha.

Kulingana na ripoti ya Benki ya Uwekezaji Ulaya (European investment bank ,2015) imeainisha  Afrika kuongoza duniani kwa matumizi ya Simu za viganjani kufanya miamala ya fedha. Kwa Upande wa Afrika Mashariki, nchi ya Kenya wananchi 6 kati ya 10 (62%) ya watu wake wamekua wakitumia simu za viganjani kufanya miamala ya kifedha.

 Teknolojia hiyo imeleta changamoto mbalimbali ambapo watu wenye nia mbaya huitumia kujipatia fedha kwa njia zisizo halali kutoka kwa watumiaji wa mtandao.

Licha ya matukio  ya wizi wa fedha kwa njia ya mtandao kupungua nchini ikilinganishwa na miaka iliyopita, wizi wa fedha kwa miamala ya simu umeonekana kushika kasi huku mkoa wa Dar es salaam ukiwa katika nafasi ya juu ukifuatiwa na mkoa wa Mwanza.

Taarifa na takwimu za matukio ya wizi wa mtandao zilizotolewa na Jeshi la Polisi nchini, zinathibitisha kuwa kuanzia Oktoba 2016 hadi Machi 2017 mkoa wa Dar es salaam ulikuwa na matukio 1,423 ya wizi wa fedha kwa njia ya mtandao wa simu huku ukifuatiwa kwa mbali na mkoa wa Mwanza ambao ulikuwa na matukio 659.

 Mikoa mingine inayotajwa kuwa na matukio mengi ya wizi wa fedha kwa njia ya simu ni Arusha, Dodoma, Morogoro na Mjini Magharibi (Zanzibar).

Kulingana na Takwimu za Jeshi la Polisi kulikuwa na matukio 5,253 ya wizi wa fedha kwenye mtandao wa simu katika mikoa 19 ya Tanzania Bara na Visiwani.  Zaidi ya robo tatu ya matukio hayo yalitokea katika  mkoa wa Dar es salaam ambapo ni sawa na asilimia 27 ya matukio yote.

Matukio hayo ya Dar es salaam ni pungufu kidogo ya matukio yaliyotokea katika mikoa mitatu  ya Mwanza, Mjini Magharibi na Dodoma  (1,648) . Tofauti hiyo kubwa ya mkoa wa Dar es salaam ikilinganishwa na mikoa mingine inatajwa kuchochewa na ongezeko la idadi ya watu wengi wanaotumia miamala ya simu kuliko taasisi nyingine za fedha zikiwemo benki.

Ndani ya mkoa wa Dar es salaam pia kuna tofauti kubwa kutoka wilaya moja hadi wilaya nyingine. Mathalani Wilaya ya Kionondoni ilikuwa na matukio 1,303 ikifuatiwa kwa mbali na Wilaya ya Temeke (101) na Ilala (19).

Tofauti hii inaweza kuthibitisha kuwa tatizo la wizi wa fedha kwa njia ya mtandao wa simu ni kubwa zaidi katika wilaya ya Kinondoni kuliko maeneo mengine ya nchi.

Takwimu hizo za Jeshi la Polisi nchini zinaonyesha kuwa mikoa ya Geita, Tabora, Mtwara, Iringa, Tanga,  Manyara na Kigoma ilikuwa na matukio machache.

Kutokana na wizi huo wa mtandao baadhi ya watu wamekamatwa na kufikishwa mahakamani na kuchukuliwa hatua huku kesi nyingine zikiwa chini ya upepelezi.

Kauli ya Jeshi la Polisi

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, ACP Barnaba Mwakalukwa amesema matukio mengi ya wizi wa mtandao yanatokeo katika miji mikubwa kama Dar es Salaam na Mwanza kwasababu miji hiyo ina idadi kubwa ya watu na shughuli nyingi za kiuchumi ambapo ni changamoto katika matumizi sahihi ya mitandao.

"Unaweza kuuliza kwa nini Mwanza, ule mji umekua kuna wafanyabiashara wakubwa, wahalifu nao wanabuni mbinu mpya," amesema ACP Mwakalukwa.

Kwa upande wake,  Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Hamza Hassan amewataka watumiaji wa mitandao ya simu kuzingatia sheria ya makosa ya mtandao  ili kujiepusha na matukio ya wizi ambayo yanaweza kuwatia hatiani na kuleta hasara kwa taifa.

"Unaweza kufanya jambo leo mtandaoni halafu athari zake zikaanza kuonekana baada ya miaka kadhaa, tuitumie vyema mitandao na elimu zaidi itolewe kwa wananchi," amesema.

Hata hivyo kwa nyakati tofauti, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikishirikiana na kampuni za simu nchini imeendelea kutoa elimu na tahadhari kwa watumiaji wa simu za mkononi kuwa makini na matapeli ambao hutumia ujumbe wa simu kujipatia fedha kwa udanganyifu. Pia watumiaji wa simu wametakiwa kujiridhisha kabla ya kutuma fedha kwa mtu wasiyemfahamu.

Kupitia sheria ya Makosa ya Mtandao (CyberCrime Act, 2015), wale wote wanaojihusisha na matukio ya kudanganya au kujipatia fedha isivyo halali kwa njia ya mtandao wanaweza kukabiliwa na adhabu ya kulipa fidia isiyopungua milioni 20 au  kufungwa jela miaka isiyopungua saba (7) au vyote kwa pamoja.

Ripoti ya shirika linaloangazia wizi unaotokea katika mitandao (ACFE, The Nationals on occupational Fraud and abuse,2016)  inaeleza kuwa kesi 2,410 zimelipotiwa katika nchi 114 ambapo dola bilioni 6.3 zimepotea kutokana na wizi wa mtandao.

Katika ukanda wa Afrika Mashariki nchini ya Kenya inaongoza kuwa na matukio mengi ya wizi wa mtandao kupitia simu. Kila mwaka nchi hiyo inapoteza kiasi cha Shilingi bilioni 5 za Kenya (Dola milioni 50) na kiasi hicho kinaendelea kuongezeka.

Jinsi ya Kupambana na Wizi wa mtandaoni

Kituo cha Usalama cha kampuni ya Google kinawashauri watumiaji wa mtandao kuwa waangalifu dhidi ya ujumbe wowote au tovuti zinazowauliza maelezo yao binafsi, au ujumbe unaowaelekeza kwenye ukurasa wa wavuti wasioufahamu na unaouliza maelezo yoyote kati ya yafuatayo: majina ya mtumiaji, manenosiri, nambari za usalama wa jamii, nambari za akaunti ya benki, PINs (Nambari Binafsi za Utambulisho) na Siku yako ya kuzaliwa.

“Pia Ukiona ujumbe kutoka kwa mtu unayemfahamu ambao hauonekani kama umetumwa na yeye, huenda akaunti yake imevamiwa na mhalifu wa mtandaoni ambaye anajaribu kupata pesa au maelezo kutoka kwako – hivyo kuwa mwangalifu jinsi unavyojibu”.

Watumiaji wanashauriwa wasitume nenosiri kupitia barua pepe na kuwashirikisha watu wengine na

 “Manenosiri yako ni ufunguo wa akaunti zako na huduma mtandaoni, na kama ilivyo katika maisha nje ya mtandao, unapaswa kuwa mwangalifu na unayempa fungua zako. Tovuti na huduma halali hazitakuuliza uwatumie manenosiri yako kupitia barua pepe, hivyo ukipata maombi ya kutuma manenosiri unayotumia katika tovuti fulani, usijibu”.

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *