Utafiti wa Twaweza: Elimu Bure bado ina Changamoto

Jamii Africa

Kati ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano ni utoaji wa Elimu bure. Lengo la Rais John Pombe Magufuli ni kupanua wigo na kuhakikisha elimu inapatikana kwa wote hasa uboreshaji wa elimu ya msingi.

Sera ya elimu bila malipo ya ada kuanzia ngazi ya awali hadi sekondari inaonekana kuongeza viwango vya uandikishaji wa wanafunzi kwa hali ya juu. Hii ni kwa sababu vikwazo vyote vya uandikishaji vimeondolewa.

Lakini je, ni kwa kiasi gani mfumo wa elimu nchini umejipanga kuwezesha ongezeko la wanafunzi kwenye shule za serikali kujifunza na kupata stadi tarajiwa? Au nchi itabaki katika upatikanaji wa bora elimu kwa wengi, na si kuhakikisha ubora wa elimu kama wananchi wengi waonavyo?

Licha ya ongezeko la Bajeti ya Elimu mwaka 2016/2017 kuwa jumla ya shilingi trilioni 4.77 kulinganisha na trilioni 3.887 zilizotengwa mwaka 2015/2016, ikiwa ni ongezeko la asilimia 81.3, bado elimu katika shule za serikali sio bora.

Fikrapevu imepata maoni ya watanzania wakiongelea hali ya elimu bure nchini, hii ikiwa ni utafiti wa Sauti za Wananchi uliofanywa na shirika la Twaweza Agosti 2016, uliojulikana kama ‘Hali Halisi: Maoni ya Wananchi juu ya elimu bila malipo ya ada’

Utafiti huu unaonesha serikali kuwekeza zaidi katika kutatua changamoto za miundombinu kama vile madawati na madarasa.Ubora na njia za ufundishaji kwa wanafunzi ambao idadi imeongezeka maradufu hasa shule za msingi ukilinganisha na siku za nyuma bado haujaboreshwa.

Tatizo la walimu linatajwa na wananchi wengi ikiwa ni changamoto ambayo idadi ya wanafunzi ni kubwa kulinganisha na walimu wanaofundisha. Mwananchi mmoja kati ya watatu anataja upungufu wa walimu (asilimia 34) na madawati (asilimia 30) kama changamoto kubwa zinazokabili shule za serikali nchini.

Changamoto zingine zilizobainishwa ni za muda mrefu tangu miaka ya nyuma, kama vile ukosefu wa vyumba vya madarasa, vitabu, walimu kutofundisha vizuri, huku wengine wakitaja suala la ukosefu wa chakula shuleni kuwa ni tatizo kwa shule za selikali.

Aidha elimu ya katika shule za binafsi inaelezwa kuwa na ubora kuliko serikalini kutokana na uendeshaji wenye uwiano kati ya walimu na wanafunzi darasani na miundombinu.

Wananchi 5 kati ya kumi wanasema ubora wa elimu katika shule za binafsi za msingi na sekondari ni nzuri, huku wananchi 2 tu kati ya kumi wakiwa na mtazamo kama huo kwa shule za serikali.

Asilimia 45% ya wananchi waliotoa maoni yao wanasema shule binafsi zinatoa elimu bora kulinganisha na za serikali, huku asilimia 34 pekee wakisema shule za serikali nazo zinajitahidi.

unnamed

Vilevile, utafiti huu umebainisha juu ya nafasi ya wazazi kwa watoto wao katika kuchangia maendeleo kwenye sekta ya elimu na si kuwaacha peke yao katika kila maamuzi.

Wazazi wana jukumu kubwa la kuwatia moyo na kuwawezesha watoto wao kufanikiwa, kwa kufuatilia utekelezaji wa sera za serikali na kuwawajibisha walimu na uongozi wa shule ili kuboresha matokeo ya ufundishaji na kujifunza.

Katika kumbukumbu ambazo Fikrapevu imewahi kuandika, inaonesha katika familia ambazo wazazi wameelimika kuna watoto wenye uwezo mzuri wa ufaulu kulinganisha na wale ambao wazazi wao hawana elimu hasa akina mama ambao wana muda wa kutosha wa kukaa na watoto wao.

Vilevile taasisi hii ya Twaweza katika utafiti wa mwaka 2015 katika sekta ya Elimu Tanzania “ Mwanga mpya? ” ilionesha jinsi wananchi wanavyoupokea muhtasari wa elimu bure nchini kuwa ni chagizo la kigezo cha wanafunzi kutopata elimu bora.

Katika utafiti huu, wananchi wanasema elimu bure haikidhi mahitaji kwani kuna huduma nyingine hazifikiwi kutokana na fedha kutojitosheleza ukilinganisha na shule za binafsi zinazolipa kiasi kikubwa cha fedha na hivyo elimu inayotolewa kuwa bora kwani hujitosheleza kukidhi mahitaji muhimu.

Huku wengine wakiwa hawaoni matunda ya elimu bure kwenye kipindi cha mwaka mmoja wa mwanzo, wapo wanaoona maboresho yakitendeka.

Baadhi ya wananchi walipoulizwa ubora wa elimu katika shule za serikali kufuatia tamko la elimu bila malipo ada, asilimia 50 walisema wanaamini ubora wa elimu umeongezeka, asilimia 35 walisema umebaki palepale na asilimia 15 waliamini kuwa umeshuka.

unnamed-1

Licha ya changamoto za elimu inayotolewa katika shule za serikali kuonekana kuzorotesha ustadi kwa wanafunzi, vilevile suala la wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito kurudishwa shuleni baada ya kujifungua, limepewa kipaumbele na wananchi katika kuhakikisha ndoto zao zinatimia.

Zaidi ya wananchi 7 kati ya 10 wanasema wasichana walioacha shule kutokana na ujauzito warudi shuleni baada ya kujifungua.

Kuandikisha watoto wengi shuleni kuna faida endapo tu kutakuwa na miundombinu ya kutosha na walimu. Vifaa stahiki na mazingira ya kujifunzia yanahitaji kuboreshwa ili kuhakikisha walengwa wanajifunza ili kuondoa kujirudia kwa historia ya kufeli kwa wanafunzi.

Kwa namna ambavyo serikali inavyoendelea kutoa kipaumbele katika utoaji wa huduma kwa wananchi, sekta ya elimu inapaswa kuangaliwa upya ili kuhakikisha mtaala mzima wa ufundishaji unafuatwa na kuondoa uhaba wa wafundishaji wa masomo lengwa na si wingi wa wanafunzi tu shuleni.

Lakini azma hii ya kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari inapaswa kuangaliwa upya jinsi inavyotekelezwa, kwani elimu bure inaweza isizalishe elimu bora kwa kukosa rasilimali zinajitosheleza kwa ajili ya kufufua elimu na kupandikiza stadi za maisha na badala yake shule za binafsi zikabaki kuwa kimbilio la wachache wenye kujiweza kiuchumi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *